Mwanamuziki wa kundi la THT Lameck Ditto akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari.
Kama umewahi kusikia kuhusu kituo cha Tanzania House of Talent
(THT) na ukajua kwamba kinajishughulisha na uzalishaji wa vipaji vya
sanaa ya muziki, hivi sasa kituo hicho kimetangaza mwelekeo mpya baada
ya kutimiza miaka 10.
Shamra shamra hizo ambazo zimeanza kuadhimishwa
wiki hii na zitafikia kilele Desemba mwaka huu, zimekuwa na lengo
tofauti na ule wa awali ambapo sasa kituo hicho hakitapokea wanafunzi wa
sanaa ya uimbaji na dansa na badala yake kitaegemea upande wa ubunifu
wa mitindo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho
hayo, Meneja Mkuu wa Kituo hicho, Mwita Mwaikenda alisema ni heshima
kubwa kuweza kusherehekea miaka 10, wakiwa wamefanikisha mambo mengi
makubwa.
Mwaikenda alisema kituo hicho kinatarajia
kuadhimisha miaka 10 toka kuanzishwa kwake ifikapo Januari 30 mwaka huu,
hafla itakayofanyika Escape 1 jijini Dar es Salaam.
THT iliyoanzishwa mwishoni mwa mwaka 2005 ilikuwa
na lengo la kuwasaidia vijana wenye vipaji, lakini wasio na uwezo wa
kujiendeleza wenyewe katika sekta mbalimbali za sanaa.
“Tulianzisha kituo hiki tukiwa hatuna chochote
zaidi ya imani yetu kwa vijana walio na vipaji, tulianza hatuna chochote
lakini leo tumesaidia vijana zaidi ya 3,000 waliopita katika kituo hiki
kwa miaka 10, ambao wengi wao walikuwa ni watoto wa mitaani lakini leo
wanajimudu wao na familia zao,” alisema Mwaikenda.
Akielezea kuhusu mwelekeo wa kituo baada ya miaka
10, Mwaikenda alisema anaamini kituo kimefanya kazi yake tayari kwa
kuweza kuchagiza sanaa ya muziki nchini, na sasa ni wakati wa kuendelea
kusaidia wadau au vituo vingine kama Mkubwa na Wanawe kufika THT
ilipofika.
“Kimsingi mwaka huu ndiyo wa mwisho kuendela
kupokea wanafunzi wapya wa kuimba, na mpango wetu ni kuendelea kukuza
kituo kwa kuanzisha kampuni ya ushonaji na ubunifu wa nguo kwa kutumia
kitenge ambao tunaamini utatoa ajira kwa vijana wengi zaidi hapa
nchini,” alisisitiza Mwita.
Mwaikenda alisema kampuni ya ubunifu na ushonaji
kwa kutumia vitenge, tayari ishaanza mchakato wake kwa kuhusisha wadau
wa biashara ya vitenge na mbunifu mahiri Ally Remtullah, mwanamitindo
Flaviana Matata wakiwa ndiyo walezi na wasimamizi wa mradi, ambao
utaanza na wabunifu wanaochipukia Neyonce pamoja na Adam Mchomvu.
“Kwa kuanza mradi utapeleka wabunifu nchini China
ili wakajifunze zaidi juu ya ubunifu na kuongeza ubora kwenye kazi zao,
wakirudi tunaamini wataweza kuwafundisha vijana wengi zaidi na kutimiza
lengo letu la kuwasaidia vijana kujiajiri,” alimaliza Mwita.
Meneja Masoko wa THT, Michael Nkya alisema kituo
kililenga kusaidia watoto wa mitaani, lakini baadaye walijitokeza
wengine waliokuwa na uwezo katika vipaji vyao lakini wanahitaji
kuviendeleza na hatimaye kuingia katika shughuli za uratibu.
“Tulivyoanza si tulivyo sasa, kwani tunaratibu
matamasha mbalimbali kama Fiesta, mkutano wa Smart Partnership, Sensa ya
mwaka 2013, Sherehe za miaka 50 ya Muungano pamoja na mikutano,
matamasha kadha wa kadha,” alisema.
Alisema THT imeendelea kukua kwa kuweza kuanzisha studio yake
ambayo imeweza kurekodi matangazo, nyimbo za wasanii wote wa THT pamoja
na wengine wengi kama ‘Mdogo Mdogo’ na ‘Number One Remix’ ya Diamond,
‘Me and You’ ya Ommy Dimpoz, ‘Prokoto’ ya Victoria Kimani na nyingine
nyingi.
Nkya alisema kwa sasa THT inatengeneza vipindi
mbalimbali vya televisheni kama 69 Records, na vingine vinavyorushwa
chaneli za nje huku pia ikijivunia kuwa na maktaba ya nyimbo kubwa zaidi
nchini.
“Shukrani zetu za dhati kwa kweli ni kwa Serikali,
hasa hasa Mheshimiwa Rais Kikwete, ambaye toka mwanzo alikubali wazo na
akaamini muziki unahitaji elimu ya peke yake, pia kampuni mbalimbali
ambazo wamekuwa wakitupa kazi pamoja na vyombo vyote vya habari kwa
kutuunga mkono siku zote,” alisema Nkya.
Kituo hicho kimezalisha wasanii wengi sambamba na
dansa wakiwemo Mwasiti Almasi, Linah Sanga, Barnaba Elias, Mataluma,
Marlaw, Recho, Amini, Kadja Nito, Dito na wengine wengi.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment