Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kuzuia matukio ya ujauzito kwa watoto wa kike hali si ya kuridhisha.
Mwaka 2011 idadi ya wanafunzi waliopata ujauzito
ilikuwa ni 13,146, 2012 ikashuka hadi kufikia 11,419, lakini kwa mwaka
2013 idadi hiyo iliongezeka na kufikia 21,420.
Pamoja na kuwepo kwa sababu mbalimbali zinazotajwa
kuwa chanzo cha mimba hizo hususani kwa maeneo ya mijini ni madereva
bodaboda na pamoja na makondakta wa daladala.
Uchache wa maeneo ya ndani ya miji umekuwa ni chanzo cha uanzishwaji wa shule za pembezoni.
Sasa kutokana na mbali wa maeneo zilizopo shule
hizo, watoto hulazimika kutumia vyombo vya usafiri wakati wa kwenda na
kurudi shuleni.
Kwani si jambo rahisi kwa watoto hawa kufika maeneo kama Msongola, Chanika, Mvuti na mengineyo.
Sasa kwa kuwa usafiri unakuwa sehemu ya maisha
yao, madereva na makondakta hao hutumia njia mbalimbali kuwarubuni,
matokeo yake ni kupatikana kwa hizo mimba tunazozungumzia.
Je, makondakta na madereva hao wanaliongeleaje suala hilo?
Juma Mkumba (42) ni dereva wa daladala zinazofanya
safari zake ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Anasema hapingani na kauli
iliyotolewa na mkuu wa mkoa kuwa madereva na makondakta ni miongoni mwa
vyanzo vya mimba hizo.
Pamoja na kuwa kitendo hiki hakipendezi hata kidogo kukisikia masikioni, lakini ukweli ni kwamba haya matukio yapo.
“Tumeshuhudia vijana wengi wakianzisha uhusiano na
watoto wa kike. Na pia tumejionea wenyewe wasichana hawa wanavyoishia
kukatiza ndoto za maisha yao kwa kupata ujauzito. Kama mzazi
sifurahishwi kabisa na jambo hili, kwani licha ya kuleta picha mbaya kwa
jamii pia hukwamisha ustawi wa mtoto wa kike na taifa kwa ujumla”
anasisitiza Mkumba.
Wito wangu kwa serikali ni kuwachukulia hatua wale wote wanaowarubuni watoto hawa na hata kuwaharibia maisha yao anasisitiz
Gazeti hili pia lilifanikiwa kuongea na madereva wa bodaboda
kutaka kujua mtazamo wao juu ya kauli ya mkuu wa mkoa. Kassim Hairun
(25) wa Mbagala Kingugi akiwa miongoni mwa madereva wa pikipiki wa muda
mrefu anasema kwamba, kiongozi huyo yupo sahihi kabisa.
Hata hapa ninapoongea na wewe, wapo madereva
wenzetu wanaojihusisha na uhusiano na watoto hao, cha kusikitisha zaidi
ni kuwa licha ya kuwaweka kwenye hatari ya kupata ujauzito, pia watoto
hawa wako hatarini kupata magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya zinaa
ukiwamo Ukimwi.
“Kutokana na udogo watoto hawa hushindwa kutoa
uamuzi kuhusiana na matumizi ya njia za uzazi wa mpango, kwa maneno
rahisi tunaweza kusema, hapa mtoto huyu asiye na hatia hujikuta akiingia
kwenye janga linalosababishwa na tamaa za watu hawa wasio na hata
chembe ya huruma,” anafafanua.
Kinachokera zaidi ni kule kujiweka pembeni kwa
jamii. Maana wawili hawa wanapokubaliana, si kweli kuwa huwa wanaenda
kutimiza uhalifu huo maporini. Huwenda kwenye nyumba za wageni au wakati
mwingine kwenye makazi yao, ambako kote kumezungukwa na jamii.
“Hivi ingekuwa sheria zinafuatwa ipasavyo, ni wapi ingepatikana sehemu ya kufanyia uhalifu huu,” anahoji.
Pamoja na mitazamo ya watu mbalimbali kuhusiana na
tatizo hilo waathirika wa tatizo hili wengi wao wameonekana kujutia,
wakiongea na gazeti hili kila mmoja kwa wakati wake anasema kuwa angejua
ni nini kingetokea asingethubutu kuingia kwenye janga hilo. Zainab
Matilga (18) ni mmoja wa wanafunzi hao. Yeye alichaguliwa kwenye shule
ya Jangwani mara baada ya kufaulu Shule ya Msingi Kilakala iliyopo Yombo
wilayani Temeke.
“Nilipachikwa ujauzito nikiwa kidato cha pili,
wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 16 tu, ndoto yangu ya kuwa daktari
ilizimikia hapo kwani sikuweza kuendelea tena na shule,” anafafanua.
“Kijana mmoja mwendesha bodaboda ndiyo alikuwa baba wa mtoto,” anasema.
Anasema hawezi kusahau katika maisha yake, kwani
baada ya kupata ujauzito huu, wazazi wake walimfukuza nyumbani, hivyo
akaamua kwenda kuishi na kijana aliyempa mimba hiyo.
“Maisha yalikuwa magumu sana, mtoto wangu
alidhoofika na baadaye alifariki dunia kwa malaria.” Anaongeza, “Baada
ya kifo chake niliamua nirudi nyumbani na kuomba radhi wanipokee
niendelee na masomo lakini hakuna aliyenisikiliza, matokeo yake nilirudi
mtaani na kujikuta nikipachikwa mimba nyingine. Hivi sasa nina miaka 18
na tayari nina mtoto mwingine wa pili,” anasisitiza Zainab.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sophia Mjema, anasema
kuwa, mimba katika umri mdogo ni tatizo linalozikabili wilaya mbalimbali
nchini ikiwamo Temeke.
“Tumekuwa tukifanya jitihada mbalimbali
kuhakikisha tatizo hili linakuwa historia, lakini ili tufanikiwe, juhudi
za mtu mmoja mmoja zinahitajika” anafafanua.
Yeyote atakayejihusisha na uhusiano na watoto hawa achukuliwe hatua za kisheria. Lakini pamoja na hilo, jamii ijikite katika kutoa sapoti katika mapambano dhidi ya mimba kwa watoto nchini.
Chanzo:Mwananchi
Yeyote atakayejihusisha na uhusiano na watoto hawa achukuliwe hatua za kisheria. Lakini pamoja na hilo, jamii ijikite katika kutoa sapoti katika mapambano dhidi ya mimba kwa watoto nchini.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment