
Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM leo inaketi
kutoa hatima ya makada wa chama hicho waliotajwa kuhusika katika kashfa
ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kikao hicho kitakuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa
CCM - Bara, Philip Mangula kama ilivyoagizwa na Kamati ya CCM
iliyokutana wiki iliyopita.
Walioitwa katika kamati hiyo ni aliyekuwa Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye
ni mjumbe wa Halmashauri Mkuu (NEC) na Kamati Kuu ya CCM (CC) pamoja na
wajumbe wa NEC, Andrew Chenge (Mbunge wa Bariadi Magharibi) na William
Ngeleja (Sengerema).
Kwa kuwa uamuzi wa CC unasisitiza utekelezaji wa
maazimio ya Bunge, kwa vyovyote unamlenga pia Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye mpaka sasa amewekwa kiporo.
Kamati Kuu iliyofanyika Januari 13, mwaka huu
Zanzibar iliazimia kuwa hatua za kimaadili zichukuliwe kwa wote
waliohusika na ukiukwaji wa maadili kwenye sakata la Escrow ambao wako
kwenye vikao vya uamuzi vya CCM.
Pia kikao hicho kiliitaka Serikali kuendelea
kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu sakata hilo ambalo lilikiweka chama
hicho katika wakati mgumu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliomalizika hivi karibuni.
Kutokana na azimio hilo, Ngeleja, Profesa
Tibaijuka na Chenge wanakabiliwa na adhabu ya kuvuliwa nyadhifa
walizonazo ndani ya vikao vya amuzi vya CCM.
Makada hao walitajwa bungeni kuwa walipokea
mamilioni ya shilingi kutoka katika akaunti ya VIP Engineering
inayomilikiwa na James Rugemalira. Chenge na Profesa Tibaijuka walipokea
Sh1.6 bilioni wakati Ngeleja alipokea Sh40.4 milioni.
Hata hivyo, Ngeleja anayetajwa kutaka kuwania
urais anaweza kukumbwa na adhabu nyingine iwapo atabainika kuwa
alikwenda kinyume na adhabu aliyopewa pamoja na wenzake watano ya
kuhusishwa na ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa
na chama hicho kugombea nafasi hiyo.
Adhabu hiyo aliyopewa Ngeleja pamoja na Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye,
January Makamba, Bernard Membe na Stephen Wasira inamalizika Februari
mwaka huu na baada ya hapo itafanyika tathimini kuona kama walizingatia
masharti ya adhabu zao.
Kwa mujibu wa taarifa ya CC, ambao hawakuzingatia masharti wataongezewa adhabu.
Tayari uteuzi wa Profesa Tibaijuka umeshatenguliwa
na sasa Rais Kikwete anasubiriwa kumtangaza mrithi wake na kumalizia
‘kiporo’ cha Profesa Muhongo.
Maazimio ya Bunge
Azimio la pili la Bunge lilitaka Waziri wa Nishati
na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka
yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
Kati ya hao wote, mtu pekee ambaye mpaka sasa bado hajachukuliwa hatua yoyote ni Profesa Muhongo.
Jaji Frederick Werema ameshajiuzulu nafasi yake ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Eliakim Maswi aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini alisimamishwa kazi na Bodi ya Tanesco
imeshaundwa mpya.
Bunge pia liliazimia kuwa Chenge na Ngeleja ambao
walikuwa wenyeviti wa kamati za Bajeti na ile ya Katiba, Sheria na
Utawala, mtawalia, kuvuliwa nyadhifa zao, jambo ambalo bado linasuasua.
Sakata la Escrow pia linaweza kuwaathiri wanasiasa
hao kwa upande mwingine kwa kuwa wote bado wana nia ya kutetea nafasi
zao za ubunge katika majimbo yao.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment