Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » TPDC ISEME KWA NINI MAKUBALIANO NI TOFAUTI NA MKATABA ELEKEZI?

TPDC ISEME KWA NINI MAKUBALIANO NI TOFAUTI NA MKATABA ELEKEZI?

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Baada ya kuvuja kwa mkataba wa kutafuta na kuzalisha gesi asilia kati ya TPDC na kampuni ya Norway ya StatOil na baada ya baadhi ya wachambuzi kuhoji kuhusu mkataba huo, TPDC imetoa maelezo yake.
Siyo mara moja, sasa ni mara ya tatu. Kimsingi, TPDC wanasema wachambuzi waliochambua nyongeza hiyo ya mkataba hawana uelewa wa mambo haya na wanaleta siasa.
Nadhani ni muhimu TPDC wakajikita katika kueleza kwa lugha ambayo wananchi wa kawaida wataelewa badala ya kusingizia uelewa wa watu katika masuala haya. Wizara ya Nishati na Madini haina uelewa wa pekee wa masuala ya mafuta na gesi kama wanavyotaka umma uamini.
Kuna Watanzania wengi wenye kufuatilia mambo haya na wenye uwezo mpana, hasa katika masuala ya kodi katika tasnia hii.
Ni wajibu wa TPDC kutoa maelezo yasiyochanganya wananchi na bora zaidi waweke mikataba hii ya gesi na mafuta wazi. Maelezo yaliyotolewa na TPDC mpaka sasa hayaeleweki na yana lengo la kuwachanganya wananchi kama siyo kuwadanganya.
Swali la msingi
Serikali kupitia “Model PSA” imeweka viwango vya mgawanyo wa mapato kati ya mwekezaji na nchi. Viwango hivi ni vya mgawo wa mafuta au gesi asilia yanayozalishwa kwa siku.
Mkataba huu elekezi upo kwenye tovuti ya TPDC na ndiyo mwongozo wa majadiliano kwa mikataba yote.
Kwa mujibu wa mkataba huu elekezi, uzalishaji wa gesi asilia unapokuwa wa chini kabisa (0 –249.999 MMscf kwa siku) mgawo kati ya Tanzania na mwekezaji unakuwa ni nusu kwa nusu (50 – 50) baada ya mwekezaji kuondoa gharama zake zote za uzalishaji.
Iwapo uzalishaji umefikia hali ya juu kabisa ( 1500 MMscf na zaidi) mgawo wa Tanzania unakuwa asilimia 80 na mwekezaji asilimia 20.
Mwekezaji anaruhusiwa kuchukua mpaka asilimia 70 ya gesi iliyozalishwa kufidia gharama za uzalishaji. Hivyo, kinachogawanywa ni asilimia 30 zinazobakia.
Mkataba uliovuja (TPDC na Stat Oil hawajaukanusha) unaonyesha kuwa kwa kiwango cha chini kabisa cha uzalishaji Serikali inapata asilimia 30 na mwekezaji asilimia 70 licha ya kwamba tayari gharama zake keshajirudishia
Vilevile, kiwango cha juu kabisa cha uzalishaji mgawo unakuwa sawa kwa sawa!
Swali la msingi hapa ni, kwanini makubaliano na kampuni hii ya StatOil yanaenda tofauti na mkataba elekezi? Je, mikataba yote 26 imekwenda harijojo namna hii? Maswali haya bado hayajajibiwa na TPDC.
Uelewa wetu
Mkataba wa gesi asilia au mafuta ni makubaliano ya kugawana mapato yanayotokana na kiwango kilichozalishwa. Katika maelezo yao TPDC wanaeleza kuhusu kodi ya mapato, mrahaba na kodi ya huduma.
Kodi ya Mapato na kodi ya huduma ni kodi ambazo kila mfanyabiashara nchini anapaswa kulipa. Ikumbukwe kuwa imechukua miaka 20 na kelele nyingi mpaka kampuni za madini kuanza kulipa kodi ya mapato na ushuru wa huduma.
Mpaka leo hii bado halmashauri za Geita na Kahama zinahangaika kudai kulipwa ushuru huu kampuni za uchimbaji.
Kampuni za madini na za mafuta hutumia mikakati ya kupanga kukwepa kodi kwa kutumia misamaha ya kodi (tax heavens) na mikataba ya ‘Double Taxation Treaties.’
Hivyo, TPDC kusema tutegemee Kodi ya Mapato ni sawa na kuimba kama kasuku na baada ya miaka 20 tutajikuta kwenye lawama zile zile za sekta ya madini.
Kwenye baadhi ya mikataba, kodi wanayolipa wawekezaji hukatwa kwenye mgawo wa TPDC na hivyo kodi hiyo hulipwa na TPDC na siyo mwekezaji kama tunavyoaminishwa na Serikali.
Kuhusu mrahaba wa asilimia 5 napo kuna tatizo kwani kwenye mikataba ya gesi asilia, mrahaba unalipwa na TPDC maana ndio mwenye leseni na siyo mwekezaji ambaye ni mkandarasi.
Mikataba kadhaa imeandikwa kwa namna ambayo mwekezaji akilipa mrahaba, anajirudishia kwenye mapato ya gesi kama gharama.
Hivyo, kimsingi mapato yetu ya uhakika ni kwenye mgawo wa uzalishaji. Ndiyo maana tunapiga kelele kuhusu mkataba huu wa StatOil kwenda kinyume na mkataba mwelekezi wa Serikali.
Tutaambulia kidogo
Kwa kuchambua mkataba huu kati ya Tanzania na StatOil , hesabu zinaonyesha kuwa nchi yetu itapata mgawo kidogo.
Chukulia uniti 1000 za gesi asilimia zimezalishwa kwa siku. Uniti 700 zinachukuliwa na mwekezaji kufidia gharama za kuzalisha gesi hiyo na uniti 300 zinazobakia mwekezaji anachukua uniti 150 kama mgawo wake wa faida.
Hivyo, Tanzania itabakia na uniti 150 kama mgawo wake, sawa na asilimia 15 ya gesi asilia yote iliyozalishwa katika siku hiyo. Iwapo mkataba elekezi ungefuatwa, Tanzania ingebakia na uniti 240 sawa na asilimia 24ya gesi asilia iliyozalishwa.
Vyombo vya habari nchini vifuatilie na kuandika masuala haya bila kuyumba maana yanahusu utajiri wa nchi yetu. Dhahabu imebakia mashimo kwa sababu nchi ililala na watawala kuandika mikataba ya ovyo. Tusilale kwenye gesi asilia. Tusikubali majibu mepesi. Tutake mikataba iwekwe wazi ili kuwe na uwajibikaji
Chanzo:Mwananchi 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa