Zena akiwa na mtoto wake. Mwanamke huyo na wataalamu wa tiba
wanathibitisha kuwa mama mwenye uraibu anayenyonyesha anaweza kumwathiri
mtoto.
Mtoto mwenye umri wa miezi mitatu, mkazi wa Buza, Dar es Salaam amebainika kuwa mwathirika wa dawa za kulevya.
Damu na mkojo vya mtoto huyo (jina tunalihifadhi)
vilichukuliwa na kupimwa katika maabara ya Hospitali ya Mwananyamala na
baada ya saa mbili, majibu yalitoka na kuthibitisha kwamba alikuwa na
chembechembe za dawa za kulevya aina ya heroini.
Taarifa za kitabibu zinaonyesha kuwa kuwapo kwa
heroini mwilini mwa mtu, huweza kuonekana katika mkojo ndani ya siku
mbili hadi nne iwapo dawa hizo zilitumiwa na mhusika kwa kati ya saa
mbili hadi tano.
Hatua ya kumfanyia vipimo mtoto huyo wa kiume,
inatokana na jitihada za gazeti hili kutaka kufahamu jinsi utumiaji wa
dawa za kulevya kwa wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha
unavyoweza kumwathiri mtoto akiwa tumboni au anayenyonya maziwa ya mama
mwathirika.
Mtaalamu wa tiba katika Hospitali ya Mwananyamala,
Dk Elifasi Mritu anasema: “Ni kweli ukitumia dawa za kulevya wakati
unanyonyesha au wakati wa mimba, mtoto naye huathirika.”
Kauli ya Dk Mritu ambaye ni daktari katika kitengo
cha tiba ya methadone hospitalini hapo, inaungwa mkono na Mkuu wa
Kitengo cha Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
Dk Frank Mushi ambaye anasema mama anayetumia dawa za kulevya akiwa
mjamzito humwathiri pia mtoto.
Mama wa mtoto azungumza
Mama wa mtoto, Zena maarufu Zerish, mkazi wa Yombo
Buza alikiri kwamba alipata ujauzito wakati akitumia dawa za kulevya na
kwamba hadi sasa anavuta dawa hizo huku akiendelea kumnyonyesha mtoto
huyo.
Anasema baada ya kujifungua hakukaa ndani kwa siku
40 kama wafanyavyo wanawake wengi wa Kitanzania, kwa sababu mwili wake
ulikuwa unahitaji ‘unga’ vinginevyo hali yake huwa mbaya.
Anasema baada ya kujifungua alianza kuzunguka huku
na kule akiwa na mtoto mgongoni, huku akiwa amebeba mfuko wake wa
plastiki wenye mahitaji muhimu ya mtoto kama nepi na nguo.
Anasema anapovuta au kujichoma dawa, mtoto wake
pia hupata ‘stimu’ kwa sababu hupata dawa hizo za kulevya kupitia maziwa
anayonyonya na hivyo wote wawili kulala fofofo sehemu yoyote ile.
Hata hivyo, kwa Zerish na mwanaye, anapofikia hali
ya kuwa ‘alosto’ (wakati dawa za kulevya zinapoisha mwilini na hivyo
kuhitaji tena), huwa ni adhabu kali mno
Anasema dawa zinapoisha mwilini na mtoto naye huwa katika hali
hiyo na hivyo hulia sana. Hali hiyo humfanya akimbie kutafuta dawa ili
‘kujinusuru’ yeye na mwanaye.
Uwezekano wa tiba
Dk Mushi anasema watoto wanaoathirika kwa dawa
kupitia mama zao, hulia sana na kujinyonganyonga hali inayoashiria
wanapata maumivu ya tumbo.
“Lakini tumaini lipo kwa watoto hao, kwani hupewa
dawa aina ya morphin ambayo hukata ulevi huo taratibu. Baada ya muda
hupona kabisa,” anasema.
Hata hivyo, alisema iwapo mtoto ataendelea
kunyonya maziwa bila kupata tiba huku mama naye akitumia dawa hizo,
huweza kuwa mtumiaji wa dawa hadi anapokuwa mkubwa.
Katika hospitali za Muhimbili na Mwananyamala,
wanawake wenye watoto walio na uraibu wa dawa za kulevya hutakiwa
kuhudhuria kliniki kila siku bila kukosa.
Mwanamke anayetumia dawa za kulevya hutibiwa kwa dawa aina ya methadone na mtoto hupewa morphin.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment