Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ameshauri fedha zinazokusudiwa kutumiwa na Serikali kuendesha kura ya maoni ya Katiba mpya inayopendekezwa, zitumike kununua mazao ya wakulima.
Zitto amesema zoezi hilo, ambalo linatarajiwa kufanyika Aprili, mwakani ni mwanya mwingine wa matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuwa katiba inayotafutwa haina ridhaa ya Watanzania wote.
Zitto alisema hayo alipozungumza na NIPASHE, jijini Dar es Salaam jana kuhusiana na mchakato huo na kura ya maoni itakayopigwa na wananchi kuamua kuipitisha katiba hiyo au kuikataa.
Alisema katika msimu wa kilimo wa 2013/2014, wakulima wametekeleza wajibu wao wa kuzalisha chakula kwa kiasi kikubwa kupita kiwango cha Taifa.
Hivyo, alisema kuwaachia mazao hayo yawaharibikie mikononi, kutawavunja moyo na kuwarudisha katika umaskini.
Alisema katiba ni suala la maridhiano na siyo la kundi moja na kwamba hata ukitumika ujanja wa kufanikisha kuipitisha baada ya muda, italazimika kutafutwa katiba yenye ridhaa ya pamoja, huku fedha nyingi zikiwa zimepotea.
“Wakulima wamefanya yao. Wamelima na ziada msimu wa 2013/14. Nafaka tani milioni 16 zimevunwa wakati matumizi ya nchi ni tani milioni 12. Haijapata kutokea tangu uhuru kufikia uzalishaji asilimia 120,” alisema Zitto.
Aliongeza: “Serikali fanyeni yenu, nunueni mazao haya. Maana yameanza kuoza huko vijijini. Badala ya kufanya kura ya maoni ya katiba isiyo na mwafaka, tumieni fedha hizo kununua mahindi. Wafanyabiashara waje kununua kutoka Hifadhi ya Taifa na kuuza nje.”
Alisema inauma kuona wakulima wakihimizwa kulima kwa bidii, huku kukiwa hakuna jitihada za makusudi za kununua mazao yao.
Zitto alisema hali hiyo itawarudisha katika umaskini na kwamba ni wakati muafaka sasa kwa serikali kupunguza siku za wabunge kukaa na viongozi kupunguza safari kwa ajili ya kuelekeza fedha hizo katika ununuzi wa mazao ya wakulima.
Alisema kama wakulima wataachwa katika hali hiyo, huku wakiwa wametumia fedha na rasilimali nyingi kufanikisha uzalishaji wa mazao hayo, watakata tamaa hali itakayofanya nchi kuongeza idadi ya watu walio maskini na tegemezi.
Alisema jambo hilo ni la hatari kwa mustakabali wa amani na utulivu nchini.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment