Siku zote Watanzania tunafahamu kuwa soka ni mchezo unaopendwa
na mashabiki wengi siyo katika ardhi yetu pekee bali kote ulimwenguni.
Hakuna shaka kwamba ushabiki na mapenzi hayo ya
soka vinaonekana kwa watu ambao wamekuwa wakijikamua na hivyo kulipa
viingilio na kisha kuingia katika viwanja mbalimbali ili kushuhudia
mechi mbalimbali.
Ushahidi upo wazi wa jinsi ambavyo soka
inavyopendwa na vijana kwa wazee na kwa ufupi ni mchezo ambao hauna
rika, haujali kipato cha mtu.
Kwa bahati mbaya, soka katika nchi yetu imekuwa
ikichezwa na wakati mwingine kukumbwa na matukio ambayo hayapendezi wala
kuvutia, yakiwamo ya vurugu zinazotokea kwenye viwanja vyetu vingi.
Mechi za Ligi Daraja la Kwanza zinazoendelea
katika viwanja mbalimbali nchini, ikiwamo mchezo wa Majimaji na
Kurugenzi Mafinga kutoka Iringa zimekumbwa na vurugu kubwa baada ya timu
hizo kumaliza kwa sare ya bao 1-1.
Tunakemea vitendo hivi vya utovu wa nidhamu
ambavyo vimejitokeza kwenye mechi za ligi, ikiwamo michezo inayohusisha
vyombo vya ulinzi na usalama, hususan timu zinazomilikiwa na Jeshi la
Polisi. Timu hizo za Polisi Dodoma, Tabora na Mara zimetoa mfano na
nidhamu mbaya baada ya kuhusika katika matukio ya vurugu nyingi ambako
waamuzi wamepigwa na kuumizwa.
Tunajiuliza swali ambalo wasimamizi wa ligi, kwa maana ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi lazima walijibu.
Je, wamejiandaa vipi katika kuwalinda waamuzi
ambao wamekuwa wakishambuliwa, kuumizwa na wachezaji au mashabiki kwenye
mechi ambazo zinahusisha timu za Polisi?
Kama sivyo, je, wamejiandaa vipi kukabiliana na
matukio hayo maovu kwenye mechi ambazo timu hizo za Polisi zinawania
kuingia Ligi Kuu?
Tunaishauri TFF na Bodi ya Ligi wachukue hatua
zote zinazofaa ili kuzuia matukio hayo maovu kwenye viwanja vya soka
yanayozidi kuota mizizi katika siku za karibuni.
Tunawashauri TFF lazima wachukue hatua, zikiwamo
za kuhakikisha ulinzi unakuwa wa kutosha, hasa kwenye mechi za Polisi
ambazo zina rekodi ya kufanyika vurugu kama ambazo imeshuhudiwa waamuzi
kufanyiwa vitendo vya kikatili.
Ni wazi TFF na Bodi ya Ligi lazima wachukue hatua
zikiwamo za kutoa adhabu kwa wahusika ambao wanachafua sifa za mchezo wa
soka katika nchi yetu.
Tunasema, TFF waweke mikakati madhubuti ikiwezekana wakati wa
mechi za ligi hiyo zinazohusisha polisi, watafute walinzi wakiwamo wa
vyombo vingine vya ulinzi kama Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambao
wanao polisi jeshi, yaani ‘Military Police’ ambao watasaidia kulinda
amani na kudumisha amani kwenye viwanja.
Pia, tunalishauri Jeshi la Polisi lichukue hatua
na kuwafunza askari wao namna ya kulinda amani kwenye viwanja vya soka
kwa kuangalia wenzao wa Ulaya, ambao huingia kwenye viwanja siyo kama
mashabiki, bali walinzi wanaotimiza wajibu wao.
Tunasema kuwa bado tuna imani kubwa kwa polisi
wetu na tunaamini kuwa wanaiweza kazi yao, hivyo wasiache matukio ya
vurugu viwanjani yawachafulie jina lao na kazi nzuri ambayo wanaifanya.
Tunaamini, polisi wetu hawajashindwa katika kazi
hii ya kulinda na kudumisha amani kwenye viwanja vyote vya soka, tatizo
ni kuwa hawako tayari kwa kazi hiyo ambayo ni nyeti, hata kama wao
hawaoni umuhimu wake.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment