Watu walikuwa wanakimbia utadhani mambomu ya
machozi yamerushwa. Wafanyabiashara walifunga biashara zao mapema
tofauti na siku za kawaida ili kunusuru siyo tu mali zao bali hata
maisha yao.
Mwenye ndugu jamaa au rafiki aliyekuwa maeneo hayo
alipia simu au kumtumia ujumbe ili kumjulia hali kama yupo salama au
ameshapitiwa na Panya Road. Siku ile ilikuwa kama filamu. Lakini kumbe
ni vijana wadogo tu inawezekana kudhibitiwa.
Kama hiyo haitoshi ilidaiwa kuwa baadhi ya vijana
wa kundi hilo baada ya kuona watu wengine wamefunga biashara zao na
kukimbia kwa ajili ya usalama wao, walikuwa wanarukia kwenye magari
yaliyokuwa yanatembea barabarani na kuvunja vioo vya magari.
Watakachokutana nacho halali yao.
Hata hivyo jioni polisi walitoa ufafanuzi juu ya
taharuki hiyo iliyokuwa imetokea na kusambaza na vyombo mbalimbali vya
habari hapa nchini pamoja na mitandao ya kijamii. Kauli ya kiusema kuwa,
Jeshi la Polisi lipo salama na kwamba watahakikisha amani inakuwepo na
kwamba hao vijana hawawezi kulishinda Jeshi la Polisi.
Kauli hiyo nzito ilitoa matumaini. Angalau baada
ya hapo watu walifarijika kidogo kuona kuwa polisi wanadhibiti hali
hiyo. Kesho yake wakasema kuwa wamewakamata baadhi yao.
Haikuishia hapo, Jeshi la Polisi liliendelea na
msako katika maeneo mbalimbali ya jiji hili. Vijana waliyokuwa wadhani
kuwa ni wanachama wa kundi hilo walikuwa wanachukuliwa na polisi na
kupelekwa kituoni kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Nilishuhudia moja ya kamatakamata hiyo katika
Kituo cha Daladala cha Segerea. Polisi walikuwa wanakamata kila kijana
aliyekuwa amekaa bila shughuli yoyote. Kwa sababu inasemekana kuwa kundi
hilo linaundwa na vijana wa mtaani, wavuta bangi na wasiokuwa na ajira.
Kwa hiyo kijana aliyekuwa na mwonekana wa kuvaa ovyo hakusalimika.
Nilisikia kuna wale waliotoa kitu kidogo
wakaachiwa. Sasa sijui kweli au ni maneno ya watu tu. Mimi na wewe
hatufahamu. Nadhani mbinu nyingine inahitajika hapa.
Hata hivyo, lazima tujiulize mwaka jana kundi hili
hili liliibuka na vuguru za namna hii. Mengi yalisemwa kuhusu kundi
hilo na baada ya muda hali ilikuwa shwari. Ikasemekana kuwa waliibuka
baada ya mwenzao kuuawa kutokana ana kufanya uhalifu.
Awamu hii tena inadaiwa kuwa walianzisha fujo hizo
baada ya mwenzao kuuawa. Sasa kila mara hali hii imekuwa ikijitokeza
kwa kundi hilo la vijana na watu wanaishi kwa wasiwasi.
Ni vyema tujiulize hivi hawa vijana ni kina nani,
wanaishi wapi. Inawezekana ni wenzetu, ndugu zetu marafiki zetu lakini
tunawanyamazia. Sidhani kama hatua madhubuti zikichukuliwa kundi dogo
kama hili linaweza kushinda maelfu ya watu wa jiji hili. Tusisubiri hadi
wao waibuke huko waliko na kufanya vurugu ndiyo na sisi tuanze
kuwasaka.Tena kuwasaka huko huenda wakati mwingine kukawa kwa kubahatisha ili
kuwaondoa wananchi hofu. Inawezekana wale waodhaniwa kuwa ni panya road
siyo na wasiyodhani wapo wanasubiri hali iwe shwari waanzishe vurugu.
Kama ndiyo hivyo tufuge ‘paka’ inawezekana hiyo ikawa dawa nzuri ya
kumaliza tatizo hili.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment