Home » » WABUNGE DAR WACHACHAMAA

WABUNGE DAR WACHACHAMAA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Wabunge wa Jiji la Dar es Salaam, Iddi Azzan (Kinondoni) na Abas Mtemvu (Temeke) wameitaka Serikali ikusanye kodi ya pango katika jiji hilo ili kuongeza mapato yake na kuachana na utamaduni wa kutegemea mapato katika soda, bia, sigara na vinywaji vikali.
Wakizungumza wakati wa kuchangia mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15 juzi jioni, wabunge hao pia waliponda ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo kasi, wakidai kuwa ni nyembamba na hazikidhi viwango.
“Kodi ya pango ikikusanywa Dar es Salaam kwa mwezi Serikali inaweza kupata Sh600 bilioni. Kama kweli tunataka mapato tuamue maana kuna nyumba zinakodishwa kwa mwezi Sh3 milioni,” alisema Azzan.
“Vitendo vya uhalifu vilivyokithiri Dar es Salaam kwa sasa vinatokana na Serikali kutokuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kuwalipa askari, sambamba na kuwajengea nyumba, sasa jeshi limezidiwa. Kusanyeni kodi ipasavyo,” alisema Azzan.
Mbunge huyo aliiponda bajeti hiyo na kuifananisha na bajeti za miaka ya sitini kwa maelezo kuwa haina kitu kipya na kwamba watendaji wa Serikali walioiandaa ni mizigo.
“Nitashangaa sasa Serikali ikikabidhiwa barabara za mabasi yaendayo kasi na ikapokea, barabara hizi ni nyembemba na sehemu ya watembea kwa miguu ni ndogo mno. Watu wanatumia saa mbili kutoka majumbani mwao hadi ofisini, barabara za jiji hili ni mzigo,” alisema.
Akichangia mjadala huo Mtemvu ameitaka Serikali kukopa fedha ili kulinusuru jiji hilo kwa kuweka flyovers (barabara za juu)), “Hatuwezi kupata maendeleo stahiki kama watu wanatumia saa mbili kutoka majumbani mwao kwenda kazini.”
Alifafanua kuwa kutojengwa kwa ghati namba tatu na mbili katika Bandari ya Dar es Salaam kunaikosesha mapato Serikali kutokana na meli kukaa kati ya wiki mbili hadi tatu, zikisubiri kushusha mizigo.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa