Jaji Fauz Twaib wa Mahakama Kuu wiki ijayo atatoa uamuzi wa
maombi ya kufutiwa mashtaka ya ugaidi yanayowakabili viongozi wa Jumuiya
za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki).
Mawakili wa washtakiwa hao walifungua maombi hayo
Oktoba 13, 2014, wakitaka Mahakama Kuu ifanye marejeo ya uamuzi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu ya kukataa kusikiliza ombi hilo kwa
kuwa haina mamlaka hayo.
Hata hivyo, upande wa mashtaka uliweka pingamizi
la awali dhidi ya maombi hayo, ukiomba yatupiliwe mbali kwa madai kuwa
hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo, ina dosari za kisheria na
kwamba mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza maombi hayo.
Pingamizi hilo la Jamhuri lilisikilizwa jana na
Jaji Dk Fauz Twaib ambaye baada ya kusikiliza hoja za pande zote,
alipanga kutoa uamuzi huo Jumatano ijayo, Desemba 10, 2014.
Ikiwa Jaji Twaib atakubaliana na hoja za pingamizi
hilo la Serikali, maombi hayo yatatupiliwa mbali na hivyo washtakiwa
hao kuendelea na mashtaka hayo au watalazimika kuchukua hatua nyingine
kadri mahakama itakavyoelekeza katika uamuzi wake.
Haa hivyo, kama mahakama itatupilia mbali hoja za
pingamizi hilo, kesi hiyo itandelea na usikilizwaji wa maombi ya msingi
na hatimaye kutoa uamuzi wa kuyakubali au kuyakataa.
Katika maombi yao yaliyofunguliwa chini ya hati ya
dharura, washtakiwa wanaiomba Mahakama Kuu iitishe na kuchunguza
kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo, ili kujiridhisha na uhalali na
usahihi wake.
Pia wanaiomba mahakama hiyo itupilie mbali hati ya
mashtaka waliyofunguliwa Septemba 3, mwaka huu, wakidai kuwa
imefunguliwa bila ya ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka.
Washtakiwa hao pia wanaiomba mahakama hiyo
itupilie mbali hati ya mashtaka kwa kushindwa kuweka wazi maelezo ya
makosa ya ugaidi yanayodaiwa kutendwa na Sadick na Furaha.
Pia wanaiomba mahakama hiyo itupilie mbali hati ya
mashtaka kwa kushindwa kuonyesha wazi majina ya watu ambao waliandaliwa
kwa ajili ya kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.
Katika mbadala wa maombi hayo ya juu, pia
washtakiwa hao wanaiomba mahakama hiyo iamuru kuwa kila mshtakiwa
ashtakiwe mahakama yenye mamlaka katika maeneo walikokamatiwa.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment