SIKU
moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Bw. Freeman Mbowe na Mbunge wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila
(NCCR-Mageuzi), kuituhumu Ikulu kupitia Gazeti la Tanzania Daima, jana
Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imejibu madai hayo.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi hiyo, ilisema gazeti hilo liliandika habari katika ukusara wa mbele ikiwa na kichwa cha habari, "Wabunge: Ikulu imetudhalilisha" ikiwakariri wabunge wawili ambao ni Bw. Mbowe na Bw. Kafulila.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, habari husika inadai kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kumteua Mwenyekiti wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kumruhusu Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuteua wajumbe wapya wa Bodi hiyo, kimewadhalilisha wabunge na kuwafanya waonekane wajinga kwa sababu maamizio yao yametupwa.
Kutokana na tuhuma hizo, Kurugenzi hiyo ilisema Rais Kikwete kamwe hajawahi kulidhalilisha Bunge au wabunge zaidi ya kufurahishwa na kazi yao nzuri, ushirikiano wao kwa Serikali yake.
Taarifa hiyo ilisema Rais Kikwete alirejea kusisitiza jambo hilo hivi karibuni na kulipongeza Bunge kwa kazi nzuri katika salamu za Mwaka Mpya kwa wananchi.
Uteuzi wa Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Profesa Mighanda Manyahi, uliofanywa na Rais wiki iliyopita, unatokana na mamlaka aliyonayo kisheria na haukulenga kumdhalilisha mtu yoyote.
Kurugenzi hiyo ilifafanua kuwa, hadhi ya sasa ya Prof. Muhongo, kama Waziri wa Nishati na Madini, bado inampa madaraka ya uteuzi kwa bodi zilizoko chini ya Wizara yake na hajapoteza sifa ya kuendelea kuwa ofisini na hivyo kukosa sifa ya kuteua wajumbe kama wanavyodai wabunge hao wawili.
Uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO na wajumbe wa bodi hiyo ni ushahidi mwingine usiopingika wa utekelezaji thabiti wa Maamizio ya Bunge lililojadili suala zima la Akaunti ya Escrow ya Tegeta na ushauri wa Bunge hilo kwa Rais hivyo kumshtumu Rais Kikwete kwa hatua yake ya kutekeleza ushauri wa Bunge ni jambo la kushangaza.
Tofauti na baadhi ya shutuma za wabunge wa upinzani, Rais Kikwete ametekeleza kikamilifu ushauri uliotolewa kwake na
Bunge katika maamizio yote manane, moja baada ya nyingine ukiwemo ushauri kuhusu Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, kuwajibishwa kwa maofisa wa umma, waandamizi serikalini.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imewashauri Bw. Mbowe na Bw. Kafulila wakubali kufuata misingi ya haki za kibinadamu katika kushughulika na watu wengine.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi na kuwataka wabunge hao kufahamu kuwa, hawawezi kuwa wapigaji mbinja (whistle blowers), wakawa wachunguzi, wakawa na mamlaka ya kukamata watu, kuwa na madaraka ya kushtaki, kuhukumu kuwafikisha watu jela na kuendelea kuwalinda.
Kurugenzi hiyo ilisema tayari wabunge hao wamefanya kazi yao ambayo ni nzuri ndani ya Bunge hivyo wawaachie watu wengine na vyombo vingine vilivyopewa mamlaka, madaraka kutekeleza yale yaliyoazimiwa Bungeni na kutolewa kama ushauri kwa Rais.
Utekelezaji huo wa masuala ya umma unapokuwa hauendi kwa mujibu wa matakwa yao, wawe tayari kukubali kwa sababu katika demokrasia nzuri kama ilivyo Tanzania na utawala bora safi, hakuna ambaye atafanikiwa kupata kila kitu anachokitaka na kama anavyokitaka.
Chanzo:Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment