Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » SHEIKH JONGO AMWAGA CHOZI BUNGENI

SHEIKH JONGO AMWAGA CHOZI BUNGENI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Sheikh Hamid Masoud Jongo
 
Mjumbe  wa Bunge Maalumu la Katiba na Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hamid Masoud Jongo, amemwaga machozi bungeni kwa kile alichodai ni masikitiko yake kuona waasisi wa Taifa wanatukanwa na vijana wadogo wajumbe wa Bunge hilo.
Jongo alisema waasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume walitumia nguvu, akili, muda na utashi wao wote kulikomboa Taifa mikononi mwa wakoloni na kuhakikisha undugu unadumishwa kwa kuungana hivyo si busara wazee hao kutukanwa.

“Mtume anasema msiwatukane waliokufa, walishakutana na Mungu huko waliko, Mheshimiwa Makamu wa Mwenyekiti mimi nilikosa usingizi alipobungudhiwa Nyerere na Karume, wazee hawa wanatukanwa na watoto wadogo bila sababu yoyote,” alisema huku akilia kwa sauti kubwa na kufanya simanzi itawale bungeni humo.

Jongo huku akilia, aliendelea kusema kwa mifano kuwa, Mji wa Dodoma umekuwa hivi ulivyo leo na kupata kuwepo kwa Bunge mjini hapa, uamuzi mkubwa wa kitaifa unafanywa hapa kutokana na juhudi za waasisi hao.

Aidha, Jongo alihoji ujasiri wa kutukana mtu tena aliyezaliwa, anaupata wapi na kueleza kuwa, kuwatukana waasisi hao ni sawa na kuwatukana wazazi waliowazaa watu wenye umri rika na waasisi hao kwa kuwa walishirikiana nao.

Alisema suala hilo halikubaliki na wataendelea kulipinga ili waasisi hao wasiendelee kutukanwa na kudhalilishwa.

“Haikubaliki hili, tutalipinga wazi wazi, mimi siko hapa kama mtu mwenye itikadi ya serikali tatu au nne, ila nitasema baadae, lakini, kuwatukana ni makosa,” alisema.

Akizungumzia muundo wa Serikali, Sheikh Jongo alisema Watanzania shida yao si utitiri wa serikali bali linalowaumiza ni kero za maendeleo na maisha yao.

“Matusi, mipasho si vilivyotuleta humu, haya mambo ya kufyatua na nini, si sawa, wakati yanazungumzwa nilitamani kutoka nje lakini ikawa ngumu, inatia aibu,” alisema Shehe Jongo na kusema kuwa yeye pamoja na kwamba ni kiongozi wa dini ya Kiislamu, anaamini katika serikali mbili.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa