Home » » DENI LA MSD LAATHIRI MUHIMBILI, OCEAN ROAD

DENI LA MSD LAATHIRI MUHIMBILI, OCEAN ROAD

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali, Sikika, Irenei Kiria

Bohari Kuu ya Dawa ya Taifa (MSD), imesitisha kusambaza dawa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali za Wilaya ya Kiteto, Mpwapwa na nyingine nyingi kutokana na deni la Sh. bilioni 98.3.

Kadhalika, MSD imesitisha kutoa huduma hiyo hadi pale itakapolipwa deni lake ili kulinda mtaji wake ambao umekuwa ukizidi kutetereka kutokana na madeni yaliyolimbikizwa na serikali, ikiwa ni gharama ya ugomboaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa vifaa kutoka miradi misonge.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali, Sikika, Irenei Kiria, alisema hospitali hizo zinakabiliwa na uhaba wa dawa na kwamba serikali inakwamisha huduma hiyo kutolewa kutokana na kulimbikiza deni kwa MSD.

“Kwa mujibu wa uchunguzi wa Sikika pamoja na vyombo vya habari, Wizara ya  Afya na Ustawi wa Jamii pekee inadaiwa Sh. bilioni 90, Hospitali ya Muhimbili Sh. bilioni nane na hospitali ya Wilaya ya Kiteto Sh. milioni 38 na nyinginezo… ongezeko la deni limekuwa likiathiri ufanisi wa bohari hiyo kutokana na ukweli kuwa MSD haifanyi kazi kwa faida na mtaji wa kujiendesha” alisema na kuongeza:

“MSD mtaji wa kujiendesha yenyewe umekuwa ukipunguwa siku hadi siku na hivyo kupelekea kushindwa kufanya manunuzi kwa wakati, kusambaza na kuwa na akiba ya kutosha ya dawa na vifaa tiba… kukua kwa deni hilo kunasababishwa na ufinyu wa bajeti ukilinganisha na makadirio ya mahitaji, upungufu wa pesa iliyotolewa na Serikali Kuu,” 

alisema Kiria. Alisema pamoja na kwamba wananchi wengi huchangia fedha kutoka mfukoni, rekodi za afya zinaonyesha kuwa mchango wake katika vyanzo vya mapato ni mdogo.

Alisema shirika lake linapendekeza serikali kutimiza ahadi yake ya kutoa fedha zote za dawa na vifaa tiba muhimu kwa wakati muhimu, ipitie upya utekelezaji wa mwongozo wa matumizi ya fedha za uchangiaji wa papo kwa papo.

Aidha, matatizo yanayosababishwa na uhaba wa dawa na kwamba yanatishia uhakika wa huduma kwa mgonjwa anapokwenda hospitali au zahanati na hivyo kupunguza ari ya kufanya kazi kwa watumishi.

“Uhaba wa dawa muhimu na vifaa tiba unaoendelea kwa sasa unasababishwa na ukosefu wa fedha pamoja na mrundikano wa madeni ya baadhi ya vituo vya huduma za afya…Bohari Kuu ya Dawa ya Taifa (MSD) imesimamisha kutoa huduma yake katika vituo hadi pale madeni yatakapolipwa,” alisema mkurugenzi huyo.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa