Mwenyekiti Wa Cuf, profesa Ibrahim Lipumba, akiwa kizimbani mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana.
Kufuatia mshtuko huo, Prof. Lipumba alitolewa kituoni hapo kimya
kimya na kuingizwa kwenye gari la polisi lenye namba za usajili TP 2566
na kukimbizwa Hospitali ya UN, iliyopo eneo la Kinondoni, jijini kwa
ajili ya uchunguzi zaidi.
Tukio hilo lilitokea jana baada ya Prof. Lipumba na wafuasi wa CUF
takribani 40, kuripoti kituoni hapo kwa ajili ya kuitikia wito wa jeshi
hilo kuripoti polisi baada ya kuwatia mbaroni juzi jioni walipokuwa
wakijiandaa kuandamana kwa amani kutoka ofisi za CUF Wilaya ya Temeke
kuelekea eneo la mkutano wa hadhara Zhakem, Mbagala kwa ajili ya
kumbukumbu ya miaka 14 ya mauaji ya wenzao zaidi ya 30 waliouawa mwaka
2001 na polisi katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa
Zanzibar wa mwaka 2000.
Prof. Lipumba alikutwa na maswahibu hayo jana saa 6:30 mchana
wakati akiwa chini ya uangalizi wa polisi kituoni hapo kwa takribani saa
tatu akisubiri hati ya mashitaka kwa ajili ya kupelekwa mahakamani.
Awali, Prof. Lipumba aliwasili kituoni hapo akiwa kwenye gari lake
lenye namba za usajili T467 BLJ, saa 4:42 asubuhi akitanguliwa na
wafuasi wa chama chake kwa takribani nusu saa.
PROF. LIPUMBA AZUNGUMZA
Baada ya Mwenyekiti huyo na wenzake kuhojiwa na jeshi hilo kwa
takribani dakika 30, alizungumza na waandishi wa habari waliokuwa
wamefurika eneo hilo akisema kwamba aliitwa kituoni hapo kwa ajili ya
kuhojiwa.
“Tumehojiwa na tumetakiwa kila mmoja kuwaleta wadhamini wawili
watumishi wa serikali, lakini kutokana na masharti hayo, wanasheria wetu
walizungumza na Jehi la Polisi ili kuwaomba kwamba itawawia vigumu
kuwapata wadhamini hao kutokana na makosa yanayotukabili. Hivyo
tumejidhamini sisi wenyewe na kesho (leo) saa mbili asubuhi tutakuwa
hapa kwa ajili ya kuchukua hati ya kupelekwa mahakamani,” alifafanua
Prof. Lipumba.
Akizungumza kuhusu vurugu hizo, mwanasiasa huyo mkongwe alisema
wameshtakiwa kwa kosa la kuandamana bila kibali maalum cha kufanya hivyo
kutoka kwa jeshi hilo, sababu ambayo aliipinga.
Alisema aliliandikia jeshi hilo barua ya kuomba kibali Januari 22,
mwaka huu, lakini hakujibiwa hadi Januari 26 saa 12 jioni, kuwa
maandamano yamezuiliwa, wakati tayari ameshaondoka ofisini na wanachama
wa chama hicho wameshafanya maandalizi.
“Nilichokifanya jana (juzi), siyo maandamano bali nilikuwa nakwenda
kuwazuia wanachama ambao tayari walikuwa wameshajiandaa kwa ajili ya
maandamano na mikutano ya hadhara,” alisema Prof. Lipumba na kuongeza:
“Asubuhi siku ya pili nilikwenda kuwataarifu wanachama wa CUF
Temeke kuhusu kuahirishwa kwa maandamanao hayo. Wakati nakwenda
Mbagala kuwapa taarifa vijana waliokuwa wameshakusanyika katika viwanja
vya Zakhem nilikutana na askari ambao walinizuia na kuanza kunihoji.
Baada ya kutoa maelezo yangu walinielewa, lakini baada ya muda mfupi
nilishangaa kuona hali imebadilika baada ya kupokea simu kutoka kwa mkuu
wa polisi aliyeamuru tufukuzwe.”
Alisema kufuatia amri hiyo, walianza kufanyiwa vurugu ambazo
ziliwasababishia wafuasi wanne wa chama hicho kujeruhiwa akiwamo Kaimu
Naibu Katibu Mkuu wa chama, Sheweji Mketo na Mkurugenzi wa Mawasiliano
wa Chama, Abdul Kambaya.
Kufutia kitendo hicho, Prof. Lipumba alilitupia lawama Jeshi la
Polisi na kudai kuwa linafanya kazi kwa shinikizo la siasa na kwamba
yeye na chama chake wako imara na wataendelea kupambana hadi mwisho.
“Siku zote mfa maji haishi kutapatapa. Suala hili linaonyesha wazi
kuwa Chama Cha Mapinduzi kimeishiwa hoja ndiyo maana kinatumia nguvu za
jeshi kuzima demokrasia za upinzani,” alisema.
Aliongeza kuwa huo ni mwanzo wa mapambano na kwamba wataendelea
kufanya mikutano yao kwani kila mwaka wamekuwa wakifanya kumbukumbu ya
mauaji ya wenzao bila kizuizi, lakini alishangaa sababu zilizofanya
wazuiliwe mwaka huu.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Abdul Kambaya, alisema
analishngaa jeshi hilo kutumia zana za kutengenezea magari kama vile
koleo kwa ajili ya kuwadhibiti wahalifu.
“Nilipigwa na spana ya kufungulia magari hapa kichwani,
ninavyoongea hadi sasa bado kichwa changu kinavuja damu. Jeshi la Polisi
halitendi haki na haliwezi kutumia zana ngumu kuwaadhibu watuhumiwa.
Mimi nimepasuliwa kichwani, wenzangu kwenye mabega na mgongoni, hivi
hawana silaha au walikuwa na dhamira ya kutuua?” alihoji Kambaya.
Baadhi ya wananchi waliokuwa katika maeneo hayo, walikilaani
kitendo kilichofanywa na jeshi hilo kwani wamemdhalilisha Mwenyekiti
huyo.
AFIKISHWA KORTINI
Wakati huo huo, Prof. Lipumba jana alifikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya kushawishi wanachama
kutenda kosa la jinai.
Profesa Lipumba alisomewa mashitaka hayo saa 9:22 alasiri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Isaya Arufani.
Kabla ya kusomewa mashitaka hayo, saa 7:45, Prof. Lipumba,
alifikishwa katika viunga vya mahakama hiyo akiwa chini ya ulinzi wa
askari kanzu.
Watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa chama hicho walifurika katika
viunga hivyo huku wakiwa kwenye makundi wakijadili kuhusu kiongozi wao
kufikishwa mahakamani.
MASHITAKA
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mawakili wa Serikali, Joseph Maugo
na Hellen Moshi, ulidai kuwa kati ya Januari 22 na 27, mwaka huu
mshtakiwa akiwa kama Mwenyekiti wa CUF mahali tofauti jijini Dar es
Salaam, aliwashawishi wafuasi wa chama hicho kutenda kosa la jinai.
Maugo alidai kuwa mashitaka yanayomkabili mshtakiwa yana dhamana
kwa mujibu wa sheria na kwamba upande wa Jamhuri hauna pingamizi la
dhamana dhidi ya mshtakiwa.
“Mheshimiwa hakimu, upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika tunaomba tarehe nyingine ya kutajwa” alidai Maugo.
Hakimu Arufani alisema mshtakiwa anatakiwa kusaini hati ya dhamana
yenye thamani ya Sh. milioni 2 na wadhamini wawili watakaosaini hati
yenye thamani hiyo ya fedha.
Hilda Mria, Diwani wa Kinondoni wa CUF na Mbunge wa Viti Maalum, Kuruthumu Mchuchuri, walimdhamini Mwenyekiti huyo.
Hakimu alisema mshtakiwa yuko nje kwa dhamana hadi Februari 26, mwaka huu kesi itakapotajwa.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment