SHINDANO
la elimu ya uwekezaji kwa wanazuoni kwa mwaka 2014, lililokuwa
likiendeshwa na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limemalizika kwa
kuwapata washindi watatu wa kwanza kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Shindano hilo
lililojulikana kama DSE Scholar Investment Challenge 2014 lilidhaminiwa
na Benki ya NMB pamoja na Kampuni ya Mawasiliano ya Selcom na Mfuko wa
kuendeleza sekta ya fedha (FSDT) lilimalizika Juni 2014.
Akizungumza katika
hafla fupi ya kuwatambulisha washindi hao jana Dar es Salaam, Mkurugenzi
Mkuu wa soko la hisa Dar es Salaam, Moremi Marwa alisema kuwa, shindano
hilo lilihusisha zaidi ya wanafunzi 5,000 kutoka vyuo vya elimu ya juu
kote nchini.
Marwa aliwatangaza
washindi hao kuwa ni Dynko Amosi (SUA) ambae ndiye mshindi wa kwanza na
kupewa kitita cha sh.1,000,000, mshindi wa pili akiwa ni George Firimin
(IFM) na kupewa zawadi ya sh.600,000 na mshindi wa tatu akiwa ni Godlove
Kelly(UDSM) ambae alipewa zawadi ya sh.400,000.
Aliongeza kuwa,
shindano hilo ni kampeni endelevu ya kila mwaka inayowalenga vijana wa
kitanzania walioko kwenye vyuo vya elimu ya juu nchini ili kufanikisha
dhana ya kutoa elimu juu ya uwekezaji katika taasisi za kifedha.
"Katika shindano hili
kila mshiriki hupewa mtaji wa kuanzia ili kuwaweka kwenye soko la hisa
kwa kipindi cha miezi mitatu,"alisema.
Alisema kuwa, nia kubwa
ya kampeni hiyo ni kuwafundisha na kuwahamasisha vijana kujenga tabia
ya kuwekeza na kutunza fedha kwa kuonesha kwa vitendo sababu na namna ya
kununua na kuuza dhamana kwenye soko la hisa.
Kwa upande wake Mkuu wa
Idara ya njia mbadala wa Benki ya NMB, George Kivaria alisema kuwa nia
ya benki hiyo ni kuona inafanikisha malengo ya kutoa elimu kwa vijana
juu ya namna ya uwekaji akiba kwenye taasisi za kifedha.
Aliongeza kuwa, huu ndio muda wa kuondoa ile dhana potofu ya kuwa wanaowekeza kwenye soko la hisa ni watu wenye uwezo tu.
"Katika soko la hisa
kila Mtanzania anaweza kuwekeza, sio kwa wale wenye uwezo tu hisa zipo
za bei tofauti tofauti hivyo kila Mtanzania anaweza kumudu kununua
hisa," alisema.
0 comments:
Post a Comment