Home » » ESCROW KUTINGA BUNGE LA ULAYA

ESCROW KUTINGA BUNGE LA ULAYA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema sakata la uchotaji fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, watalifikisha katika Bunge la Ulaya (EU) nchini Ubelgiji baada ya kupata mwaliko.

Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, Bw. Salum Mwalimu, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema chama hicho kimepata mwaliko wa kutembelea Bunge la Ulaya nchini Ubelgiji na kushiriki katika Mkutano Mkuu wa chama tawala nchini Ujerumani (CDU) kinachoongozwa na Counsellor Angel Merkel.

"Ziara nzima itakuwa ya siku 10 katika nchi za Ujerumani na Ubelgiji. Mwenyekiti wa chama Taifa, Bw. Freeman Mbowe atahutubia Mkutano Mkuu wa CDU akiviwakilisha vyama vyote vinavyounda UKAWA," alisema.

Aliongeza kuwa, chama hicho pia kimepata mwaliko wa kuhudhuria mkutano wa Bunge CPA, kuzungumza na viongozi wake akiwemo Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CPA.

"Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Bara Profesa Abdallah Safari, Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake (BAWACHA), Bi. Grace Tendega, Mwenyekiti wa BAVICHA, Bw. Pascal Patrobas, Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge, Bw. John Marema na mimi tutakuwepo katika ziara hiyo," alisema Bw. Mwalimu.

Alisema ujumbe huo utaondoka na ajenda kuu nne ambazo ni suala la ufisadi nchini ukiwemo wa Akaunti ya Tegeta Escrow, Tume Huru ya Uchaguzi, Suala la Haki za Binadamu likiwemo la kupigwa kwa waandidhi wa habari, kuuawa na mchakato wa kupata Katiba Mpya ambao umevurugwa kwa makusudi na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aliongeza kuwa, atayazungumza mambo hayo kwa undani kwenye Bunge la Ulaya na CDU ili wafahamu ukweli wa mambo na jinsi misaada wanayoitoa inavyotumika kuwanufaisha wachache ili kulikomboa Taifa mikononi mwa CCM.

"Katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wagombea wetu wengi wameenguliwa kwa sababu ambazo hazina msingi na wengine kuwekewa pingamizi na CCM... tumemwambia Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda ambaye ameahidi kulishughulikia, hakika kwa hilo tunampongeza sana," alisema.

Bw. Mwalimu alisema mbali ya kukutana na viongozi, pia watakutana na Naibu Spika wa Bunge la Ulaya na kuzungumza naye ambapo msafara huo utaongozwa na Bw. Mbowe kwenda nchini Ujerumani

Chanzo:Majira

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa