Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Raia wa China, Pianan Li (51), amekamatwa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akiwa na mifupa miwili ya twiga na
fuvu la kichwa cha swala likiwa na pembe zake.
Li alikamatwa juzi saa 10 jioni alipokuwa
akijianda kwa safari kuelekea China kwa kutumia ndege ya Shirika la
Qatar kupitia Doha ambapo alikutwa na nyara hizo alizoficha kwenye begi
la nguo. Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Hamisi Selemani alisema
raia huyo wa China alikuwa hana kibali chochote kinachoonyesha uhalali
wa kuzisafirisha nyara hizo nje ya nchi.
“Alidai kuwa nyara hizo alitokanazo Afrika Kusini, lakini polisi wa uwanja walipodai vibali hakuwa navyo,” alisema na kuongeza:
“Baada ya kupita kwenye mashine ya ukaguzi
tulibaini ameweka nyara hizo kwenye begi la nguo na tulikuta amezifunga
vizuri kwenye nguo zake.”
Alisema kwa hali ya kawaida, mtu anapokuwa na
nyara hizo lazima apewe kibali kutoka nchi husika, lakini walimshangaa
raia huyo akidai kuwa ametoka nazo Afrika Kusini.
Selemani alisema mtuhumiwa huyo aliyekuwa na hati
ya kusafiria ya China, alihojiwa kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili
na Utalii na upelelezi unaendelea.
Selemani alisema polisi wataimarisha ulinzi katika
maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege ili kudhibiti aina hiyo ya
utoroshaji wa nyara.
Hivi karibuni Raia wa Vietnam, Dong Van (47)
alikamatwa katika uwanja huo akiwa na meno 65 na kucha 447 za simba
zenye thamani ya Sh189.4 milioni.
Alikamatwa na nyara hizo akiwa amezificha kwenye
begi lake la nguo, huku zikiwa zimefungwa vizuri katika pakiti za mchele
na kahawa.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment