Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » SERIKALI: TUTALIPA BILIONI 22.5/- KUOKOA HISA NBC

SERIKALI: TUTALIPA BILIONI 22.5/- KUOKOA HISA NBC

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Serikali imesema, haijashindwa kulipa deni la Sh. bilioni 22.5 inayodaiwa na kampuni ya ABSA ya Afrika Kusini, iliyoikopesha kama mwanahisa kwa ajili ya kuongeza mtaji kwenye Benki ya Taifa ya Bishara (NBC). 

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alipozungumza na NIPASHE kuhusiana na deni hilo.

“Serikali haijashindwa kulipa hili deni ila tulikuwa tunasubiri ripoti kuhusu ufafanuzi. Serikali itajitahidi kulipa hilo deni ili tuweze kuendeleza na kunufaika na shirika,” alisema Waziri Mkuya.

Kwa mujibu wa Mkuya, hadi sasa bado serikali ina hisa ya asilimia 30 kwenye benki hiyo na kwamba baada ya kulilipa deni hilo, itaangalia iwapo itaendelea au la.

Wiki iliyopita, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu hali ya hisa za serikali kwenye benki hiyo.

Taarifa hiyo ilionyesha kuwa Serikali ipo hatarini kupoteza hisa zake  na hivyo NBC kubakia mikononi mwa ABSA.

Deni hilo lilitokana na Serikali kushindwa kulipa Sh. bilioni 22.5 na ABSA ili kuinua mtaji wa benki hiyo ambao uliyumba kati ya mwaka 2010 na 2011.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kadri muda unavyozidi kuendelea ndivyo serikali inavyopoteza hisa zake kwenye benki hiyo na iwapo hadi Machi 30 mwakani itakuwa haijalipa, itakuwa hatarini kupoteza hisa zake na NBC kubakia mikononi mwa kampuni binafsi.

Hata hivyo, Mkuya hakueleza iwapo serikali italilipa deni hilo kwa mkupuo au la, zaidi ya kusema itajitahidi kulilipa.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa