Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JESHI la Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, imewaomba radhi Mkurugenzi wa Kampuni ya The
Guardian, Bw. Kiondo Mshana na Mhariri wa Gazeti la Nipashe, Bw. Jesse
Kwayu.
Kamishna Msaidizi wa
Polisi ambaye pia ni Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo, Jafari Mohamed
aliomba radhi hiyo jana baada ya jeshi hilo kuwa andikia barua Bw.
Mshana na Bw. Kwayu likiwataka wafike Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi kwa
ajili ya mahojiano.
Katika barua ya jeshi
hilo iliyoandikwa Julai 21, mwaka huu, jeshi hilo lilidai mahojiano hayo
yangehusu habari iliyoandikwa na gazeti la Nipashe, Julai 8 mwaka huu,
ukurasa wa kwanza ikiwahusisha polisi wa kikosi cha pikipiki kuomba na
kupokea rushwa.
"Tunawaomba radhi Bw.
Mshana, Bw. Kwayu pamoja na Wahariri wote wa vyombo vya habari nchini
kwa usumbufu uliojitokeza kwani jeshi halikufuata taratibu zinazopaswa
badala yake tuliandika barua ya kuwaita Kituo Kikuu kwa mahojiano kuhusu
habari hii.
"Hakuna jalada lolote
la kesi ambalo limefunguliwa dhidi ya viongozi hawa ila tulikuwa
tukihitaji msaada wao ili tuweze kuwabaini Polisi wanaojihusisha na
rushwa," alisema Mohamed.
Aliongeza kuwa, yeye
kama Kamishna wa jeshi hilo, hakuwa akifahamu kama Msaidizi wake
Mrakibu wa Polisi (SSP), Amani Makanyaga, amewaita Wahariri hao ofisini
kwake kwa barua.
"Nawaombeni radhi kwa
hilo kwani si lazima kila kitu kinachofanyika, bosi akifahamu hasa
kikiwa cha kawaida lakini kwa hili la msaidizi wangu kuwaita bila
kunijulisha, limenishtua na kukiri amepotoka," alisema.
Alisema SSP Makanyaga
alipaswa kuwatafuta Wahariri hao kwani ni wadau muhimu ili waweze kumpa
ushirikiano wa kuwapata Polisi wanaotumia nafasi zao kulichafua jeshi
hilo.
"Kimsingi sisi hatuna
ugomvi na vyombo vya habari kwani niwadau wetu wakubwa wa kufichua
maovu...nitafanya mazungumzo na hawa Wahariri ili tuweze kulifuatilia
suala hili," alisema.
Hata hivyo, SSP
Makanyaga alikiri kosa hilo na kuwaomba radhi Wahariri akiwaomba
waendelee kushirikiana kwani barua aliyoiandika imetafsiriwa vibaya na
tayari kuna askari waliohojiwa na wanaendelea kukusanya malalamiko
kutoka kwa wadau wengine na wananchi.
"Lengo langu la
kuwaandikia barua viongozi hawa si kuwashtaki ila ni kupata msaada
kutoka kwao tuweze kuwabaini askari wengine wenye tabia ya kuomba na
kuchukua rushwa," alisema.
Kwa upande wake, Bw.
Mshana alisema ipo haja ya askari polisi kupewa mafunzo ambayo yatahusu
namna ya kufanya kazi na vyombo vya habari ili kuacha kujikuta wakiita
watu wasiohusika kuwahoji.
"Mimi kama Mkurugenzi
ni Mtendaji ndani ya chumba cha habari lakini sihusiki kuandaa gazeti
hivyo kuniita kuhojiwa ni kunipotezea muda wa kutekeleza majukumu yangu
kikazi...najitolea kutoa mafunzo kwa vijana wa jeshi hili ili waweze
kufahamu namna ya kufanyakazi na vyombo vya habari," alisema.
Naye Bw. Kwayu
aliungana na Bw. Mshana akisema kitendo kilichofanywa na SSP Makanyaga
kinaonesha ni namna gani ana uelewa mdogo kiutendaji.
Katika habari
iliyoandikwa na gazeti hilo, ilielezea jinsi askari hao walivyozigeuza
pikipiki walizopewa kuwa nyenzo za kukusanya pesa bila huruma na
walivyojigeuza kuwa askari wa usalama barabarani na kuvizia malori.
Habari hiyo iliongeza
kuwa, askari hao wamekuwa kero jijini Dar es Salaam wakiacha kutekeleza
jukumu lao la kupambana na uhalifu na kujiingiza katika vitendo vya
kukamata magari na kudai rushwa
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment