Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Sera ya Maendeleo ya Hifadhi ya jamii isipofanyiwa mikakati ya
kujumuisha sekta sizizo rasmi nchini umaskini utaendelea kuwa mwiba
mchungu na janga la kitaifa katika siku za usoni.
Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa Watanzania
wengi wapo kwenye sekta isiyo rasmi. Takribani asilimia 70 wapo kwenye
ukulima mdogo na asilimia 10 wamejiajiri kwenye shughuli mbalimbali kama
biashara ndogondogo, madini, sanaa, michezo na uchuuzi mwingine.
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2013
inaonyesha kuwa wanachama wa mifuko yote ya hifadhi ya jamii nchini ni
takribani 1.1 milioni hivyo ni dhahiri kuwa hifadhi ya jamii inawahusu
watu wachache ambao ni sawa na asilimia sita ya nguvu kazi na asilimia
tatu ya Watanzania wote.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema kuwa kundi kubwa la wananchi
hawachangii katika kapu la pensheni kwa sasa hii ikiwa na maana kwamba
mzigo huo ni mkubwa na usiokwepeka kwa taifa pindi idadi ya wazee
itakapoongezeka katika kipindi cha miaka michache ijayo.
“Hili ni janga la taifa…tusifumbwe na muundo wetu
wa idadi ya watu hivi sasa ambapo zaidi ya nusu ya Watanzania wana umri
chini ya miaka 18 na asilimia 72 wana umri chini ya miaka 30. Hili kundi
la watoto linaweza kuwa gawio iwapo tutajipanga vizuri,” alisema Kabwe
na kuongeza;
“Tusipojipanga hili ni bomu ambalo likilipuka
tutatafutana. Ipo siku itafika ambapo hili kundi la watoto halitakuwa na
uwezo wa kufanya kazi tena lakini itabidi livishwe na kulishwa.”
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma
Kaskazini alisema lazima Serikali ihakikishe kuwa hifadhi ya jamii
inahusisha watu wengi zaidi kwa kuwaandikisha katika sekta isiyo rasmi
na hasa wakulima na wafugaji, wavuvi na wachimbaji madini, wafanya
biashara ndogondogo na wengineo.
Alisema huko ndiko kwa kuelekea ikiwa inahitajika
Tanzania imara, bora na yenye neema huku akitoa angalizo kuwa suala hilo
linahitaji utashi wa uamuzi makini.
Akitolea mfano wa nchi ambazo zimechukua hatua hiyo kiongozi huyo alisema nchi kama Korea ya Kusini, Thailand na China.
“Nchi ya China imepata mafanikio makubwa kwa
kufikisha hifadhi ya jamii kwa wakulima vijijini. Serikali za nchi hizo
zimeshirikiana na mifuko ya hifadhi ya jamii kuhakikisha raia wao wengi
wanapata ulinzi wa kijamii ili kupambana na umaskini,” alibainisha
Kabwe.
Hata hivyo Kabwe alisema Tanzania ilijaribu
kufanya hivyo katika Jimbo la Kigoma Kaskazini ambapo wakulima 750 wa
kahawa kupitia Chama cha Ushirika cha Msingi kiitwacho Rumako walijiunga
na NSSF mwaka 2013 Machi lakini bado nguvu na jitihada zaidi
zinahitajika.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment