Ilitosha kwa FM Academia kumweteka na umaarufu na uzoefu wao
mkubwa kwenye soko la muziki wa dansi na kudharau bendi nyingine
zinazojaribu kukaribiana nao, lakini haijavimba kichwa na badala yake
inaheshimu wapinzani wao wote.
“Bila ya kuwapo washindani, hakuna ambaye angeweza
kupima ubora wa bendi nyingine,” anasema kiongozi wa bendi hiyo
inayojumuisha wasanii wengi wenye asili ya Kongo, Nyoshi El Saadat.
“Kama ilivyo kwa timu (za mpira) na hata wagombea,
kwenye nafasi yoyote lazima kuwe na sababu ya kuwapo kwa ushindani,
ndiyo anatambulika nani bora.”
Nyoshi alifafanua kuwa wao wameliona hilo na kila
siku wanafanya kazi kupambana na ushindani uliopo sokoni na hata katika
kumbi za burudani, ikiwa ni pamoja na kuangalia watu wanataka nini.
“Bendi za muziki wa dansi zipo nyingi, hasa
zinazopiga kwa lengo la kuwateka vijana wapenda burudani, hivyo lugha ya
taifa ya FM Academia ni muziki wenye kiwango kwanza , mengine baadae,”
alisema mwimbaji huyo kiongozi wa FM Academia.
Bendi hiyo inakabiliwa na kibarua kigumu ya
kushinda ushindani kutoka bendi kama African Stars, maarufu kwa mtindo
wa Twanga Pepeta, Mashujaa, Malaika na Akudo Sound, ambazo pia
zinajumuisha wasanii mchanganyiko kutoka Tanzania na Kongo.
FM ilianzishwa mwaka 1997 na kundi la wanamuziki
kutoka FM Musica iliyokuwa chini ya Kampuni ya FM Bank ambao waliungana
na wanamuziki wengine waliokuwa pamoja jijini Nairobi kwenye bendi ya
Bogoss Musica.
Bendi hiyo imepata kutoa albamu 10 zilizopata mafanikio makubwa sokoni na kushinda tuzo za Kili Music Awards mara kadhaa.
Kwa mujibu wa Nyoshi, FM Academia kwa sasa
inatamba na nyimbo kama “Fataki”, “Otilia”, “Ndoa ya Kisasa”, “Neema”,
“Dai Chako Ulaumiwe”, “Maisha”, “Madudu”, “Miraessa” na “Intro” ambazo
zitakuwa kwenye albamu mpya.
Nyoshi alielezea siri ya mafanikio kwa miaka 18,
kuwa ni kuona mbele na kutambua mashabiki wanahitaji nini kwenye utitiri
wa bendi za muziki wa dansi uliopo sasa.
Alisema kuwa hapingi kuwapo na bendi nyingi
anafurahia kwani anaamini ni changamoto kwa viongozi na wamiliki wa
bendi kuwa makini wakitambua kuna wanaowakimbiza wakitaka kuwapora tonge
walilonalo mkononi.
Kiongozi huyo alisema kuwa haamini kuwa wingi wa bendi na muziki wa dansi kutopigwa redioni kunavunja umaarufu wa muziki huo.
Alisema kwa kawaida bendi mara nyingi huwa na mashabiki wake
ambao hupelekeana habari wanapokwenda kwenye shoo, hivyo kazi ya bendi
ni kuhakikisha mashabiki wanapoingia ukumbini wanapata wanachokitaka.
Alieleza kuwa mashabiki wakiburudika wanakuwa
mabalozi wazuri kuutangaza muziki kwa kuomba nyimbo redioni na kwenye
vituo vya runinga na wenye redio watalazimika kupiga ili kuwaridhisha
wateja wao.
Alizitaja changamoto za kuendesha bendi ikiwamo kuhakikisha wanamuziki wanaridhika na kubaki kwenye bendi kwa muda mrefu.
“Siku za hivi karibuni imeingia tabia ya
wanamuziki kupenda kuhamahama wakidhani watapata maslahi au wanaweza
kuwa wanayapata kweli. Hali hiyo imekuwa ikiyumbisha bendi nyingi, hivyo
changamoto kubwa ni kuwafanya waone umuhimu wa kubaki kwenye bendi yao,
” alisema Nyoshi
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment