Home » » PENGO: KATAENI WASAKA URAIS KWA MABILIONI

PENGO: KATAENI WASAKA URAIS KWA MABILIONI

 
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ameitaka jamii kuungana kuhakikisha anapatikana rais aliye bora na kutodanganyika kuchagua mabilionea wanaotumia fedha nyingi kuelekea uchaguzi mkuu kutafuta uongozi wa nchi mwakani.
 Kardinali Pengo amesema kiongozi wa aina hiyo akishaingia madarakani hatawatumikia wananchi maskini.

Kauli hiyo ilitolewa na Kardiali Pengo wakati kukiwa na baadhi ya viongozi wa chama tawala cha CCM walioonyesha nia za kutaka kuwania nafasi ya rais katika uchaguzi mkuu ujao mwakani.

 Alitoa kauli hiyo  juzi wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari, baada ya ibada maalumu ya kutimiza miaka 70 ya kuzaliwa kwake, iliyoandaliwa na mapadri wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kufanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph.

 Alisema ili kuondoa wimbi la viongozi hao, jamii inapaswa kuungana na kuwaondoa madarakani kupitia nguvu ya umma.

“Viongozi wenye uwezo mkubwa kifedha kamwe huambatana na wenzao wenye tabia kama hiyo, hivyo ni mara chache sana viongozi kama hao kushirikiana na watu maskini,  ambo ni wengi,” alisema Kardinali Pengo.

  Alisema viongozi wa aina hiyo ndiyo chanzo cha matatizo katika jamii, ikiwamo kuleta tofauti ya kipato baina yao kwa kuvunja maadili ya uongozi.

 “Hali ya uchumi imekuwa ni mbaya, hasa kwa watu wenye kipato cha chini kutokana na kuongezeka kwa tofauti ya aliyenacho na asiyenacho. Hali hii siyo nzuri kwa amani, utulivu na ustawi wa nchi,” alisema Kardinali Pengo.

 Aliongeza: “Tunahitaji kuwa na viongozi wenye nia halisi, ambao wanaweza kuweka umakini kwa changamoto hizi ili kuwainua watu wa kawaida.”

Aliionya jamii kuacha kufikiri kwamba viongozi walio na fedha nyingi ndiyo wanaoweza kuchangia ustawi wa watu maskini ambao ni wengi.

 Alisema historia katika nchi tofauti duniani, zinaonyesha kuwapo kwa mabadiliko ya maendeleo katika nchi hizo baada ya kutumika nguvu ya umma kwa kuwaondoa viongozi wasio wawajibikaji.

 Kwa mujibu wa Kardinali Pengo, kwa sasa nchi inakabiliwa na changamoto kubwa ya tofauti ya kipato na kuporomoka kwa maadili ya watumishi umma na kusababisha rushwa.

 Kuhusu matarajio yake, alisema iwapo Mwenyezi Mungu atamjalia uhai, kabla ya kustaafu angependa kuona idadi ya parokia za jimbo kuu zimefikia 100, ambazo kwa sasa zipo 85.

 Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Titus Mdoe, alisema jamii na viongozi wana wajibu wa kujifunza kutokana na utumishi uliotukuka ulioonyeshwa kupitia utumishi wa Kardinali Pengo.

 Alisema utumishi wa Kardinali Pengo, unaweza kuelezewa kwa namna tofauti, ikiwamo uanzishwaji wa Parokia mbalimbali, ujenzi wa vituo vya afya, shule na vyuo vya ufundi.

 Naye Mwenyekiti wa Mapadri Wazalendo wa Jimbo hilo, Novatus Mbaula, alisema awali maadhimisho hayo yalitakiwa kufanyika Agosti 5, mwaka huu, lakini ikashindikana kutokana na Kardinali Pengo kuhudhuria matibabu ya afya nje ya nchi.

  “Kutokana na hali yake kiafya kuimarika, tumeamua kufanya ibada hii kipindi hiki,” alisema Padri Mbaula.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na maaskofu wasaidizi;  Askofu Eusebius Nzigilwa na Askofu Mdoe pamoja na mapadri, watawa wanaofanya kazi katika jimbo hilo na waumini.

 Kwa mujibui wa sheria za Kanisa hilo, askofu maaskofu na makardinali hustaafu rasmi katika utumishi wa kanisa wanapofikisha umri wa miaka 75.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa