Home » » WAANDISHI WA SHERIA KUWEZESHWA KUANDAA MISWADA KWA KISWAHILI

WAANDISHI WA SHERIA KUWEZESHWA KUANDAA MISWADA KWA KISWAHILI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki
 
Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) inatarajia kutoa mafunzo kwa waandishi wa sheria ili  kuwaongezea uwezo wa kuandaa miswada katika lugha ya Kiswahili ambayo inatumiwa na Watanzania wengi.
Akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, Philippe Poinsot, jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki, alisema kwa sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatekeleza mkakati wa kuandaa miswada yote inayowasilishwa bungeni katika lugha mbili, Kiingereza na Kiswahili, ili kuwawezesha wananchi wengi kuisoma.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Naibu Waziri Kairuki, katika kutekeleza kazi hiyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Uandishi wa Sheria inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo uhaba wa watumishi na uwezo na hivyo kuhitaji msaada wa mafunzo.

“Kwa sasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ina kazi ya kuandaa miswada katika lugha mbili ikiwamo Kiswahili ambayo ndiyo lugha ya taifa ambayo wananchi wengi wanaifahamu,” alisema Kairuki.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Mkurugenzi wa Mashtaka, Dk. Eliezer Feleshi, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Mandisa Mashologu na maafisa wengine waandamizi wa serikali.

Akizungumza katika mkutano huo,  Masaju alisema kwa sasa ofisi yake ina waandishi wa sheria 18 tu na kuwa idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na majukumu ya Idara ya Uandishi wa Sheria.

Kwa upande wake, Poinsot, alisema shirika lake limepokea maombi ya serikali na kuwa litayafanyia kazi kwa kushirikiana nayo ili miradi hiyo itekelezwe.

Kwa mujibu wa Poinsot, shirika lake limepanga kuisaidia serikali kupitia mradi wake unaolenga kuimarisha usimamizi wa utoaji haki (Strengthening Administartion of Justice Project).
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa