Home » » MAUAJI YA WASICHANA WAWILI YACHUNGUZWE-UWT

MAUAJI YA WASICHANA WAWILI YACHUNGUZWE-UWT

UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT), umeitaka Serikali ifanye uchunguzi wa kina kuhusu mauaji ya wasichana wawili yaliyotokea hivi karibuni Mjini Bagamoyo na Dar es Salaam katika mazingira ya kutatanisha.

Mauaji hayo yamemhusisha mwanafunzi wa Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS), mjini Bagamoyo Novemba 19 mwaka huu na mwingine kuuawa Novemba 21 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya Habari Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa UWT, Bi. Amina Makillagi, alisema Umoja huo umelaani mauaji hayo ya kinyama.

“Ukiondoa mauaji haya, kuna mengine yaliyotokea katika kipindi hicho yakihusisha wanawake na watoto, hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Serikali; hivyo UWT tunaomba hatua zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika na unyama huo.

“Serikali ihakikishe inafanya uchunguzi wa kina dhidi ya mauaji ya kinyama ya wanawake yaliyofanywa na watu wasiofahamika ili kukomesha vitendo hivyo,” alisema.

Aliongeza kuwa, Kamati ya Utekelezaji UWT imelaani mauaji yaliyotokea wakati wa mapigano ya wafugaji na wakulima kutokana na migogoro ya ardhi kwenye Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara.

Alisema kutokana na mauaji hayo, wanaiomba Serikali ichukue hatua za haraka ili kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani humo.

“Mauaji dhidi ya wakulima na wafugaji yanazidi kushamiri siku hadi siku; hivyo Serikali iwajibike kutafuta suluhu ya haraka ili kukomesha mauaji yanayoendelea,” alisema.

Kamati hiyo pia inawapongeza wanawake wa UWT-CCM, watendaji, viongozi na wananchi kwa ushiriki wanaoutoa ili kufanikisha Uchaguzi wa Serikali ya Mitaa, Vijiji, Vitongoji na kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura.

Alisema UWT inawataka wanawake, wananchi na wapenda maendeleo kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, kuwachagua viongozi wao ili kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali.

Chanzo:Majira

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa