Home » » KARDINALI PENGO, WARIOBA WAONYA

KARDINALI PENGO, WARIOBA WAONYA

 ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, wamesema wanakerwa na tabia ya ufisadi inayoendekezwa na baadhi ya viongozi wa serikali.

Viongozi hao walitoa kauli hiyo inayofanana kwa nyakati tofauti mjini Mwanza na jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 10 ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino jijini Mwanza jana, Kardinali Pengo, alisema wapo baadhi ya viongozi wanaosema Tanzania ni masikini wakati kuna wachache miongoni mwao wanaokwapua mabilioni ya fedha kwa ufisadi na hawafanywi kitu.

“Mimi nashangaa ninaposikia viongozi wanaposema, tena kwa kuwadanganya Watanzania kuwa nchi ni maskini, hakuna pesa za kununua dawa za binadamu kwenye mahospitali, wakati kuna wachache wanaofanya ufisadi wa mabilioni ya fedha, lakini wanaachwa.

“Eti serikali haina pesa, watu hawana aibu ya kutamka hivyo, wakati mabilioni ya pesa yanatumika vibaya kulipia matibabu ya watu wasiojulikana nje ya nchi, ambao hadi leo hawatajwi hadharani na wananchi hawaelezwi pesa hizo zimeenda wapi,” alisema Kardinali Pengo.

Akitolea mfano wa hospitali ya kutibu magonjwa ya saratani jijini Dar es Salaam, Ocean Road, Kardinali Pengo alisema kuna tabia ya wagonjwa kuandikiwa dawa na kuambiwa wakanunue kwenye maduka ya dawa wakati hawana pesa, huku wachache wakikwapua mabilioni kwa ufisadi ambayo yangeweza kusaidia matibabu yao.

Alisema Watanzania hawawezi kusema viongozi wao wana maadili wakati wapo wasioguswa na vifo vya wagonjwa kwa kukosa dawa na wakati wachache wakiendelea kujineemesha kwa kujikusanyia pesa na kuwaacha maskini wakihangaika na kufa.

Bila kutaja majina ya viongozi mafisadi, Kardinali Pengo alisema wapo wanaofanya kufulu kwa kuishi maisha ya peponi, kwa kuiba fedha za walalahoi, bila kujali kwamba kuna watu mahospitalini wanaokufa kwa kukosa dawa na huduma bora.

“Mtu mwenye maadili, hawezi kula na kumiliki mabilioni wakati watu wanakufa kwa njaa, hayo si maadili na ni dhahiri kwamba wamemwacha Mwenyezi Mungu na hayupo ndani yao,” aliongeza.

Mbele ya maaskofu wengine wa majimbo 22 nchini, Kadinali Pengo alisema wasomi wa leo wanapoingia katika ofisi za serikali, wanageuka miungu watu na kuanza kuchezea mali za umma kwa manufaa yao binafsi, huku ufisadi ukiendelea kuwa tabia yao ya kawaida.

Mbali ya kauli hiyo, Kardinali Pengo aliwataka wanafunzi wa kozi za Uandishi wa Habari kuwa makini kwenye kazi zao na wajikite kwenye uandishi wa habari, kwa kuibua mambo ya ufisadi na kusimamia ukweli.

“Waandishi wa habari, siku zote simamieni, ibueni ufisadi na kusimamia ukweli na uwazi na ujasiri bila kuogopa vitisho na kukataa rushwa,” alisema.

Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino kilianza mwaka 1998 na mwaka huu kimetimiza miaka 10.

Maadhimisho hayo yanaenda sambamba na mahafali ya 10 ya chuo hicho yatakayofanyika kesho katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba ya Afya cha Bugando na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete.

Wakati Kardinali Pengo akitoa kauli hiyo, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema taifa lina hali mbaya kwa ufisadi unaotokana na mmomonyoko wa maadili.

Warioba alisema ili kukomesha hali hiyo na kurejesha maadili, kuna ulazima wa kuanzisha Azimio la Arusha namba mbili, kwa lengo la kuweka misingi ya maadili kama ya awali.

Jaji Warioba, alitoa ushauri huo jana, alipokuwa akifungua semina ya siku moja iliyoandaliwa na Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD) kuhusu maadili ya viongozi.

Alisema kwa hali ilivyo sasa, ni wakati muafaka kwa viongozi kutafakari na kuona kama kuna uwezekano wa kuwa na Azimio la Arusha namba mbili na kuonya kwamba hilo lisipofanyika, nchi itaelekea pabaya.

“…Tusipofanya hivyo tofauti kati ya viongozi na wananchi itaendelea kukua na italeta matatizo, hivyo umoja, amani na utulivu tunaojivunia, utakuwa shakani,” alisema.

Jaji Warioba, alisema maadili ya viongozi, hayaletwi na sheria, wala sheria haiwezi kulinda maadili na kwamba sheria mara kwa mara zimekuwa zikibadilishwa lakini mambo hayabadiliki.

Alisema wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere hakukuwa na matabaka kati ya viongozi na wananchi, kwani viongozi walikuwa hawatangulizi mbele masilahi binafsi.

Katika kipindi hicho, alisema wafanyakazi wa kawaida walikuwa wakiongezewa mshahara kwa kiwango kikubwa kuliko viongozi kwa lengo la kuepusha matabaka.

Alitolea mfano kuwa kati ya mwaka 1966 hadi mwaka 1985 Mwalimu Nyerere ( akiwa Rais) alikuwa akipotea mshahara wa sh 4,000 kwa mwezi na yeye (Warioba) wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu, alikuwa akipata mshahara wa sh 7,000 kwa mwezi.

Alisema mshahara wa rais ulikuwa ukiongezwa kwa azimio la Bunge, lakini Mwalimu Nyerere mara kadhaa alikataa kuongezewa mshahara huo.

Aidha, alisema mwaka 1976 viongozi walipitisha Azimio la Arusha ambalo liliweka masharti kuwa kiongozi ni pamoja na kutokuwa na hisa katika kampuni yoyote wala kuwa mkurugenzi na kupokea mishahara miwili kwa mwezi.

Alimtokea mfano mzee Rashid Kawawa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa muda wa miaka 15, kwamba aliweza kufuata miiko hiyo hadi alipoachia madaraka.

“Angalia maisha ya nyumba ya Madale na Kiluvya za mzee Kawawa, zinafanana na cheo alichokuwa nacho? Hata ile ya Songea ni nyumba ya kawaida,” alisema.

Jaji Warioba, alieleza kusikitishwa na nchi kupoteza ujasiri wa kujitegemea na kutegemea kila kitu kuomba kutoka kwa wafadhili.

“Sasa tunaona kila kitu hatuwezi kufanikiwa mpaka tuwe na wafadhili…kila mmoja anaomba mfadhili. Tumepoteza ujasiri wa kujitegemea na ufadhili una matatizo yake,” alisema Jaji Warioba.

Kadhalika, alieleza kusikitishwa na viongozi kuweka masilahi binafsi mbele na kuongeza kuwa baadhi yao wamefikia hatua ya kukataa kuhudhuria mikutano isiyo na posho.

“Unaweza kukuta baadhi ya semina, mikutano anayotakiwa kuhudhuria kiongozi ni sehemu ya kazi yake, naye anapata posho, wakati mwingine unaweza kukuta posho ni kubwa kuliko mshahara… hata baadhi ya wabunge hawaendi kwenye semina za mafunzo mbalimbali kwa kuwa hazina posho,” alisema.

Pia aliezea kushangazwa na kitendo cha wabunge wa Tanzania kutaka kupata mishahara inayolingana na wabunge wa nchi ya Kenya na kusema kuwa wabunge hao hawakupaswa kufanya hivyo, bali walipaswa kulinganisha na masilahi ya wananchi wao.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu, alisema baada ya kuondolewa kwa masharti hayo katika Azimio la Arusha, wakulima na wafanyakazi wameondolewa kwenye uongozi, jambo ambalo limejenga matabaka.

Awali, akimkaribisha Jaji Warioba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema nchi ipo mahali pagumu kutokana na viongozi kupoteza maadili na kukumbatia matajiri na kuwaacha maskini.

Profesa Lipumba, aliwaasa viongozi wenzake kubadilika na kuwa viongozi wa umma na kuheshimu miiko ya uongozi, ili kulinusuru taifa.

 Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa