Home » » SALA, MAOMBI KUDUMISHA AMANI ASEMA MAMA MARIA NYERERE

SALA, MAOMBI KUDUMISHA AMANI ASEMA MAMA MARIA NYERERE

MJANE wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, amepokea nishani ya kudumisha na kuhamasisha amani nchini, huku akimtaka kila mwananchi kwa nafasi yake kuombea taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kukabidhiwa nishani hiyo kutoka kwa Kamati ya Kitaifa ya Mkesha wa Mwaka Mpya, Mama Maria alisema sala na maombi kwa taifa, ndiyo pekee yatakayosaidia kudumisha amani iliyopo hapa nchini.
Alisema ni vyema kila mmoja pia kuwa mfano kwa kuidumisha amani hiyo kama kielelezo cha mazuri yaliyoasisiwa katika Taifa hili.
“Yapo makosa yaliyofanyika zikiwemo vurugu katika mikoa ya Arusha, Morogoro na Mtwara lakini ni vyema watu wakajirekebisha kutokana na makosa hayo ili yasijirudie tena,” alisema.
Alifafanua kuwa haina haja ya kunyosheana vidole katika makosa hayo na mengine na badala yake watu wazidishe maombi ili wasamehewe.
Alisema maombi ya kitaifa yatasaidia kuliongoza taifa huku akiasa kila mtu kuomba na kuombea taifa sambamba na kufanya kazi kwa ajili ya maisha yake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maombi hayo yanayotarajiwa kufanyika usiku wa Desemba 31, Askofu William Mwamalanga alisema nishani hiyo imetolewa kwa lengo la kutambua mchango wa mama huyo katika kuhamasisha amani.
Alisema tuzo hiyo ambayo hutolewa kwa watu maalum na walio mstari wa mbele kudumisha amani ni ishara ya kumkumbusha Mungu kwa kazi za kuendeleza amani inayofanywa na watu mbalimbali akiwemo Mama Maria Nyerere.
Alisema Watanzania wanapaswa kuidumisha amani kwa vitendo.
Chanzo;Habari Leo

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa