WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, ameonya Watanzania kujiepusha na upokeaji fedha za wagombea wanaotaka uongozi katika chaguzi mbalimbali nchini kwani kitendo hicho kinawanyima haki zao za kuchagua viongozi wenye sifa.
Bw. Sumaye aliyasema hayo Dar es Salaam jana kwenye uzinduzi wa albamu ya nyimbo na ngoma ya kwaya ya Uinjilisti Changanyikeni kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Changanyikeni, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
Alisema hivi sasa kumezuka wimbi kubwa la matumizi makubwa ya fedha ili kuwanunua wapiga kura wakati wa uchaguzi ambapo hizo ni dalili za kuwaabudu watoa rushwa.
“Hali hii inaonesha tunawaabudu watoa rushwa ambao wanatumia fedha hizo kununua uongozi wakiwa na lengo la kutuibia fedha zetu baada ya kuchaguliwa na kuingia madarakani,” alisema.
Aliongeza kuwa, kama Watanzania watakubali kitendo hicho hakuna haja ya kuanza kulalamika hasa panapokosekana maendeleo katika maeneo yao.
“Hili ni janga la demokrasia yetu, fedha hizi zinatoka wapi na watazirudishaje wakipata uongozi... kama tunakubali kumchagua kiongozi kwa sababu ametununua, tusilalamike,” alisisitiza.
Bw. Sumaye alisema kiongozi mzuri anayefaa kuwaongoza Watanzania si anayetanguliza fedha kuwanunua wapigakura bali ni yule mwenye uwezo wa kuomba kura kwa heshima na utu akieleza mipango yake kwa kushirikisha wananchi.
Katika hatua nyingine, Bw. Sumaye aliitaka jamii ichukie ufisadi na kuwachukia mafisadi akisema kwaya hiyo katika moja ya wimbo wake umeonesha kuna kundi kubwa la Watanzania ambalo halithubutu kukemea vitendo vya rushwa na ufisadi hadharani.
Alisema hali hiyo inasababisha mapambano dhidi ya rushwa kuwa magumu hivyo lazima wapambane ili washinde vita.
“Binafsi nimefurahi sana kwa sababu niko kwenye vita hii muda mrefu, napata faraja kuona jeshi hili linapoongezeka, natamani kuona wimbo huu wa “fisadi Wewe” ukipigwa katika vituo vingi vya redio...najua haitawezekana kwa sababu watoa rushwa, wala rushwa na mafisadi ni watu wenye nguvu ya fedha,” alisema.
Aliongeza kuwa, rushwa ina madhara makubwa katika jamii yakiwemo kudidimiza uchumi wa nchi, kutishia amani, utulivu na kuwaumiza wote wanaopenda haki na watu wa kawaida.
Alisema mahali penye rushwa, maskini hunyang’anywa haki yake na kupewa mwenye uwezo na kutolea mfano mahali ambapo haki inaweza kunyang’anywa kuwa ni pamoja na hospitali ambako mtoto wa maskini ananyimwa huduma kutokana na ukosefu wa fedha.
Aliyataja maeneo mengine ambayo rushwa inaweza kumnyima haki maskini kuwa ni mahakamani ambako maskini anaweza kudhulumiwa haki yake na kupewa mwenye fedha.
Chanzo:Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment