Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » WAZIRI LUKUVI AKLIWA KOONI

WAZIRI LUKUVI AKLIWA KOONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
 
Jumuiya  ya Vijana wa Chama cha Wananchi-CUF (JUVICUF) na Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema (Bavicha), vimemtaka Rais Jakaya Kikwete, kumfuta uwaziri Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kwa madai kwamba anatumia nafasi hiyo kuwagawa Watanzania na kutoa vitisho visivyokuwa vya msingi.
Mbali na kutaka Lukuvi afutwe uwaziri, vijana hao pia wanataka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anayedaiwa kumtuma Lukuvi kwenda kuhubiri udini kwenye madhabau ya nyumba za ibada na ndani ya Bunge Maalumu la Katiba kwa niaba yake, aombe radhi taifa.

Tamko la JUVICUF lilitolewa na Mwenyekiti wake Taifa, Katani Katani, huku lile la Bavicha likitolewa kwa pamoja na Mwenyekiti wa Baraza hilo Taifa, John Heche na Katibu Mkuu wake, Deogratius Munishi, jana.

Katani alitoa tamko la JUVICUF alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana na kusema Rais Kikwete anapaswa kumfuta uwaziri Lukuvi kwa kuwa hafai kuwa sehemu ya serikali.

“…Kwani amekosa hekima na busara za kuwaunganisha Watanzania. Badala yake yeye anatumia nafasi yake ya uwaziri kuwagawa Watanzania na kutoa vitisho visivyo na msingi,” alisema Katani.

Aliongeza: “Jambo hili kamwe halikubaliki na ni jambo linaloonyesha kutaka kuchochea vurugu nchini na kuzorotesha demokrasia.”

Alimtaka Waziri Lukuvi na wenzake, kuacha kuwatisha Watanzania kwa kusema kuwa jeshi litachukua nchi.
“Sisi vijana tunaamini kuwa katika nchi za kidemokrasia kama hii yetu, vijana ndiyo kundi la kuogopwa na kuheshimiwa na serikali kwani tuna ushahidi na mifano mingi duniani hivi sasa kwamba vijana wamechukua hatua za kuzinusuru nchi zao punde wanapoona mambo hayaendi sawa.

Lukuvi asitake kutufikisha huko kwani bado tunaamini katika demokrasia na utawala wa sheria,” alisema Katani. 
Alisema JUVICUF inaunga mkono hatua ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaunga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge hilo.

Katani alisema wanaunga mkono hatua hiyo kwa kuwa Bunge hilo limeonyesha wazi kujikita katika kujadili maisha binafsi ya watu, kuchochea mifarakano ya udini, ukabila na aina zote za ubaguzi, kama vile rangi na asili za Watanzania badala ya kujadili katiba itakayowafaa wananchi na kuwavusha kwenye dimbwi la umaskini linalowakabili.

“Na katika hili, JUVICUF inaunga mkono kauli ya kuliita Bunge hilo kuwa linashabihiana kabisa na Intarahamwe,” alisema Katani.
Alisema Bunge hilo limetungiwa majina mengi mabaya na Watanzania mitaani kuliko hata hilo la Intarehamwe linalotambulika na wengi kutokana na mwenendo wake kutowaridhisha wananchi, lakini hilo la Intarehamwe limesikika hadharani tu ndiyo maana linatajwa sana.

Aliwataka vijana wote nchini kuwa makini na kuanza kuchukua hatua za awali, kwani pamoja na kuwa wengi kwa idadi kutokana na sensa ya mwaka 2012, ndiyo kundi linaloumia zaidi kutokana na hali ngumu ya maisha iliyopo hivi sasa nchini.

Wakati JUVICUF ikieleza hayo, Bavicha kwanza limepongeza hatua wajumbe wa Ukawa kutoka ndani ya ukumbia Bunge hilo, kwa madai kwamba limekuwa la hatari kwa umoja, mshikamano na amani ya taifa.

Katika tamko lake Bavicha ilieleza kuwa lugha za ubaguzi wa waziwazi wa kidini zilizotelewa na viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni sumu mbaya kwa taifa.

Lilieleza kuwa hiyo ni kutokana na kundi linalobaguliwa likikosa uvumilivu Watanzania watalishuhudia taifa likitumbikia kwenye machafuko, kama yale yanayoendelea kwenye Jamhuri ya Afrika ya Kati na kwamba, kutibu donda kama hilo daima haiwezekani.

“Aidha, kubagua Watanzania kwa makabila yao ni kitendo haramu kinachopaswa kukomeshwa mara moja, kwani hii ni kemikali mbaya isiyo na kifani kwa umoja wa taifa letu,” lilieleza tamko hilo la Bavicha.

Liliongeza: “Hivyo ni mwendawazimu pekee angekubali kushiriki dhambi hii mbaya na isiyosameheka ya kulipasua taifa na kuhujumu maoni ya wananchi wanaotaka mabadiliko ya taifa lao kupitia katiba mpya iliyokua ikiendelea ndani ya Bunge hilo.

Lilisema Bavicha inaamini kuwapo kwa hali ya namna inayojitokeza kwenye mchakato wa katiba mpya, kunatokana na udhaifu wa viongozi wa serikali.

Kutokana na hali hiyo, tamko hilo la Bavicha linamtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anayedaiwa kumtuma Lukuvi kwenda kuhubiri udini kwenye madhabau ya nyumba za ibada na ndani ya Bunge Maalumu la Katiba kwa niaba yake, aombe radhi taifa.

Limesema hiyo ni kwa kitendo hicho, kwani kwa vyovyote vile haitarajiwi kiongozi wa serikali kupanda chuki za namna hiyo miongoni wa wananchi wa taifa.

“Kwa kuwa mpaka sasa Waziri Lukuvi kwa kauli zake ameonekana kuwa kirusi cha hatari kwa umoja, mshikamano na amani ya taifa letu, ni vema na muhimu akafukuzwa kwenye nyadhifa zake zote,” lilisema tamko hilo la Bavicha.

Lilisema kwa kuwa tume aliyoiteua Rais Kikwete ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya katiba mpya iliundwa na watu waliokuwa na wanaoheshimika kwa utumishi wao ndani na nje ya taifa na ambao kwa uadilifu wao wamefanya kazi kama ilivyostahili hata kama haiipendezi serikali na CCM, waombwe radhi.

Tamko hilo la Bavicha lilisema hiyo ni kwa tume hiyo kutukanwa na wajumbe na viongozi mbalimbali wa CCM  ndani na nje ya Bunge hilo.

“Bavicha inaamini hata mtu angekuwa amepungukiwa na akili kiasi gani, matusi yaliyoelekezwa kwa wazee kama akina Warioba, Butiku, Ahmed Salim, Jaji Ramadhani, Profesa Baregu na wengine, hayavumiliki kwa kiwango chochote kile” lilisema tamko hilo la Bavicha.

Aprili 19, mwaka huu, Lukuvi akizungumza katika sherehe za kumsimika Askofu Joseph Bundara wa Kanisa la Methodist Dodoma, alisema mfumo wa serikali tatu haufai na kwamba, serikali ya Muungano ikikosa mapato itasababisha wanajeshi kukosa mishahara na kuiangusha serikali.

Lukuvi pia alisema kwamba kuruhusu serikali tatu kutasababisha kuibuka kwa siasa kali za Kiislamu upande wa Zanzibar na kuishutumu CUF kuwa inatekeleza siasa za kidini za Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), maarufu kama “Uamsho”.

Kauli hiyo ya Lukuvi ilimfanya Profesa Ibrahim Lipumba kulilinganisha Bunge hilo na kundi la Interahamwe lililochochea ubaguzi wa kikabila uliosababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda kutokana na kukumbatia propaganda.

Profesa Lipumba alitoa kauli hiyo iliyosababisha wajumbe wanaounda Ukawa kutoka nje ya Bunge, akidai kuwa kauli zilizotolewa na Lukuvi ni za ubaguzi.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa