Home » » UCHAGUZI MITAA, K’NDONI WATANGAZA KIAMA KWA WATENDAJI

UCHAGUZI MITAA, K’NDONI WATANGAZA KIAMA KWA WATENDAJI

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, imetangaza kuwachukulia hatua kali watendaji wote ambao wamelalamikiwa kukiuka sheria za uchaguzi na kutangaza matokeo ya Serikali za Mitaa kinyume cha sheria.

Akizungumza na Majira mwishoni mwa wiki, Meya wa Manispaa hiyo, Bw. Yusuph Mwenda, alisema wapo baadhi ya watendaji waliolalamikiwa hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

"Malalamiko dhidi ya watendaji hao yametolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vingine kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF), hivyo lazima sheria ichukue mkondo wake," alisema Bw. Mwenda.

Alisema kutokana na malalamiko hayo, inaonesha kuwa baadhi ya watendaji si waaminifu ambapo suala hilo lisiposhughulikiwa linaweza kuleta matatizo kwenye chaguzi zinazokuja hivyo kuharibu mpangilio mzima wa uchaguzi.

Katibu wa Wilaya hiyo, Bw. Athuman Shesha, alisema maeneo mbalimbali yaliyolalamikiwa ni pamoja na Michungwani, Kimara Stop Over ambapo watendaji pasipo kujua wanavunja sheria za uchaguzi, walitangaza matokeo kwa nguvu na kusema wagombea wa CHADEMA walishinda.

"Eneo lingine ni Mbopo lililopo Mabwepande, Mtendaji alikataa kura 36 na kusema zimearibika wakati zilikuwa kwenye boksi la wajumbe na kusababisha mgombea wa CCM kushindwa kwa kura moja na mgombea wa CHADEMA," alisema.

Aliongeza kuwa, eneo lingine ambalo Mtendaji alitangaza ushindi kwa CUF ni Bonde la Mpunga ambapo kura zilizidi baada ya kuongezwa kutoka eneo la Ananasifu.

Alisema wasiwasi uliopo, inawezekana baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi wasiokuwa waaminifu walijua mchezo huo ambapo fujo zilizofanywa na wafuasi wa vyama vya upinzani zilisababisha watu wengi waliojiandikisha kutokwenda kupigakura.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa