Home » » NAKUSHAURI RAIS KIKWETE, MUACHE MUHONGO AMALIZE KIBARUA CHAKE

NAKUSHAURI RAIS KIKWETE, MUACHE MUHONGO AMALIZE KIBARUA CHAKE





Said Mwishehe

PANAPO MAJAALIWA ya Mungu, kesho tunaungana na mataifa mengine duniani kusheherekea mwaka mpya wa 2015.

Hivyo, kwa hesabu za kalenda ya mwaka 2014, leo hii tunamaliza muda uliobaki kabla ya kuingia mwaka 2015.

Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuendelea kutupa pumzi yake. Ametujaalia afya njema. Hili ni jambo la kushukuru.

Pia nitumie nafasi hii kutoa pole kwa ndugu, rafiki na jamii zetu ambao leo hii hatunao tena. Wametangulia mbele za haki.

Hiyo inatokana na mapenzi yake muumba wa mbingu na ardhi. Tuwaombee dua njema huko waliko.Mbele zao, nyuma zetu.

Wakati tunakaribia kuingia mwaka 2015, nitumie nafasi hii kuowambea wale wote wenye kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali.

Imani yangu Mungu atawaponya na kuwarejesha kwenye afya njema na hatimaye kuendele na ujenzi wa taifa.

Wakati tunajiandaa kuupokea mwaka mpya, kuna mambo mengi ambayo yametokea kwenye mwaka huu wa 2014.

Yapo ambayo yametunufaisha kama taifa lakini wakati huo huo yapo ambayo yametufedhehesha.

Mwaka 2014 ulikuwa mwaka wa matukio mengi katika nyanja mbalimbali. Nikiri kuna mambo ya kujivunia na kuna mambo ya hovyo ambayo yametokea kwenye taifa hili ambalo linaendelea na juhudi za kusaka maendeleo yake.

Sote ni mashahidi Watanzania kwa nafasi zao mbalimbali wameendelea na ujenzi wa taifa leo. Wameendelea kudumisha umoja na mshikamano wao.

Wameendelea kuungana kupigania maisha yao. Ni watu ambao hawataki kukataa tamaa. Wanafanya kila juhudi kuhakikisha taifa linasonga mbele.

Nikiri kauli ambayo inaliumiza taifa hili ni kuendelea kuimba wimbo wa "Sisi maskini". Wimbo ambao kwangu mimi unaniumiza kichwa. Sitaki hata kuusikia. Sitaki kuusikia kwasababu ni sehemu ya adui wetu wa maendeleo yetu.

Sisi maskini ni kauli ambayo imetukwamisha kwa miaka mingi sasa. Hata mwaka huu wa 2014, kauli ya sisi maskini imeturudisha nyuma.

Kujiita kila siku maskini ndio matokeo yake tunashinda kuishi maisha ya kuendelea kuomba misaada. Kisa tu nchi yetu eti maskini.

Kwangu naamini sisi si maskini ila huenda tunakosa mipango na usimamizi mzuri wa kufikia malengo yetu.hili ndilo tatizo ambalo linatusumbua kwa miaka mingi.

Mwaka 2015 ni mwaka wa kubadili mitazamo na fikra zetu. Tukitumia vema rasilimali zetu, tutapiga hatua. Kila kitu tunacho.tunachotakiwa ni mipango na usimamizi mzuri. Tuache akili za kuwa tegemezi kwa kila jambo.

Inashangaza tunapokuwa na msitu mkubwa wa misitu kama ule wa Sao hili Iringa halafu kijiti cha kusafishia meno kinatoka China. Ama kweli!

Inasikitisha kuona imefika mahali eti kila kitu lazima kitoke nje. Kasumba hii inatokana na yale yale ambayo wengi yametutawala kwenye akili zetu kuwa lazima tuwe tegemezi.

Hatupaswi kuwa na akili hiyo kwa mwaka 2015. Ni mwaka wa kutafakari kama taifa nini tufanye ili tusonge mbele.

Kwa bahati mbaya tumekuwa na kundi kubwa ambalo linatumia muda mwingi kupiga soga vijiweni kwa ajenda ambazo hazina mashiko ya kimaendeleo. Ni rahisi kusikia watu wanajadili nani kavaa nini. Fulani analula nini?

Wanaojadili tunapigaje hatua kama taifa ni wa chache. Hata hao tunaowategemea kutupigania wamekuwa wa kuishi kwa matukio. Likija tukio hili wamo, likija lingine wamo.Mafundi wa kuongoa kuliko kutenda.

Inasikitisha sana.Tumeyaona hayo mwaka 2014.Si vizuri yakajirudia tena mwaka 2015. Kufanya kosa si kosa ila kurudia kosa, ndio kosa. Tusimamie kama nchi tuangalie maisha yetu. Tumetoka wapi na tunakwenda wapi.

Tukisoma vitabu vya historia tunaambia Tanzania na China zilianza harakati za kusaka maendeleo mwaka mmoja. Nenda leo China kaingalie.

Hatufanani nayo kwa namna yoyote ile.Watu tulianza nao kwenye harakati za kutafuta maendeleo, eti leo tunawapigia magoti kuwaomba msaada.

Wachina wameijenga nchi yao.Wameamua kusimama kidete kuhakikisha taifa lao linapiga hatua na kuwa lenye nguvu duniani.  Sishangai Marekani inapokwenda kuomba misaada ya kifedha China.

Kwetu sisi maendeleo yetu yamekuwa ya mwendo wa kinyonga. Wananchi wamekata tamaa ya maisha. Kila kukicha wanasema afadhali ya jana. Ndio maisha ambayo tumeamua kuishi.

Imefika mahali Wachina wameamua kuja nchini kwetu na kufanya kazi ambazo tumeshindwa kuzifanya. Nenda Kariakoo jijini Dar es Salaam, Wachina wanauza maua.Wanauza karanga.

Inasikitisha inapofika mahali hata karanga tunashindwa kuuza. Tunasibiri Wachina waje wauze. Halafu tumebaki kupiga kelele tu.Tumefika mahali pabaya.

Sifa ya taifa kupiga hatua za maendeleo linahitaji kuwa na siasa safi, utawala bora, ardhi na watu.

Nikiri tunaweza kuwa tumekosa siasa safi na uongozi bora lakini tuna ardhi ya kutosha na watu. Kwa bahati mbaya watu wapo lakini kasi ya maendeleo haiendani na idadi yetu.

Kitendo cha kukosa siasa safi imefika mahali, wanasiasa wengi wametugeuza kama vile kichwa na mwendawazimu. Wanatuongopea watakavyo.

Wanajua hatuna tunaloweza kulifanya. Hakika mwaka 2014, licha ya kufanya mambo ya maendeleo, yapo ambayo tunapaswa kujiepusha nayo mwaka 2015.

Msomaji wa safu hii, baada ya kutoa maelezo hayo ambayo kwangu mimi kwa siku ya leo ni kama utangulizi sasa nije kwenye ajenda yangu ya Jumatano ya leo.

Ajenda yenyewe ni hili sakata la Escrow.Sakata ambalo limekuwa gumzo kwenye kila kona ya nchi yetu. Limekuwa likizungumza na kila mtu. Kama hulizungumzi wewe basi analizungumza mwenzio.

Sakata la Escrow limetikisa nchi yetu kwa sehemu kubwa. Sote tunafahamu mjadala huo wa Escrow unatokana na utata wa fedha wa sh. bilioni 306 zilizopo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, wajanja kuamua kuzichukua.

Wanasiasa wa kada mbalimbali wamekuwa wakilizungumza hilo kwa kina. Wamekuwa wakipambana kwa hoja. Wamekuwa wakijadili na kuelezea umma kuhusu fedha hizo.

Nikiri mwaka 2014, mjadala wa Escrow kwangu mimi naona ulikuwa ni mjadala uliochokuwa sehemu kubwa ya mazungumzo kuliko mijadala mingine.

Ni kweli kulikuwa na mjadala kuhusu Katiba mpya lakini ujio wa sakata la Escrow umefunika kabisa mazungumzo ya Katiba inayopendekezwa.

Kwa kuwa hata wanasiasa wetu nao wanaishi kwa matukio. Wengi wao wameachana na ajenda ya Katiba mpya ambayo wananchi wanahitaji kuelimisha licha ya wao wenyewe kujisomea Katiba inayopendekezwa kabla ya kufanya uamuzi kwa kupiga kura ya ndio au hapa.

Leo hii ili mwanasiasa aonekane amezungumza jambo la maana basi anaamini akizungumzia Escrow ndio nyota ya siasa inasafishika.

Sina tatizo na wanasiasa ambao wamelizungumzia sakata hilo hadi hapa lilipofikia. Tunajua Bunge limetoa maazimio nane kwa Serikali.

Maazimio ambayo kwa sehemu kubwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete inatakiwa kuamua kwa kuchukua hatua dhidi ya wanaohusishwa na uchotaji fedha wa Escrow.

Ndio maana aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema ameamua kuachia ngazi.

Uamuzi huo unatokana na ukweli kwamba ushauri wake kisheria hakueleweka. Jaji Werema anasema amechafua hali ya hewa.

Pia tunafahamu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi naye amsimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi. Kisa sakata hilo hilo la Escrow.

Nani ambaye hafamu kama aliyekuwa Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka naye ametemwa kwenye baraza la mawaziri.

Kilichomuondoa ni kupokea fedha za Escrow.Prof. Tibajuka aliwekewa kwenya akaunti yake binafsi sh. bilioni 1.6.

Wakati mjadala huo unaendelea, hakuna mwanasiasa ambaye ameweza kupata ujasiri wa kuliambia taifa fedha hizo ni za umma au si za umma. Nani mwenye fedha hizo?.

Ujasiri ambao wanasiasa wetu walio wengi wanao hadi sasa ni kwamba sh. bilioni 306 za Escrow ni za umma. Wamesema hivyo wakiwa bungeni na wanaendelea kusema hivyo nje ya Bunge.

Kwangu mimi na hata kwa Watanzania wengine, nimefurahishwa na hotuba ya Rais Kikwete.Hotuba ambayo aliitoa Desemba 22 mwaka huu. Alikuwa anazungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam.

Kama kiongozi wa nchi ameonesha kulifahamu vema suala hilo. Akatumia nafasi hiyo kuelezea historia nzima ya sakata la Escrow.

Akaeleza namna ambavyo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na IPTL walivyokuwa wanalipa.

Pia, akaeleza namna ambavyo akaunti ya Tegeta Escrow iliovyofunguliwa hadi hatua ya IPTL na wanahisa wenzake kuuziana hisa na kisha kufunga akaunti ya Tegeta Escrow na kuchukua fedha zilizomo.

Rais Kikwete baada ya kutoa maelezo mengi ya kueleweka pengine kuliko yale yaliyokuwa yanatolewa na wanasiasa walio wengi akatumia nafasi hiyo kuwahakikishia Watanzania kuwa fedha hizo ni za IPTL.

Rais Kikwete katika hotuba yake alisema"Fedha hizo ni za IPTL maana ni malipo ambayo yalikuwa yanalipwa kutoka Tanesco ambazo ni tozo la uwekezaji, lakini toafuti yake fedha zilikuwa zinawekwa kwenye akaunti maalumu".

Kimsingi hotuba ya rais imejibu swali la msingi ambalo Watanzania wengi walikosa kulisikia.Pamoja na kusema fedha hizo ni za IPTL bado akauthibitisha umma kuna kodi ya Serikali ndani yake.

Hivyo tunapoumaliza mwaka 2014, naamini rais amesema kile ambacho wengi tulipaswa kukisikia.Akasisitiza uchunguzi ufanyike na kisha sheria ichukue mkondo wake.

Akaagiza mamlaka zinazohusika na uchunguzi zitakapokamlisha taarifa , yeye atakuwa na uamuzi wa kufanya.

Baada ya kulifafanua kwa kina suala hilo, rais akatumia nafasi hiyo kuweka wazi Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amemuweka kiporo.

Bwana we! kauli hiyo ya Prof.Muhongo kuwekwa kiporo imeamsha hasira za wanasiasa hasa za wapinzani.

Wametoa matamko ya kumtaka Rais Kikwete kumuwajibisha Prof.Muhongo kwa kumuondoa kwenye nafasi hiyo.

Wengine wametangaza kufanya maandamano nchi nzima.Najiuliza sababu za  msingi za kufanya maandamano hayo.

Najiuliza hivi wanaotaka Prof.Muhongo aondolewe kwenye nafasi hiyo ni kweli wanashinikiza kwa maslahi ya Taifa au kwa maslahi binafsi.

Hapa kuna siri kubwa, ambayo wenye kumshinikiza rais amuondoe Prof.Muhongo kwenye nafasi ya uwaziri wanaijua. Nani ambaye hajui kazi ambayo imefanywa na Prof.Muhongo kwenye wizara hiyo.

Amefanya mambo makubwa kwa maslahi ya nchi.Waziri Muhongo kwa usimamizi wake mzuri umeme umekwenda kwenye vijiji mbalimbali vya nchi yetu.

Nimezunguka wilaya za nchi hii 129 hadi sasa.Naiona kazi ambayo Prof.Muhongo ameifanya katika nishati ya umeme.

Nani ambaye hajui umuhimu wa nishati ya umeme kwa wananchi. Misimamo yake katika wizara hiyo imefanikisha ujenzi wa bomba la gesi.Angekuwa Waziri legelege , bomba la gesi kutoka Mtwara kuja(kwenda) Dar es Salaam lisingejengwa.

Alijua anasimamia maslahi ya taifa.Pia najua kwenye eneo la gesi amekasirisha wengi.Wapo ambao hawataki hata kumsikia.Leo si wakati wake kuzungumzia hilo.

Wanasiasa wanataka rais amuondoe Prof.Muhongo, hivi waziri mwingine ambaye atakwenda kwenye wizara hiyo na kukaa kwa miezi nane iliyobaki ya utawala wa rais Kikwete anakwenda kufanya jambo gani kubwa.

Kuna dhambi gani Waziri Muhongo akiachwa amalizie muda ambao Rais Kikwete ameubakisha.

Kwa kuwa tunaingia mwaka 2015, ni bora niseme ukweli maana utaniweka huru.Naamini sioni sababu ya kumuondoa Waziri Muhongo Wizara ya Nishati na Madini.

Tangu amekuwa Waziri wa Nishati na Madini Waziri Muhongo amefanya kazi kubwa na nzuri.Hata hao ambao leo wanamuandama wanajua.

Nikiri najua, haya ninayoeleza kuna watu nawakera lakini ni bora niwe huru kwenye kile ninachoamini.

Kauli ya Mwishehe, kaushauri Rais wangu, Rais Jakaya Kikwete , nakuomba umuache Waziri Muhongo amalizie kazi anayoifanya kwenye wizara hiyo.Binafsi sioni mahali ambapo Waziri Muhongo amechukua fedha za Escrow.

Sioni mahali ambapo Waziri Muhongo ameshauri fedha zitoke. Waziri Muhongo msimamo wake unajulikana wazi kuhusu fedha hizo.

Kwa bahati mbaya wanasiasa wetu wameng'ang'ania tu kumtaka rais amuondoe Muhongo badala ya kutoa suluhu ya nini kifanyike ili hayo ambayo yanatokea na kusababisha taifa kushindwa kuchukua kodi yake yasijirudie.

Wanasiasa wanashindana kuita vyombo vya habari kumshinikiza rais kumuondoa Waziri Muhongo.

Naamini na ndio ukweli wanafanya hivyo si kwasababu ya maslahi ya taifa , bali wanafanya hivyo kwa msuko mwingine. Ipo siku nitausema.Kwenye hili nitasimamia ukweli.

Kwenye siasa za Tanzania kuna mambo huwa yanakera sana. Moja ya mambo yanayokera ni pale mtu anaposimama kujifanya anapigania maslahi ya taifa kumbe, kichwani kwake anawaza tofauti.

Kuna wakati huwa najiuliza kwanini , wanashinikiza Prof. Muhongo aondolewe. Nawaza weee , lakini napata majibu tofauti tofauti. Moja ya jibu ambalo huwa nalipata ni kwamba wanaogombea urais nao wana yao kwenye hilo.

Tena si wa CCM tu, bali hata wa upinzani. Wanaona sakata la Escrow ni karata ya mwisho ya kufanikisha malengo yao.

Wengine wanaamini kupitia sakata hilo itakuwa njia rahisi ya kuiangusha Serikali ya Rais Kikwete bungeni.

Hivyo, kila mmoja analiangalia kivyake na si kweli wote wanaopigania hilo ni kwa ajili ya maslahi ya taifa. Ingekuwa ni maslahi ya taifa wangetuambia kwenye sh. bilioni 306 za Escrow za umma ziko sh. ngapi?

Nimalizie kwa kueleza tunaingia mwaka 2015, tudumishe upendo, umoja na mshikamano wetu. Najua wapo ambao watakaosema nimetumwa. Sijatumwa. Sitajali.

Kubwa zaidi kila Mtanzania ana haki ya kutoa maoni yake kwa kile anachokiamini anaweza kuchangia alau kidogo hasa kwa kuzingatia mwaka 2014 umebakisha saa chache tu wa uhai wake.

Karibu mwaka 2015, nitumie nafasi hii kuwataka mafanikio mema kwenye mwaka wa uchaguzi wanasiasa wote. Mwaka ambao kila anayetaka kugombea udiwani, ubunge au urais anarudi kuomba kura kwetu.

Nawaheshimu wanasiasa wote na wa vyama vyote. Kwenye ukweli nipo pamoja nanyi na kwenye uongo nitakuwa kando yenu.

Tuwasiliane 0713833822

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa