Mvua kubwa isiyotabirika inatarajiwa kunyesha katika maeneo
mbalimbali nchini hasa katika ukanda wa Pwani ya Kaskazini, maeneo ya
Dar es Salaam, Tanga, Unguja na Pemba; pia katika ukanda wa Kaskazini
Mashariki kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Akitoa taarifa ya hali ya hewa jana kwa Januari na
Februari mwaka ujao, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA), Dk Agness Kijazi alisema mvua ya msimu katika maeneo
hayo inatarajiwa kwisha leo.
Hata hivyo, alisema mvua kubwa ya nje ya msimu
inatarajiwa katika kipindi cha Januari, 2015. Dk Kijazi alisema hali
kama hiyo pia itaikumba mikoa ya Kagera, Mwanza, Shinyanga na Geita.
“Maeneo mengine yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa
mwaka yatakuwa na mvua ya wastani. Maeneo hayo ni Mbeya, Rukwa, Katavi,
Iringa, Lindi, Dodoma na Mtwara.
Dk Kijazi alisema mvua hiyo inasababishwa na
ongezeko la joto linalolifanya anga kushindwa kutengeneza unyevunyevu
ambao hugeuka kuwa mvua. “Ninawashauri wananchi kuchukua hatua ya
kujikinga na athari za kiafya na mazingira zinazoweza kusababishwa na
ongezeko la joto linaloendelea sambamba na mvua kubwa inayonyesha,”
alisema Dk Kijazi.
Juzi, mvua kubwa ilinyesha jijini Dar es Salaam
kwa saa mbili na kusababisha vifo vya watu wawili katika Wilaya ya
Kinondoni kuleta kero kwa wasafiri wanaotumia vyombo vya moto na
watembea kwa miguu.
Mitaa ya Azikiwe, Bibi Titi na Morogoro ambayo juzi ilijaa maji, jana ilionekana kuwa mikavu baada ya maji yote kukauka.
huku watumiaji wa barabara wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.
Yusuph Said, mmoja wa wafanyabiashara wa magezeti
Mtaa wa Azikiwe, alisema eneo hilo hujaa maji kila mvua inaponyesha na
kuwasababishi kufanya kazi yao katika mazingira magumu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius
Wambura aliliambia gazeti hili jana kuwa hakuna madhara zaidi
yaliyotokea ukiacha matukio ya watu wawili kufariki dunia kutokana na
mvua hiyo.
Naye Kamanda wa Polisi Ilala, Mary Nzuki alisema:
“Mkoani kwangu sijapokea taarifa yoyote ya maafa yaliyosababishwa na
mvua mpaka sasa.” Kamanda Kihenya Kihenya wa Mkoa wa Kipolisi Temeke
naye alisema hajapokea taarifa yoyote ya maafa.
Akizungumzia matukio ya mvua kipindi cha Oktoba –
Disemba, 2014, Dk Kijazi alisema maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za
wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo machache ya mikoa ya Tanga,
Dar es Salaam, Dodoma (Hombolo), Kilimanjaro (Same), Njombe, Mtwara na
Lindi ambayo yalipata mvua za chini ya wastani.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa matukio ya mvua hizo ambayo
yaliambatana na vipindi vifupi vya upepo mkali, yalisababishwa na
kuimarika kwa ukandawa mvua magharibi mwa nchi ambao uliambatana na
kuwepo kwa makutano ya upepo.
“Wananchi wajenge pia utamaduni wa kupanda miti
ili kusaidia kupunguza kasi ya upepo unaombatana na mvua kubwa ambazo
zinaweza kusababisha uharibifu wa mali na madhara kwao,” alisisitiza Dk
Kijazi.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment