Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Jakaya Kikwete amemteua Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Eliezer Feleshi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Feleshi ameteuliwa pamoja na wengine 19 kushika
wadhifa huo akiwamo Naibu Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru ), Lilian Mashaka na wataapishwa leo
Ikulu.
Uteuzi huo umepongezwa na Rais wa Chama cha
Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura akisema Serikali
imesikiliza kilio chao cha muda mrefu cha kutatua tatizo la upungufu wa
majaji nchini.
“Tunaipongeza Serikali kwa kutusikiliza ingawa si kwa asilimia 100.”
Mara ya mwisho Rais Kikwete aliwateua majaji saba
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Juni 8, 2012. Majaji wengine walioteuliwa
katika uteuzi mpya ulioanza Agosti 13, mwaka huu ni Penterine Kente
ambaye alikuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani na Benedict Mwingwa
aliyekuwa Msajili wa Mahakama Kuu.
Wengine ni Edson Mkasimongwa ambaye alikuwa Katibu
wa Jaji Mkuu, David Mrango aliyekuwa Msajili Baraza la Ushindani na
Mohamed Gwae aliyekuwa Msajili Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi.
Dk John Ruhangisa aliyekuwa Msajili Mahakama ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Firmin Matogoro aliyekuwa Naibu Mwenyekiti,
Baraza la Rufaa la Kodi, Barke Sehel aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi, Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Winfrida Korosso aliyekuwa Katibu
Mtendaji, Tume ya Kurekebisha Sheria, Leila Mgonya aliyekuwa Msaidizi wa
Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu na Awadhi Mohamed ambaye alikuwa
Mchunguzi Mkuu wa Takukuru.
Wengine ni waliokuwa mawakili wa kujitegemea,
Lugano Mwandambo kutoka Kampuni ya Rex Attorneys, Amour Said Khamis wa
Kampuni ya AKSA Attorneys na Dk Paul Kiwelu ambaye pia alikuwa Mhadhiri
Mwandamizi, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Wengine ni Rose Ebrahimu ambaye alikuwa wakili wa
kujitegemea wa kampuni ya Bulyankulu Gold Mine Ltd, Salma Maghimbi
aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Ushindani (FCC), Dk Mary Levira ambaye
alikuwa Kaimu Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha
na Dk Modesta Opiyo Makopolo aliyekuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo
Kikuu, Mzumbe.
Akizungumzia uteuzi huo, Dk Modesta alisema: “Nimejisikia furaha kwa kuniona na kutambua kwamba ninaweza na sitawaangusha. ”
Dk Kiwelu alisema: “Uadilifu ni changamoto kubwa
ninawaomba wenzangu kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mmoja na
kuepuka kupindisha sheria”.
Sehel alisema: “Nitatumia nafasi yangu kuhakikisha haki inaendelea kutendeka na kusimamiwa ipasavyo.”
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment