MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP) amewasilisha katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kusudio la Kukata Rufaa dhidi ya uamuzi wa ombi lililowasilishwa na Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Shekhe Farid Hadi Ahmed na wenzake.
DPP amewasilisha kusudio hilo, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ulioamuru Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusikiliza hoja za washitakiwa katika kesi hiyo kwa kuwa ina mamlaka ya kusikiliza na kuzitolea uamuzi.
Wakili wa serikali, Peter Njike alidai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kuomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa kuwa DPP ameamua kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu na tayari amewasilisha kusudio.
Hakimu Hellen Riwa alisema jalada la kesi hiyo amelipata, lakini hajalisoma na hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi leo ili alisome kabla ya kuendelea.
Hata hivyo, Hakimu Riwa aliutaka upande wa Jamhuri ukumbuke uamuzi ambao haumalizi kesi, huwa haukatiwi rufaa. Desemba 19 mwaka huu Jaji Dk Fauz Twaib wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, alitoa amri kwa Mahakama ya Kisutu kusikiliza na kuzitolea uamuzi hoja za washitakiwa hao, zilizowasilishwa na mawakili wao.
Katika hoja washitakiwa hao, waliiomba Mahakama ya Kisutu ifute mashitaka ya ugaidi dhidi yao, pia walihoji uhalali wa kushitakiwa Tanzania Bara wakati Zanzibar ni nchi, ambayo ina Mahakama Kuu.
Hata hivyo, Mahakama ya Kisutu ilikataa kwa madai kuwa haina mamlaka ya kutolea uamuzi, kwakuwa kesi ipo katika hatua za awali na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashitaka yao, isipokuwa Mahakama Kuu.
Chanzo:Habari leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment