Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, amesema wizi na ufujaji wa fedha za walipa kodi nchini unatokana na watendaji wakuu kwenye sekta ya umma kukwepa kubanwa na mifumo ya ufuatiliaji na tathmini.
Amewataka Makatibu Wakuu wa Wizara na Makatibu Tawala wa Mikoa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kwamba asiyeweza kubadilika ajiengue kabla hajaenguliwa.
Aliyaeleza hayo wakati akifungua mkutano wa Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa (RAS) wa kila mwaka mjini hapa jana.
“Kwa miaka mingi tulitakiwa kuwa na mikataba ya utendaji kazini katika utumishi, lakini miaka mingi linapigwa danadana, hata kwenye mkutano uliyopita tuliazimia uanze kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2014/2015, mpaka sasa rasimu ya kwanza haijafika kwenye mkutano wa Makatibu Wakuu,” alieleza Balozi Sefue
Balozi Sefue alielezea kwamba waraka huo ungekuwa unapendekeza kuboresha maslahi, ungefikishwa kwenye Baraza la Mawaziri na utekelezaji wake ungeanza tangu Julai, mwaka jana.
Kwa mujibu wa Balozi Sefue, taasisi na watumishi wa umma wanatumia kiasi kikubwa cha bajeti inayotokana na kodi za wananchi na alihimiza viongozi hao wakubali kupokea mifumo inayopima na kutathmini utendaji wao.
Balozi Sefue alibainisha kuwa baada ya kuanzishwa Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu, imethibitika kuwepo mapungufu makubwa kwenye udhibiti wa ndani na kwamba mwarobaini wa hali hiyo ni viongozi hao kuwa na dhamira ya kweli kwa kusema “sasa basi” na wasiokuwa tayari kwa mabadiliko hayo wawapishe.
Alitoa mifano michache ya mambo ambayo serikali inataka kupitia kwa viongozi hao yakome, kuwa ni pamoja na udanganyifu uliyogunduliwa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wakati akihkiki madai ya walimu tangu wa elimu ya msingi hadi wa vyuo vikuu.
SOURCE: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment