Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » MMOJA AJERUHIWA ,29 MBARONI VURUGU KANISA MORAVIANI DAR

MMOJA AJERUHIWA ,29 MBARONI VURUGU KANISA MORAVIANI DAR

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Vurugu zilizosababisha muumini mmoja kujeruhiwa kichwani zimetokea katika Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Misheni Mashariki na Zanzibar, lililopo Mtaa wa Msisiri, Kinondoni, jijini Dar es Salaam zilizosababisha askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waumini wa kanisa hilo waliozua vurugu hizo.
Vurugu hizo zilitokea jana baada ya waumini wa kanisa hilo waliogawanyika pande mbili kutofautiana.

Upande wa kwanza, ambao wanasali sehemu ya ghorofa ulifungiwa mlango na waumini wa upande wa pili wanaosali sehemu ya chini ya jengo la kanisa hilo.

Baadhi ya mashuhuda, ambao ni wakazi wa eneo hilo, walisema mgororo huo ulianza juzi saa 9.00 alasiri baada ya waumini wa upande wa kwanza, ambao awali walizuiwa na serikali kusali katika kanisa hilo, kufika kanisani hapo na kufungiwa milango.

Walisema awali waumini hao walikuwa wakisali nje ya kanisani hilo chini ya mwembe, lakini cha kushangaza jana waliingia kanisani na ndipo wenzao wa upande wa pili wanaosali sehemu ya chini ya kanisa kuwafungia.

Mwaharusi Salumu, ambaye ni jirani na lilipo kanisa hilo, alisema: “Baada ya waumini kufungiwa kule ghorofani leo asubuhi (jana) waumini wenzao waliwaletea chakula na ndipo waumini wanaosali chini, waliwakatalia kuingia na vurugu kuanza na kusababisha waumini kuanza pande zote kupigana,” alisema Salum.

Katika vurugu hizo, muumini mmoja alijeruhiwa kichwani, baada ya kupigwa na wenzake na kupakiwa katika bajaji na kukimbizwa hospitali iliyopo maeneo ya Mwananyamala kwa matibabu.

Kutokana na hali hiyo, askari wa FFU walianza kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya waumini wa kanisa hilo na umati wa watu waliokuwapo kushuhudia tukio hilo.

Viongozi wa kanisa pamoja na baadhi ya waumini walikamatwa na polisi na kupelekwa kituo cha polisi Oysterbay.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema wanawashikilia watu 29, ambao ni viongozi wa pande zote mbili na baadhi ya waumini kuhusiana na tukio hilo.

Mgogoro wa kanisa hilo ambao umedumu kwa miaka miwili sasa upo chini ya usuluhishi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini, Dk. Lusekelo Mwakafwila, na awali mgogoro huo ulitolewa maamuzi na serikali kwamba kila upande kuendelea na ibada na waumini wake, wakati viongozi wote wakiendelea na usuluhishi.
 
SOURCE: THE GUARDIAN

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa