Hatima ya mawaziri na watendaji waliotajwa katika sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow itajulikana Jumatatu ijayo wakati Rais Jakaya Kikwete atakapohutubia taifa kupitia mazungumzo na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Hotuba hiyo ya Rais Kikwete inafanyika ikiwa
imepita wiki moja iliyopangwa kukamilisha uchambuzi na kutoa uamuzi
dhidi ya wahusika.
Hatua hiyo ya kusogeza mbele muda wa Rais Kikwete
kuzungumzia suala hilo inazidi kuwaweka tumbo joto mawaziri na viongozi
wengine wanaotuhumiwa kuhusika katika sakata hilo.
Taarifa za awali zilizotolewa na vyombo kadhaa vya
habari zilieleza kuwa Rais Kikwete angezungumza jana alasiri, lakini
Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilikanusha na kutoa taarifa nyingine,
ikieleza kuwa atazungumza Jumatatu.
“Rais Kikwete atazungumzia masuala mbalimbali ya
kitaifa, yakiwamo yale ambayo yamekuwa yanasubiri uamuzi wake tangu
alipokuwa anajiuguza kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita,”
ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, baadaye Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Rais Ikulu, Salva Rweyemamu alikaririwa na vyombo vya habari akisema
kuwa tayari Rais Kikwete ameshatoa uamuzi wake kuhusu suala la escrow na
kwamba atautangaza Jumatatu.
Baadhi ya mambo yaliyotokea nchini wakati Rais
Kikwete akiwa Marekani alikokwenda kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa
tezi dume, ni pamoja na sakata la escrow ambapo Bunge lilipitisha
maazimio manane, likiwamo la kumtaka Rais Kikwete kuwachukulia hatua
mawaziri na watendaji wa Serikali waliotajwa kuhusika katika wizi wa
mabilioni hayo.
Rais Kikwete atatoa hotuba hiyo zikiwa zimepita
siku nne tangu alipokatisha ziara ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika
Falme za Kiarabu kwa kile alichokieleza kwamba ni kuitwa nyumbani kwa
shughuli maalumu, kitendo kilichotafsiriwa kuwa ni kwa ajili ya kutoa
uamuzi wa mwisho kuhusu sakata la escrow.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata ndani ya
Serikali zinasema kuwa utendaji wa kazi wa baadhi ya mawaziri, wakuu wa
wilaya na hata baadhi ya watendaji walioko chini yao umeshuka kutokana
na kila mmoja kutojua jinsi uamuzi wa Rais Kikwete utakavyokuwa.
Desemba 9 mwaka huu, Ikulu ilitoa taarifa ya kuwa
Rais Kikwete ameshaanza kusoma Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Umma
(PAC) na maazimio ya Bunge kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow na atatoa
uamuzi ndani ya wiki moja ijayo.
Katika taarifa hiyo, Rais Kikwete alielekeza kuwa
Ripoti ya CAG iwekwe hadharani kwenye vyombo vya habari vinavyofikia
watu wengi kwa ajili ya umma kuisoma na kujua nini hasa kimesemwa na
kupendekezwa, jambo ambalo hadi sasa halijafanyika.
Juzi, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
alisema, “Rais Kikwete bado ana nia ya kuzungumza na atafanya hivyo wiki
hii kabla ya Jumamosi (leo). Hakusema siku atakayozungumza, alisema
atazungumza wiki hii.”
Alisema Rais Kikwete pia atafanya uteuzi wa wakuu wa wilaya
kabla ya mwaka huu kuisha kutokana na baadhi ya wakuu wa wilaya kufariki
dunia, kustaafu na wengine kurejea jeshini. “Nadhani wanaweza kufikia
10 hivi,” alisema.
Kuhusu ripoti ya CAG, Sefue alisema iliagizwa
ofisi ya CAG iweke ripoti hiyo katika mtandao wake, sijafuatilia ila
nadhani wameweka maana ninaiona ikichapwa katika vyombo vya habari.”
Katika kuonyesha kuwa hotuba hiyo ya Jumatatu
imebeba ujumbe mzito, jana mchana Ikulu ilikana taarifa zilizotolewa
awali kuhusu mkutano wa Rais Kikwete na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam,
uliotarajiwa kufanyika jana alasiri, kwa maelezo kwamba Ofisi ya Rais
haikuwa imetoa taarifa za mkutano huo.
Taarifa hiyo ya awali ilitangazwa na kuthibitishwa
na Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abilahi Mihewa akieleza kwamba
Rais Kikwete atazungumza na wazee wa mkoa huo katika Ukumbi wa Blue
Pearl Ubungo jijini Dar es Salaam jana.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana usiku
zinaeleza kuwa kikao kizito kilikuwa kikifanyika Ikulu, huku nyingine
zikieleza kuwa jambo lolote kubwa kuhusu sakata hilo linaweza kutokea
leo au kesho kutokana na uamuzi wa Rais unaweza kuwa hitimisho la sakata
hilo.
Salva Rweyemamu
Rweyemamu alionyesha kushangazwa na taarifa hizo
alizoziita za ‘mtandaoni’ ambazo zilichapishwa na baadhi ya magazeti
(siyo Mwananchi) na kutangazwa na baadhi ya redio na televisheni, kwamba
Rais angefanya mkutano huo jana.
Wakati hayo yakitokea, kuchelewa kwa uamuzi dhidi
ya watuhumiwa hao kumetajwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa
mtihani kwa watuhumiwa kutokana na kutojua hatua zitakazochukuliwa dhidi
yao.
Mbali na mawaziri na watendaji, vile vile wakuu wa
wilaya nao wameendelea kuwa njiapanda kutokana na tamko la Rais Kikwete
kuwa amewapangua na wengine kutengua uteuzi wao, upangaji wa vituo
vipya ukabaki kumsubiri Waziri Mkuu.
Wasomi
Wakizungumza na gazeti hili Profesa wa sheria
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chris Maina alisema, “Uamuzi
ulitakiwa kutolewa mapema kwa sababu ripoti zote tatu ziliwataja
wahusika na makosa waliyoyafanya. Jambo hili halikuhitaji uchunguzi wala
fikra mpya.”
Alisema wahusika walitakiwa kujiuzulu baada ya
kutolewa kwa ripoti hizo na si kusubiri kuwajibishwa kwa kuwa suala hilo
linahitaji uaminifu zaidi kuliko uamuzi wa kisheria.
“Huwezi kuwa kiongozi wakati wananchi wana mashaka na wewe,
busara ni kung’atuka tu. Unawezaje kwenda ofisini wakati unatuhumiwa,”
alisema.
Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
alisema, “Rais hawezi kuchukua uamuzi wa kushinikizwa na mataifa mengine
yaliyotishia kutotoa msaada kwa sababu ya suala hili, ila kifupi ni
kwamba makosa ya wachache yasihesabiwe kama makosa ya Watanzania wote.”
Alisema udhaifu unaowakabili Watanzania unatakiwa
kushughulikiwa na Watanzania wenyewe na siyo kushinikizwa na watu
wengine. “Naamini Rais atachukua hatua, lakini pia anaweza asichukue
hatua yoyote kwa sababu rais hashinikizwi na mtu na hakuna pa kumshtaki.
Tusubiri tuone uamuzi utakaotolewa,” alisema.
Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam alisema kuendelea kuwapo kazini kwa watuhumiwa wa wizi wa
mabilioni hayo unatokana na nchi kuwa na Katiba inayompa rais madaraka
makubwa.
“Bunge lilitoa uamuzi wake ambao ulipewa baraka
pia na Serikali, lakini badala ya wahusika kuchukuliwa hatua inaagizwa
ufanyike uchunguzi mwingine.
Mamlaka makubwa ya rais yanaminya uamuzi wa vyombo
vingine,” alisema. Alisema hivi sasa Bunge kazi yake ni kushauri na
kupendekeza, kwamba anayeshauriwa ana uwezo wa kukataa au kukubali
ushauri husika.
“Bunge linatakiwa kupewa meno ili liwe na uwezo wa kuamrisha jambo,” alisisitiza.
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Faraja Christoms alisema, “Utendaji wa Rais Kikwete una falsafa
ya ‘huu ni upepo utapita’. Inatakiwa kila linapotokea tatizo rais
azungumze na kutoa uamuzi, hii itasaidia kuongeza uwajibikaji kwa
watendaji wa Serikali.”
Alisema ukimya ukizidi unaweza kuondoa imani ya
wananchi kwa Serikali yao, wanaweza kudhani kuwa kuna watu wanaohusika
ambao wako nyuma ya watuhumiwa waliotajwa kuchota mabilioni ya escrow na
ndiyo maana hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa.
Alisema ukimya katika sakata la escrow ni moja ya
sababu ya CCM kupata upinzani mkali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliofanyika Desemba 14 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu
Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama
alisema: “Tusubiri kuona nini kitafuata, ni muhimu kwa hatua kuchukuliwa
yanapotokea mambo yanayogusa masilahi ya nchi.”
Maazimio ya Bunge
Baada ya mjadala wa Tegeta Escrow, Bunge liliazimia kwamba:
1. Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine
husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa
mujibu wa sheria za nchi yetu, watu wote waliotajwa na taarifa maalumu
ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya
Akaunti ya Escrow na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika
vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea.
2. Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Tanesco wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua
uteuzi wao.
3. Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua
za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua
nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika za kudumu za Bunge.
4. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde
Tume ya kijaji ya uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi
ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama
Kuu ya Tanzania.
5. Serikali iandae na kuwasilisha muswada wa
marekebisho ya sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi
mahususi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa
kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi,
kijamii na kisiasa.
6. Mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi,
ziitaje Stanbic Bank (Tanzania) Ltd na benki nyingine yoyote
itakayogundulika, kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi,
kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya
Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
7. Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie
uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa
Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.
8. Serikali itekeleze Azimio la Bunge la kuitaka
iwasilishe mikataba husika bungeni au kwenye Kamati zake kwa lengo la
kuliwezesha kutekeleza vyema wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri
Serikali mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile, kabla ya kumalizika
kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/16.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment