Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » MBARONI WAKIHUSISHWA NA MAUAJI YA WANAWAKE DAR

MBARONI WAKIHUSISHWA NA MAUAJI YA WANAWAKE DAR

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya utekaji, unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya wanawake.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema watuhumiwa hao wamehusishwa na vitendo hivyo baada ya upelelezi wa kina na wa kitaalamu uliosaidia kuwakamata wahalifu hao wakiwa na vielelezo mbalimbali.
Kova aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni wakazi wa Dar es Salaam, Abubakar Amani (28) wa Mwenge katika Manispaa ya Kinondoni na Ezekiel Kasenegala (25) wa Tandika, katika Manispaa ya Temeke.
Pia alisema watuhumiwa hao walikiri kuhusika na mauaji ya Wenze Makongoro (23), aliyekuwa mwanafunzi wa Stashahada ya Ukutubi katika Chuo cha Bagamoyo na Jacqueline Frederick (30), mkazi wa Kisarawe.
‘’Watu hao waligundulika kuuawa Novemba 19 mwaka huu na kutupwa maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam,’’ alisema Kova.
Aliongeza kuwa baada ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao walikutwa na vielelezo mbalimbali zikiwamo suruali mbili za kike, sketi moja, kikoi kimoja, mikoba minne ya kike na simu moja aina ya Tecno.
Pia walikutwa na sidiria moja, vidani vya mikononi viwili, pete moja, hereni jozi tatu, vibanio vya nywele, vipodozi vya kike na shanga tatu.
Alisema katika mahojiano na watuhumiwa hao walijihusisha na ulaghai wa kimapenzi, utekaji nyara, kuwawekea dawa katika vinywaji watu hao na kuwanyanyasa kijinsia na kusababisha mauaji.
Alitoa onyo kwa wanawake hasa wasichana na wanafunzi wa kike kutokukubali kuingia katika mahusiano ya kimapenzi haraka na watu wasiowafahamu.
Alisema watuhumiwa hao wata- fikishwa mahakamani muda wowote kwani upelelezi umeshakamilika

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa