Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Serikali ipo hatarini kupoteza hisa zake katika Benki yaTaifa ya Biashara (NBC), kutokana na kudaiwa Sh. bilioni 22.5 na Kampuni ya ABSA, ambaye pia ni mwanahisa, kwa muda mrefu sasa.
Hayo yalibainishwa katika kikao baina ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali PAC), uongozi wa benki hiyo na Hazina, kilichofanyika kwenye ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam jana.
Kamati ilikuwa inapokea taarifa kutoka Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu maendeleo ya hisa za serikali katika benki hiyo.
Ofisa kutoka Hazina, Domi Malosho, alisema awali NBC ilikuwa inamilikiwa na serikali kabla ya kubinafsishwa kwa ABSA mwaka 2000 na hivyo kuwa mmoja wanahisa na kuwa ya kubinafishwa mwaka 2000, ABSA ilikuwa na umiliki wa hisa kwa asilimia 70, huku asilimia 30 zikimilikiwa na serikali.
Alisema baada ya ubinafsishaji huo, NBC iliendelea kuimarika, lakini mwaka 2010 kukatokea mkanganyiko kati ya serikali na mwanahisa mwenzake, ABSA kuhusu kuuza hisa kwa kampuni nyingine.
Hata hivyo, alisema mkanganyiko huo ulizimwa na Waziri wa Fedha na Kampuni ya IFC kuuziwa hisa ya umiliki wa NBC kwa asilimia 15 na hivyo benki hiyo tangu kipindi hicho kuwa na jumla ya wanahisa watatu.
Alisema mwaka 2011 na 2012, hali ya NBC ilikuwa mbaya na serikali ikafanya maamuzi ya kuitia nguvu kwa kuipa Sh. bilioni 75, ambazo zilitakiwa kuchangiwa na wanahisa wote watatu, huku serikali ikitakiwa kutoa Sh. bilioni 22.5.
Domi alisema serikali kama mwanahisa ilishindwa kulipa kiasi hicho cha fedha na hivyo kuiomba ABSA imkopeshe, ambaye alikubali, lakini tangu kipindi hicho hadi sasa fedha hizo hazijalipwa.
Hali hiyo imekuwa ikifanya hisa za serikali kuendelea kupungua kwa takriban asilimia 12.
Kwa mujibu wa mikataba, iwapo serikali itashindwa kulipa kiasi hicho cha fedha hadi mwishoni mwa Machi mwakani, hisa zake zitakuwa zimeyeyuka na hivyo kukosa kupoteza umiliki wake.
Alipotakiwa kuonyesha mbele ya kamati hiyo baadhi ya mikataba iliyokuwa inafanywa katika matukio hayo yote tangu mwaka 2000, alisema hakuwa nayo hapo na kuahidi kuleta itakapowezekana.
Pia ofisi ya CAG katika taarifa hiyo, ilionyesha kuwapo kwa matumizi mabaya ya fedha za mikopo iliyokuwa inatolewa kwa wafanyakazi wa benki hiyo kwa ajili ya kununulia magari ya mizigo (malori).
Domi alisema mtu aliyekuwa anataka kununua gari, alitakiwa kupewa kupitia wakala aliyewekwa na uongozi wa benki kwa ajili ya kuagiza magari hayo.
Hata hivyo, ripoti hiyo ya CAG ilionyesha kwamba, wateja walikuwa wanapatiwa kadi zinazoonyesha kwamba magari waliyonunua ni mapya jambo ambalo halikuwa kweli, badala yake walikuwa wanafojiwa kadi na kupewa magari mabovu kwa gharama za magari mapya.
0 comments:
Post a Comment