JAMII nchini imeonesha kuwa na uelewa mkubwa kuhusu matukio ya ukatili wa kijinsia kwa asilimia 69.2 huku yakiwepo baadhi ya matukio ambayo yameshindwa kupungua kutokana na kuendelezwa kwa mila na desturi.
Ripoti ya awali iliyotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) juu ya ukatili, inaonesha elimu ambayo imekuwa ikitolewa ndiyo kichocheo kikubwa kwa matukio hayo kufahamika kwa jamii.
Akizungumzia ripoti hiyo jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valerie Msoka alisema mwaka 2012 jamii ilikuwa na uelewa wa matukio hayo kwa asilimia 56 pekee.
“Elimu inayotolewa hivi sasa juu ya matukio ya ukatili wa kijinsia imekuwa ndiyo sababu kubwa kwa jamii kuwa na muamko wa kutoa taarifa ya ukatili bila kuwa na woga ingawaje wapo baadhi ambao wanakatishwa tamaa na Mahakama pamoja na Polisi katika kushughulikia kesi hizo,†alisema Valerie.
Alisema awali jamii ilikuwa ikichukulia matukio ya ukatili kama vipigo kwa wanawake kuwa ni kawaida na kukaa kimya, lakini kwa sasa wanaelewa kuwa ni kosa kisheria baada ya kuelimishwa.
Kuhusu utafiti huo alisema ulifanyika katika wilaya 10 zikiwemo tatu za visiwani ambazo ni (Pemba Kaskazini), Magharibi (Unguja Mjini Magharibi), Unguja Kusini na 7 za Tanzania Bara ambazo ni pamoja na Kisarawe (Pwani).
Msoka alisema kuwa utafiti huo uliofadhiliwa na Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania utasaidia kuendelea kufichua hali halisi ya vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake na watoto vikiwemo, ukeketaji, ubakaji, vipigo kwa wanawake, mimba katika umri mdogo.
Kwa upande wake, mtafiti kutoka Taasisi ya Mafunzo na Utafiti katika Kituo cha MK, Ibrahimu Ugurumo, alisema masuala ya unyanyasaji wa kijinsia ni masuala mtambuka yanayogusa jamii nzima ya Tanzania yakihitaji ushirikiano wa kila mmoja katika kukabiliana nayo.
Chanzo;Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment