Hatua hiyo ilifikiwa na Makinda baada ya wabunge wote wa upinzani
kusimama bungeni na kugoma kukaa chini ili kuruhusu shughuli za Bunge za
jana asubuhi kufanyika.
Shughuli hizo ni pamoja na taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na
Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Taarifa hizo zilipangwa kuwasilishwa katika kikao cha Bunge cha jana asubuhi kabla ya wabunge kupewa fursa ya kuzijadili.
Wabunge wa upinzani walfikia hatua hiyo wakipinga mwongozo
uliotolewa na Makinda dhidi ya hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa
Kuteuliwa, James Mbatia, ambaye alitaka Bunge lisitishe shughuli zake za
jana ili kujadili kwa dharura suala la kudhalilishwa kwa Lipumba na
wafuasi wengine wa CUF.
Mbatia aliomba mwongozo huo baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika bungeni.
Alipopewa nafasi, alitoa hoja ya kulitaka Bunge lijadili kwa
dharura suala la Jeshi la Polisi kumkamata, kumpiga na kumdhalilisha
Prof. Lipumba na wananchi wengine waliopigwa mabomu ya machozi na jeshi
hilo.
Mbatia alisema kitendo hicho kinahatarisha amani ya Taifa kwa kuwa
Prof. Lipumba ni mwenyekiti wa chama, ambacho kina wabunge wengi ndani
ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia ni mwenyekiti wa
chama kinachounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani Zanzibar.
Alisema Jeshi la Polisi wakati likitekeleza suala hilo lilisema
kuwa limepata maagizo kutoka juu, hivyo akataka suala hilo lijadiliwe
ili ijulikane kuwa uko juu, ambako agizo lilitoka ni wapi.
“Hili Jeshi la Polisi lilisema kuwa limepata maagizo kutoka juu,
nadhani tunahitaji kujua huko juu, ambako agizo hilo lilitoka kwa nani
na kwa lengo gani?” alihoji Mbatia.
Alisema matukio ya Jeshi la Polisi kupokea maagizo ya kuvunja amani
na kuyatekeleza yanahatarisha amani ya nchi na kwamba, suala hilo
lisiposhughulikiwa mapema, linaweza kusababisha madhara makubwa kwa
taifa.
“Mheshimiwa Spika, tusipoziba ufa, utajenga ukuta. Mwaka juzi
waandishi wa habari waliuawa, matukio ya aina hii yanaendelea na yana
madhara makubwa. Natoa hoja Bunge lako Tukufu liahirishe shughuli zake
za leo ili tujadili suala hili kwa uzito wake,” alisema Mbatia.
Baada ya kutoa hoja hyo, wabunge wote kutoka vyama vya upinzani walisimama kuasharia kuiunga mkono.
Hata hivyo, Spika Makinda alisimama na kusema kwa mujibu wa kanuni, hoja za aina hiyo, huwa haziungwi mkono.
Alisema badala yake, kanuni inaelekeza kuwa Spika ataangalia
mazingira na uzito wa hoja kwa kadri anavyoona inafaa na kuamua
ijadiliwe au isijadiliwe bungeni.
Hata hivyo, alisema hoja hiyo ni kubwa na nzito, hivyo akaitaka
serikali itoe kauli kabla ya Bunge kuanza kuijadili na kutoa uamuzi leo.
Makinda aliwaomba wabunge kuendelea na shughuli za Bunge za siku ya
jana ili kutoa nafasi kwa serikali kujiandaa kulitolea kauli suala hilo
bungeni.
Hata hivyo, mwongozo huo wa Spika Makinda ulipingwa na wabunge wa upinzani na kuzua tafrani bungeni.
“Kwa mazingira haya naagiza serikali kesho (leo) itoe kauli na ndipo turuhusu mjadala,” alisema Makinda.
Baada ya kutolewa kwa mwongozo huo, wabunge wote wa upinzani
walisimama kuupinga, jambo lililomfanya Makinda kuketi kwenye kiti chake
kwa zaidi ya dakika tano, kupisha malumbano yasiyo rasmi baina ya
wabunge wa upinzani na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika kujaribu kuwatuliza, Makinda alisikika akiwaeleza wabunge
hao kuwa mwongozo alioutoa ni sahihi na unazingatia kanuni, hivyo kama
hawaridhiki wanaweza kufanya kile walichokusudia.
“Kama mnataka kufanya mnachotaka kufanya fanyeni, lazima tutumie
busara, kama mnataka kutoka tokeni, lakini huo siyo mtindo wa kufuata
kanuni,” alisema Makinda huku akimwita Katibu aendelee na shughuli
inayofuata.
Hata hivyo, wabunge wote wa vyama vya upinzani waliendelea
kusimama, huku wakipiga kelele za kupinga mwongozo uliotolewa,
wakishinikiza suala hilo lijadiliwe wakati huo.
Jitihada za Spika Makinda kuwataka wabunge hao kukaa kwenye viti vyao, ziligonga mwamba.
Hali hiyo ndiyo iliyomlazimisha kuahirisha kikao cha Bunge cha jana
asubuhi hadi jioni. Hata hivyo, jioni Spika aliliahirisha tena Bunge
hadi leo.
NJE YA BUNGE
Nje ya Bunge, baadhi ya wabunge walitoa maoni kuhusiana na tukio hilo.
Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walidai kuwa wenzao wa
upinzani wamekosa uvumilivu na wameonyesha utovu wa nidhamu, huku
wabunge wa upinzani wakiunga mkono hatua hiyo.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, alisema kuwa wanapuuza
suala hilo kwa sababu wameshaona kuwa ni sahihi wapinzani kuonewa,
kupigwa na kunyanyaswa, hivyo suala hilo ni kama haliwagusi.
“Sisi wapinzani kila wakati tumekuwa tukinyanyaswa na kupigwa, mimi
mwenyewe wananiandama kila wakati, katika mazingira kama haya siwezi
kuona suala hili likianza kupigwa danadana, tunajua hiyo ni janja yao ya
kutaka wajipange namna ya kuzima hoja yetu,” alisema Nasari.
Alisema wamegundua kuwa lengo la Spika ni kuchelewesha mjadala wa
suala hilo ili Prof. Lipumba afikishwe mahamani na baadaye wazuie suala
hilo kujadiliwa kwa madai ya kuingilia muhimili wa Mahakama.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema kitendo cha wabunge
wa upinzani kutotii maagizo ya Spika siyo cha kiungwana na kwa kufanya
hivyo wameliingiza taifa hasara.
Alisema wabunge wote tayari walikuwa wamelipwa kwa ajili ya kufanya
kazi za kibunge za jana, hivyo kitendo chao cha kugomea maelekezo ya
Spika na kusababisha Bunge kuahirishwa kinamaanisha kuwa fedha
walizolipwa zimepotea kwa kuwa hawakufanya kazi iliyokusudiwa.
“Ingawa unaweza usiione hasara hii moja kwa moja au ukaona kama
wamefanya kazi nusu siku, lakini ikitokea kazi, ambazo zilipaswa
kufanyika leo zikapangiwa siku nyingine, maana yake ni kwamba, lazima
walipwe fedha nyingine kwa ajili ya siku hiyo kwa kazi, ambazo
zingepaswa kufanywa leo, hii ni hasara kubwa kwa taifa,” alisema
Mwigulu.
Hata hivyo, Mwigulu aliungana na wabunge hao kwa kukiri kuwa
kitendo alichofanyiwa Prof. Lipumba cha kupigwa na kukamatwa na Jeshi la
Polisi siyo cha kiungwana na wabunge hao wako sahihi kuhoji suala hilo.
Alisema kosa la wabunge hao ni kutotii maelekezo ya Spika na kwamba
kitendo hicho ni utovu wa nidhamu, ambao kama utaendekezwa itakuwa
vigumu kuendelea kuliongoza Bunge katika njia iliyo sahihi.
Alisema licha ya wabunge hao kusababisha shughuli za leo
kusitishwa, bado hoja hiyo itajadiliwa leo kama ambavyo Spika alielekeza
na hivyo walichofanikiwa ni kuliingiza taifa hasara kwa kuzuia shughuli
za Bunge za jana asubuhi kufanyika.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ester Bulaya, alisema wabunge wa
upinzani licha ya kuwa na hoja yenye mashiko, wamekosea kutotii
maelekezo ya Spika.
Alisema kitendo cha wabunge hao kinapanda mbegu mbaya kwa kizazi
cha Kitanzania, ambacho kinaweza kuanza kuiga tabia mbaya ya kuwagomea
viongozi wao.
Mbunge wa Ileje (CCM), Aliko Kibona, alisema Watanzania wameridhia
utawala wa sheria, hivyo polisi kama wataendelea na vitendo vyao hivyo,
watashindwa kufanya kazi.
Hata hivyo, alisema mwongozo uliotolewa na Spika alitegemea kuwa wabunge wangevuta subira.
Hata hivyo, Mbatia aliwaambia waandishi wa habari katika viwanja
vya Bunge baada ya Bunge kusitishwa jana asubuhi kuwa hawawezi kusubiri
kama hadi leo kama alivyoamua Spika.
Alisema hiyo inatokana na kwamba, iwapo Prof. Lipumba na wafuasi
wengine wa CUF waliokamatwa watafikishwa mahakamani, inaweza kujengwa
hoja bungeni kwamba, kadhia hiyo isijadiliwe kwa kuwa suala hilo liko
mahakamani.
Juzi Jeshi la Polisi lilitumia nguvu kuwatawanya wafuasi wa CUF kwa
kurusha mabomu, risasi za moto na maji ya kuwasha na kumkamata Prof.
Lipumba na wafuasi wengine 32.
Nguvu hiyo ya polisi ilitumika wakati wa kuzuia msafara wa Prof.
Lipumba kuelekea eneo la Zakhem, Mbagala, kulikokuwa kumeandaliwa
mkutano wa hadhara, kutoa taarifa kwa wafuasi waliokuwa wamekusanyika
kuwa mkutano na maandamano yamezuiliwa na polisi.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment