Hakika teknolojia inazua mengi, hata yale ambayo hayakuwahi kufikiriwa na mababu zetu karne nyingi zilizopita.
Hivi karibuni, wanasayansi wameweza kugundua namna
ya kuzisafisha mbegu za kiume za mtu mwenye virusi vya Ukimwi na
kuondoa virusi hivyo ili kumwezesha kutungisha mimba bila kumwathiri
mwenza wake.,
Hii ni kwa wenza ambao mwanamume anaishi na VVU na mwanamke akiwa hana virusi hivyo.
Programu hiyo maalumu ijulikanayo kama SPAR,
ilibuniwa ili kuwasaidia wenza hao kupata mtoto bila kumwambukiza mama
na mtoto ambao mwanamume anaishi na VVU aweze kuzalisha.
Inafanyikaje?
Kisayansi, damu pekee si kipimo cha kuonyesha kuwepo kwa maambukizo ya VVU katika mwili bali hata katika majimaji ya mwilini.
Ogani zinazozalisha majimaji ya mbegu za kiume huathiriwa kwa namna ya pekee na VVU.
Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa magonjwa, Henry
Mwakyoma anasema kwa kawaida Virusi vya Ukimwi hupenda kukaa katika
chembehai nyeupe(CD4).
“Kwa kawaida VVU haviishi katika mbegu za kiume.
Lakini hupendelea zaidi kukaa katika CD4 au chembehai nyeupe za damu
ambazo zipo katika damu na katika majimaji ya mbegu za kiume au semen,”
anasema.
Anasema ndiyo maana inawezekana mwanamume mwenye VVU asimwambukize mwenza wake.
“Kama hana michubuko mwanamke anaweza asipate
maambukizo, kwa kuwa majimaji ya mbegu za kiume yanakosa mahali pa
kuingia,” anasema.
Hata hivyo, Dk Mwakyoma aliona kuna ugumu
kuzisafisha mbegu za kiume na kuondoa majimaji yake yenye VVU, ili
kuzipandikiza mbegu hizo ili zitungishe mimba kama unavyosema utafiti
huo.
Daktari wa Kitengo cha Uchunguzi wa magonjwa katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili, Innocent Mosha anaungana na Dk Mwakyoma na kusema,
kwa kawaida mbegu za kiume hazina VVU kwa sababu ni seli inayojitegemea
lakini majimaji yanayobeba mbegu hizo ndiyo huwa na VVU.
Wanasayansi wanasema mwanamume anaweza asionyeshe
VVU katika damu, lakini majimaji ya mbegu za kiume yakaonyesha uwepo wa
virusi.
Wanaeleza kuwa lakini kwa mwanamume anayetumia
dawa za kufubaza makali ya VVU, majimaji hayo yakipimwa hayaonyeshi
uwepo wa VVU bali virusi huonekana katika damu tu. Hii ni kwa sababu ARV
hupunguza wingi wa virusi na hivyo kushuka na kufikia kiwango cha
kutoonekana.
Jarida la Science Daily la nchini Uingereza
linasema robo tatu ya wanaume wanaoishi na VVU na wanaotumia ARV,
walipopimwa majimaji yanayobeba mbegu za kiume hayakuwa na VVU.
Hata hivyo, utafiti uliofanywa mwaka 2009 na
Jarida la Tiba la nchini Canada ulibaini kuwa mbegu za kiume zina nafasi
kubwa ya kusambaza virusi vya Ukimwi.
Utafiti huo ulikinzana na huu wa usafishwaji wa mbegu hizi kuondoa majimaji ambayo kwa kawaida ndiyo hudhaniwa kubeba VVU.
Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa mbegu za
kiume zina nafasi kubwa ya kusambaza VVU wakati wa tendo la ndoa kwani
virusi hivyo hujichimbia katika chembehai nyeupe ambazo utafiti ulisema
ipo katika mbegu za kiume.
Utafiti huo ulikanusha tafiti za awali ambazo
zinathibitisha kuwa ni majimaji tu yanayobeba mbegu hizo ndiyo yenye
kuathiriwa na VVU.
Jinsi inavyofanyika
Programu ya SPAR huanza kwa kuwapa ushauri nasaha
wenza. Kisha majimaji ya mbegu za kiume hupimwa iwapo yana virusi.
Kipimo maalumu na makini cha PCR hutumika kuangalia uwepo wa VVU.
Utafiti wa taasisi ya Bedford unaonyesha kuwa
asilimia 24 ya vipimo vya majimaji hayo yaliyotolewa kutoka kwa wanaume
262 ulionyesha uwepo wa VVU hata kama sampuli za damu hazikuonyesha VVU.
Hii ilionyesha hakuna VVU katika majimaji hayo kwa kuwa walengwa
walikuwa wakitumia ARV.
Kwa kawaida majimaji haya ni ya muhimu kwani ndiyo
huzipa mbegu uhai na kuzilinda. Ndizo zinazosaidia mbegu
kusafiri/kuogelea kwa urahisi hadi katika mji wa mimba.
Katika kusaidia uzalishaji huu, majimaji yenye mbegu hutenganishwa kwa kifaa maalumu na kuhifadhiwa.
Mahali zinapohifadhiwa mbegu, huwekwa majimaji ambayo huzipa uhai kama zinapokuwa katika korodani.
Baadaye, mbegu hizo huhifadhiwa na ili mama ashike mimba mchakato wa upandikizaji au In Vitro Fertilization (IVF) hufanyika.
Mwanamke hutakiwa kupimwa iwapo amepata maambukizo kwa bahati mbaya kila mara anapofanya majaribio ya upandikizaji.
Usafishaji huu wa mbegu za kiume unahusisha pia
kuondoa uteute wa aina yoyote katika majimaji hayo. Pia katika
usafishaji huu, magonjwa ya aina yoyote ya zinaa huondolewa ili kuondoa
nafasi ya kuambukiza mama.
Inaelezwa kuwa hata kwa wanaume ambao bado wana
idadi ndogo ya virusi (Viral load) kwenye damu bado VVU vinaweza
kuonekana katika majimaji ya mbegu za kiume.
Hivyo basi, teknolojia hii ya usafishaji wa mbegu
hizi ili kuondoa VVU, inahitajika zaidi kwa wenza ambao wanahitaji
kupata watoto hasa pale mwanaume anapokuwa na VVU na mwanamke hana
Tangu Januari 2014, watoto 150 walizaliwa kwa kupitia programu hii. Miongoni mwao ni pacha 22.
Dk Athuman Mjombikisa, wa Hospitali ya Nyangao,
Lindi anasema watafiti wamekuwa wakijaribu njia mbalimbali za kuwasaidia
wenza wenye VVU kupata watoto bila mafanikio.
Akielezea teknolojia hii katika muktadha wa
Tanzania, Dk Mjombikisa anasema bado ni vigumu wenza kukubali, pia
watakaoweza ni wachache wenye kipato kikubwa.
Umuhimu wa majimaji ya mbegu za kiume
Kwa kawaida majimaji haya si mbegu za kiume.
Lakini yana umuhimu mkubwa katika utengenezwaji na uhifadhi wa mbegu
hizo. Majimaji haya husaidia mbegu kusafiri kwa urahisi hadi katika mji
wa mimba.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment