Ni dhahiri mpambano wa kuwania urais ndani ya
CCM unazidi kunoga, ikiwa imebakia miezi michache kabla ya kupulizwa
rasmi kipenga.
Mmoja wa makada kutoka CCM waliotangaza nia ya
kuwania kiti hicho, January Makamba ameandikiwa kitabu kinachoeleza nia
yake hiyo.
Kitabu hicho pamoja na mambo mengine kinaeleza
mikakati ya mwanasiasa huyo kijana iwapo atapitishwa na chama chake ili
kuwania na hatimaye kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi kitaifa.
Katika kitabu hicho chenye kurasa 196, Makamba
ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mbunge
wa Bumbuli, Tanga anasema rais ajaye lazima awe na tafakuri pana na nia
ya kuendeleza nchi na siyo kuwa na kaulimbiu nyepesi za afya bure,
elimu bure zisizo na ufafanuzi ili kuwahadaa wananchi.
Kitabu hicho kilichoandikwa na mchambuzi na
mwandishi wa makala za siasa, Padri Privatus Karugendo kimebeba sera na
mikakati yake kiundani ya kuiongoza nchi iwapo atapatiwa dhamana na CCM
kugombea urais.
Katika kitabu hicho kinachoitwa, ‘Maswali na
Majibu 40: Mazungumzo na January Makamba kuhusu Tanzania Mpya’,
mwanasiasa huyo anasema uongozi hauishii kwa kauli za juu juu za
kuongeza ajira, kuboresha elimu kwani kila mtu anaweza kuyasema hayo.
Anamwonaje rais ajaye
Anasema katika tafakuri zake anaona rais ajaye
anatakiwa kuzitambua kwa kina changamoto za nchi yake na kuwa na
mikakati ya kuzitatua.
Changamoto hizo, Makamba anasema ni za kiuongozi
na utatuzi wake unategemea kiongozi mwenyewe, hulka, mtazamo wake na
usahihi wa uamuzi anaoufanya.
“Kuomba uongozi wa nchi siyo harakati binafsi na
wafuasi wako kupata vyeo. Ni dhamana kubwa ya kujenga mustakabali wa
nchi na kuwaunganisha Watanzania wote. Kwa hiyo, uamuzi wa kugombea
lazima uupe heshima na nafasi inayolingana na dhamana yenyewe,” anasema
Makamba kwenye kitabu hicho.
Anaongeza kuwa rais anatakiwa kuongeza kasi ya
kuondoa umaskini, kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali, vyombo vya
dola na mahakama na hayo yatadhihirika kwa vitendo vya kuchukua hatua
dhidi ya viongozi wabadhirifu, walarushwa na kudhibiti matumizi ya
Serikali.
Pia, Makamba anatumia fursa hiyo kuelezea mikakati yake kuhusu
kutatua matatizo ya elimu, kusimamia muungano, umoja, mshikamano na
upendo, kukuza ujasiriamali, umilikaji wa ardhi na unufaikaji wa
rasilimali kwa wananchi na jinsi alivyo tayari kuboresha hali hiyo.
Hoja ya ujana
Mwanasiasa huyo aliyeingia kwa mtazamo wa uongozi
wa kizazi kipya, anapoulizwa na mwandishi wa kitabu kuhusu mjadala
kuhusu umri na urais na kwa nini vijana waaminiwe kwa nafasi hiyo wakati
hawana uzoefu, anajibu kuwa haamini kuwa umri pekee ni sifa ya uongozi.
“Siamini kwenye dhana kwamba ukiwa mzee unafaa na
ukiwa kijana hufai, au ukiwa mzee hufai na ukiwa kijana unafaa. Ujana si
sifa na uzee si kashfa. Ujana si kashfa na uzee si sifa,” anasema.
Anabainisha kuwa wanapokubaliana umri si kigezo,
maana yake ni kwamba mwenye miaka 40 asionekane hawezi kutokana na miaka
yake, lakini anaongeza kuwa uongozi ni suala la rika. Anasema kila rika
au kizazi kina wakati wake, wajibu wake na ndiyo maana Mwalimu Julius
Nyerere aliamua kung’atuka urais akiwa na miaka 62 na siyo kwa kushindwa
kuongoza, bali kwa ajili ya kuachia rika na kizazi kingine kiendeleze
alipoishia.
“Uongozi ni kutengeneza kesho njema. Wenye kesho
nyingi hawapaswi kukaa pembeni na kukunja mikono na kuwaachia wenye jana
nyingi kazi ya kujenga kesho njema. “Wakifanya hivyo, uhakika wa kesho
njema unaweza usiwe mkubwa kwa sababu wenye jana nyingi wanaweza
kuhangaika na masaibu ya jana zao kuliko matumaini ya kesho,” anasema.
Uzoefu wa JK
Makamba aliyewahi kuwa mwandishi wa hotuba wa Rais
Jakaya Kikwete, anasema ushiriki wake katika kampeni za urais mwaka
2005, akiwa msaidizi wake na baadaye kufanya naye kazi Ikulu, ulimpatia
uzoefu mkubwa uliosadia kuyajua matatizo yanayowakabili Watanzania
karibu kila eneo la nchi.
“Nilijifunza pia kwamba matumaini wanayowekeza
Watanzania kwa viongozi wao ni makubwa na pale tunapowaangusha kwa kweli
tunatenda makosa.
“Nilijifunza kwa Kikwete kwamba unaweza kuomba
kura, kuelezea dira yako, fikra zako, sera na ilani ya chama chako bila
kutumia matusi, kejeli, ulaghai na lugha kali na bado ukafanikiwa,”
anasema Makamba katika kitabu hicho.
Anaongeza kuwa alipokuwa msaidizi wa JK wa kuandika hotuba,
alijifunza namna Serikali inavyoendeshwa kwa kuhimili msisukosuko wakati
wa vipindi vigumu na jinsi kiongozi wa juu anavyotakiwa kutotetereka.
Kwa mujibu wa Padri Karugendo, kitabu hicho ni
sehemu ya mradi walioubuni wa kutaka kuwafahamu vijana, hasa wale
waliochomoza kwenye medani za siasa na kushika nafasi za juu za uongozi
serikalini wakiwa na umri mdogo na kiu ya kuleta mabadiliko katika nchi.
Anasema Karugendo kuwa wataendelea kuuliza maswali
kwa kila kijana kutokana na umri wake na kwamba iwapo anayo miaka 40,
basi ataulizwa maswali 40, vivyo hivyo kwa yule mwenye miaka 55 au
zaidi.
Katika maswali hayo ya kichokozi, Makamba
aliulizwa na Padri Karugendo kuwa haoni kuwa CCM imepoteza mwelekeo na
inapata upinzani mkubwa na iwapo kuna sababu ya kuendelea kuaminiwa na
Watanzania?
Katika majibu yake, Makamba anasema ni kweli
ushindani umeongezeka na kwamba hali hiyo si ya ajabu kwa kuwa ndani ya
miaka 22 ya mfumo wa vyama vingi ni lazima ushidani ungetokea, ila
anapinga kuwa CCM imepoteza mwelekeo.
Anasema zipo changamoto kadhaa zilizo kawaida kwa
kila taasisi ambazo zitatatuliwa kwa kuwasemea na kuwatetea wanyonge,
kukemea rushwa na maovu katika chama chenyewe na kutekeleza ilani na
ahadi za CCM.
“Ni kweli kwamba chama kimeingiliwa na wajanja wachache ambao wanataka kununua uongozi kwa ajili ya kujinufaisha.”
Makamba, katika kitabu hicho ambacho dibaji yake
imeandikwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi au Mzee
Ruksa, anasema haoni mbadala wa CCM kwa sasa katika utayari wa uongozi
wa Taifa na kwamba amani, utulivu, umoja na maendeleo na salama ya nchi
ipo mikononi mwa CCM.
Akielezea namna ya kupunguza makali ya umaskini
kwa kukuza uchumi na ajira kwa vijana, Makamba anasema kuna haja ya
kuweka muswada maalumu wa matumizi kwa uwezeshaji kiuchumi kwa vijana,
utakaokuwa sheria maalumu ya matumizi ya Sh3.6 trilioni kwa ajili ya
miaka mitatu.
Anasema sheria hiyo itasaidia kupanua ajira kwa
kuchochea shughuli za uzalishaji mali na uchumi, zikiwamo kutoa motisha
kwa biashara kubwa na viwanda vitakavyoongeza ajira rasmi 50 za kudumu
kwa mwaka, pia kupunguza kodi ya mshahara (PAYE).
Dibaji ya Mwinyi
Katika dibaji kwenye kitabu hicho, Mzee Mwinyi anasema Makamba
anaonekana dhahiri ameandaliwa au amejiandaa vilivyo kuwa kiongozi
mkubwa wa nchi.
Mzee Mwinyi anasema kitabu hicho kimemfanya
amfahamu zaidi kiongozi huyo kuliko awali alipokuwa kama kiongozi ndani
ya chama na Serikali.
“Fursa ya kusoma mazungumzo yake imenisaidia kumfahamu zaidi kama mtu, pia fikra zake,” anasema Mzee Mwinyi.
Anaeleza kufarijika kwake kuona nchi na Rais
Kikwete wameendeleza utamaduni aliouanzisha Mwalimu Nyerere na
kuendelezwa naye wa kuwaamini vijana na kuwapatia fursa za uongozi ili
kuwaanda kuongoza nchi.
Kauli ya Makamba
Akizungumzia kitabu hicho, Makamba alisema jana
kuwa kilichoandikwa na Padri Karugendo kinaakisi mawazo yake na kwamba
amewasilisha vyema mazungumzo yao.
“Amefanya kazi nzuri na imechukua muda mrefu kama
mwaka mzima hivi. Kuna kipindi nilikata tamaa kwamba kitabu hakipo,
lakini hatimaye amekikamilisha,” alisema Makamba na kuongeza:
“Watu wanaotaka kunifahamu wakisoma kitabu hicho watanielewa January ni nani.”
Anahimiza wanasiasa wengine wafanye hivyo ili wananchi wawajue viongozi wao ili iweze kusaidia nchi kupata kiongozi bora.
“Wananchi wengi wanawajua viongozi wao kwa vyeo walivyoshika, lakini hawawajui kwa undani,”anasema.
Anapoulizwa kwamba haoni vipaumbele vilivyomo
kwenye kitabu hicho vinapingana na zuio la CCM kwa wanachama wake
kufanya kampeni za urais mapema, Makamba anajibu kuwa hivyo ni
vipaumbele vya Tanzania mpya na havihusiani na kampeni.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment