Home » » WALIMU 200 WAVAMIA OFISI YA MKURUGENZI DAR

WALIMU 200 WAVAMIA OFISI YA MKURUGENZI DAR

Walimu wa Manispaa ya Kinondoni wakiandamana kudai malipo ya malimbikizo ya likizo na kupandishwa madaraja. Walimu hao walivamia ofisi za manispaa hiyo jijini Dar eas Salaam jana. PICHA: TRYPHONE MWEJI
Walimu karibu 200  wa shule za msingi na sekondari  wilayani  Kinondoni mkoani Dar es Salaam, jana walivamia  Mkurugenzi wa Manispaa hiyo ofisini, wakidai stahiki zao na utatuzi wa matatizo sugu yakiwamo malimbikizo ya mishahara, posho za safari, likizo na kupandishwa madaraja.
Wanadai stahiki hizo kwa miaka kadhaa  lakini wanapigwa danadana licha ya kuwasilisha malalamiko kwenye ofisi hiyo.

Kabla ya  kwenda kwa ofisi ya mkurugenzi, walianza msafara wa madai katika ofisi ya Chama cha Walimu ya (CWT) Kinondoni,  huku wakiutaka uongozi wa chama hicho kuwaeleza hatma ya madai yao ya miaka mingi.

Aidha, baada ya viongozi wa CWT kuwaeleza kuwa, wamekuwa wakiyawasilisha manispaa  bila utekelezaji, walimu hao waliamua kwenda ofisini kwa mkurugenzi kutaka utekelezaji.

Miongoni mwa madai yao ni uhamisho usiofuata sheria ikiwa ni pamoja na  kutolipwa stahiki zao, kutopandishwa madaraja na  pindi watokapo masomoni hunyimwa barua za kupandishwa cheo pasipo sababu za msingi.

Pia walimu hao wanalalamikia serikali kutogharamia mazishi  ya  wenzi  au watoto wao kama kifungu namba saba (q) cha kanuni za kudumu za watumishi wa umma kinavyoelekeza.

Sababu nyingine iliyowapeleka ofisini hapo ni kutaka kujua sababu za kupelekea  asilimia mbili ya mikopo yao kwa  Mkurugenzi wa Manispaa hiyo bila maelezo ya kisheria.

Walitaka kujua sababu za kutopewa fedha za masomo licha ya kwamba serikali imewaweka kwenye mpango wa kusomeshwa na inagharamia mafunzo yao.

Aidha, baada ya walimu hao kuwasili kwenye ofisi ya mkurugenzi huyo, walipokelewa na Afisa Mtumishi Mkuu, Godfrey Mugomi,  na mara madai hayo walipoyawasilisha, aliyapokea na kuwataka wayawasilishe kwa maandishi ili yafanyiwe kazi.

Mugomi alisema wameyapokea maelezo ya walimu kupitia viongozi wao wa CWT na kuwaomba wayalete ili ndani ya mwezi mmoja menejimenti iyapitie.

“Yapo mambo ambayo yanahusu Manispaa ya Kinondoni na mengine ni ya serikali kuu, kwa hiyo baada ya kutuletea ndani ya mwezi mmoja tutayafanyia kazi yale yaliyo ndani ya uwezo wetu, lakini yale ya ngazi za juu tutayaelekeza huko,” alisema.

Mugomi alisema  wapo baadhi ya walimu waliokwishalipwa posho za likizo  na kwamba awali walikuwa wanadai malimbikizo ya nauli lakini wamelipwa karibu Sh. milioni 410 na kwa upande wa masomo alisema  wanalipiwa kulingana na mahitaji.

Wanapohitajika wa sayansi wanapelekwa mafunzoni  huwa wanalipiwa masomo  lakini si kila anayetaka kwenda kusoma analipiwa.

“Uhamisho hauwezi kufanyika kama  hakuna fedha hivyo madai haya sijui kuwa yana mashiko, lakini  mwajiri anagharamia misiba ya wenza na watoto wao “ alisema.

Walimu walitishia kuwa endapo ndani ya mwezi mmoja Manispaa ya Kinondoni itashindwa kupata ufumbuzi na kuwalipa stahili zao wataandamana na kusisua kazi.

Wakuzungumzia kufaulu miongoni mwa wanafunzi wa shule za manispaa hiyo, walieleza kushangazwa na uongozi wao kuwa kimya bila kuwapa motisha wakati wanafunzi wamekuwa wakifanya vizuri kila mwaka.

Katibu CWT Kinondoni, Stephen Mnguto, akizungumza na gazeti hili alisema wamekubaliana na walimu hao kuwa, barua ya malalamiko itapelekwa Manispaa ya Kinondoni, Jumanne ijayo.

Alisema wanashangazwa na manispaa hiyo ambayo kwa mwaka imekuwa ikikusanya shilingi bilioni 40 inashindwa kugharamia kwa wakati  shilingi  milioni 500 kwa ajili ya likizo za walimu wake.

“Walimu walisema  wamechoka na kama haya yataendelea hawatasimamia uchaguzi mkuu ujao", alisema na kuongeza kuwa Kinondoni ina walimua 7,547 wa shule za msingi na sekondari.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa