Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao akiwasha
Mshumaa wa Pasaka wakati wa Misa ya mkesha wa Pasaka uliofanyika kwenye
Kanisa la Kuu la Makatifu Joseph, Zanzibar jana
Ni katika waraka maalumu unaoitwa ‘Ujumbe wa kichungaji wa Pasaka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema.
Maaskofu 32 wa
Kanisa Katoliki Tanzania, wametoa waraka maalumu wa Pasaka wakiwataka
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuheshimu maoni ya Watanzania
yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kuweka pembeni itikadi za kisiasa
katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
Kupitia tamko lao la pamoja walilolitoa jana na
kulipa jina la “Ujumbe wa kichungaji wa Pasaka kwa waamini na watu wote
wenye mapenzi mema,” maaskofu hao walisema hivi sasa kuna makundi yenye
nguvu ambayo yameanza kushinikiza kuingizwa mambo yenye masilahi kwao
kwenye Katiba Mpya.
“Tunalisihi na kulishauri Bunge Maalumu la Katiba
kuheshimu mawazo yaliyowasilishwa na kutumia busara zilizopendekezwa za
kujenga muundo wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya utangamano,
mshikamano, amani, maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi na raia wa
Tanzania,” walisema katika tamko hilo ambalo, Makamu wa Rais wa TEC,
Askofu Severine Niwemugizi alithibitisha kuwa umetolewa na kanisa hilo.
Kauli ya viongozi hao ambayo ilisomwa katika
makanisa mbalimbali nchini jana, imekuja ikiwa zimepita siku sita tangu
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vya Bunge Maalumu la
Katiba kutokana na mvutano unaoendelea juu ya hoja ya muundo wa
Serikali.
Tangu kuanza kwa Bunge hilo kumekuwa na mvutano
kuhusu muundo wa Serikali, huku CCM kikiupinga muundo wa serikali tatu
uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kutaka muundo wa
serikali mbili, ambao unapingwa na upinzani.
“Kazi ya kuandika Katiba ni ngumu na haishangazi
kuona migongano ya hoja kwa makundi kinzani. Mawazo ya wengi
yamewasilishwa kisheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya
kujadiliwa na Bunge Maalumu la Katiba,” inasomeka sehemu ya tamko hilo
ambalo limechapishwa kwa ukamilifu katika ukurasa wa 6 wa gazeti hili na
kuongeza:
“Sasa, tunashuhudia makundi yenye nguvu yakijaribu
kushinikiza kuingizwa matakwa yake kwenye Katiba kwa njia zozote zile
ili kujihakikishia kuendelea kulinda masilahi yake ya kisiasa.”
Maaskofu hao ambao majina yao yameorodheshwa
kwenye waraka huo, wamewataka wajumbe wa Bunge hilo kuachana na itikadi
za kisiasa ili kufikia mwafaka katika masuala muhimu
yatakayowahakikishia raia wa kawaida kushiriki kwenye fursa za maendeleo
kwa manufaa ya wote.
Huku wakitolea mfano umoja, amani na utulivu
nchini ambao umekuwa kimbilio kwa mataifa mengine, walisema hivi sasa
kuna dosari kadhaa katika umoja wa Watanzania.
“Kupungua kwa hisia za kujisikia watu wote ni
taifa moja, ni dosari iliyoanza kukua taratibu na sasa inaonekana kuwa
ndiyo ukweli,” walisema.
Walisema kasoro zilizojitokeza katika mambo
mbalimbali ndiyo chanzo cha watu kutaka mabadiliko: “Watu wengi walitaka
na wanataka mabadiliko au mageuzi ya msingi. Kwa msukumo huo ndiyo
sababu ya kuingia katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.”
Walisema Watanzania hawatakiwi kukata tamaa, huku wakiwakata
watu wenye nia njema kushirikiana na kupambana na nguvu za maovu na
ubinafsi na kuachana na itikadi za kisiasa ili kupigania haki za
wanyonge.
“Tuandae Katiba ambayo itatupatia misingi imara ya
maadili itakayotuongoza kupigana dhidi ya ubinafsi na ufisadi na
kutetea haki za binadamu kwa wote,” walisema.
Hata hivyo, walisema iwapo utakuwapo muafaka na
kukubaliana katika mambo muhimu kwa maisha ya mshikamano wa kitaifa
ambayo katika Rasimu ya Katiba yameandikwa kwenye sura ya kwanza hadi ya
tano, muundo wowote wa serikali unawezekana.
Walisema ili kufikia lengo la kuwa na Katiba bora
ni lazima maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaheshimiwe kama ambavyo
imetamka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kuwe na nia njema ya kutafuta suluhisho la
matatizo mengi ya utendaji katika dola zilizopo katika Muungano,
kutokuwa wabinafsi pamoja na kuchambua matatizo ya sasa ya Muungano na
kuridhia mfumo utakaomaliza matatizo hayo,” walisema.
Akizungumzia waraka huo, Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema ameusikia ukisomwa na Askofu
Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar na kuelezea kufurahishwa na
yaliyomo.
Malasusa aonya
Kwa upande wake Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa alisema wanasiasa
wanatakiwa kutambua kuwa Katiba Mpya si mali yao, bali ya Watanzania
wote.
Akizungumza katika ibada ya Pasaka katika Kanisa
la Azania Front jana Malasusa ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya
Mashariki na Pwani, alisema: “Katiba Mpya itapatikana kama watu
wakiheshimiana, kuridhiana na kuaminiana. Waliapa kufanya kazi bila
upendeleo na hilo ni lazima walizingatie.”
Alisema kazi ya kuandika Katiba ni ngumu na kwamba
licha ya misuguano ya wajumbe wa Bunge hilo bado wanatakiwa kuweka
tofauti zao za kisiasa pembeni na kufikiria mustakabali wa taifa.
“Hatupendi kuona kundi lililoshindwa na lililoshinda. Tunachotaka kukiona ni Katiba itakayowaweka Watanzania pamoja,” alisema.
Ibada hiyo iliyofanyika kitaifa katika kanisa hilo
ilihudhuriwa na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Mkuu wa
Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Ernest Mangu.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment