TAASISI ya Tanzania
Islamic Peace Foundation (TIPF), imesema sakata la kashfa ya uchotwaji
wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, limegeuzwa kuwa mtaji wa
kisiasa zaidi.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Shekhe Sadiki Godigodi, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, baadhi ya wagombea urais katika Mchaguzi Mkuu mwaka huu, wamejipanga kuwachafua wanasiasa wenzao kupitia sakata hilo.
Shekhe Godigodi alisema Rais Jakaya Kikwete tayari ameanza kuchukua hatua kwa watu waliotajwa kuhusika na sakata hilo na kulitolea ufafanuzi Desemba 22,2014 alipohutubia Taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Kama Rais Kikwete tayari amechukua hatua na kulitolea ufafanuzi, iweje leo kila kukicha watu waendelee kuchafuliwa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii,” alihoji.
“Taasisi yetu imefanya uchunguzi wa kina na kulifuatilia kwa karibu suala la Escrow na kubaini suala hili lipo kisiasa zaidi kuliko uhalisia wenyewe.
“Utafiti wetu umeanzia katika ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambayo imeeleza wazi kuwa kampuni ya VIP iliuza hisa zake asilimia 30 kwa halali, kulipa kodi na haimchagulii Bw. James Rugemalira marafiki wala kumpangia utaratibu wa kuzitumia fedha zake,” alisema.
Aliongeza kuwa, kutokana na maelezo ya PAC ni wazi kuwa hakuna kosa lolote la viongozi wa dini, wanasiasa na watu wengine waliopewa fedha na Bw. Regemalira kwa makubaliano wanayoyajua wenyewe.
Alisema kitendo cha viongozi na wanasiasa kuomba misaada kutoka kwa watu, kampuni na taasisi mbalimbali ili kutatua kero za wapigakura ni jambo la kawaida kwani mara nyingi wamekuwa wakipewa misaada ya fedha, bati, nondo, saruji, vifaa vya michezo.
“Kama ukweli ndio huo, iweje leo wanasiasa na viongozi waliopewa fedha na Bw. Rugemalira wasakamwe...tulichokiona, hapa ajenda kuwa na mambo ya kisiasa, tunampongeza Rais Kikwete kwa umakini wake wa kutekeleza maazimio ya Bunge.
“Rais Kikwete ametumia vizuri madaraka yake kwa kuheshimu misingi ya utawala bora ikiwa ni pamoja na kutomhukumu mtu bila kumpa nafasi ya kujitetea ndio maana akaagiza uchunguzi ufanyike ili aweze kujiridhisha kama wana makosa au ni uzishi,” alisema Shekhe Godigodi.
Aliishauri mihimili mingine Bunge na Mahakama, iige busara na hekima za Rais Kikwete kwa kufanya uchunguzi wa kina, kuwahoji watuhumiwa na aliyewapa fedha kabla ya kuwahukumu badala ya kukurupuka kuwaadhibu.
Shekhe Godigodi alitoa wito kwa Watanzania kuwa makini kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu kwani mengi yatasikika yakiwa na lengo la kuwachafua baadhi ya watu wanaoonekana kuwa na mvuto katika jamii kwa uzalendo na uadilifu wao.
Chanzo:Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment