Home » » MWAKYEMBE AELEZA ALIVYOITIMUA CCCC

MWAKYEMBE AELEZA ALIVYOITIMUA CCCC

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
 
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amefichua siri kwamba aliamua kuvunja mkataba kati ya serikali na kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC) Limited iliyopewa zabuni ya ua ujenzi wa gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam baada ya kubaini kulikuwa na utata katika gharama za ujenzi wa mradi huo ambao ungeigharimu serikali Dola za Marekani milioni 523 (Sh. bilioni 889.545).
Aidha, alisema alipoomba ushauri kwa mwanasheria kusitisha mkataba huo, alielezwa kuwa serikali ingeshitakiwa na kampouni hiyo, lakini aliamua kuusitisha kwa kuelewa kuwa hata kama kampuni hiyo itashtaki isingeweza kushinda kesi.

Akizungumza juzi katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, alisema: “Nilipoona ngoja nivunje mkataba, mwanasheria akasema hapa tutashitakiwa, nikamwambia mimi mwenyewe ni mwanasheria, nina uhakika kwa asilimia 99.9 wakienda kushtaki tutashinda kesi.”

Dk. Mwakyembe alisema tangu alipovunja mkataba huo, kampuni hiyo haijashtaki na kwamba hivi sasa zimekuja kampuni nyingine ambazo zitapewa kazi ya kujenga gati hizo ujenzi unaotarajia kuanza mwezi ujao.

Alisema alipoingia katika wizara hiyo kitu ambacho alikiona ni gharama kubwa za ujenzi wa mradi ambazo ujenzi wa gati hizo ilikuwa ni Dola za Marekani milioni 523.

Aliongeza kuwa kilichomshtua aliposafiri kwenda Singapore alielezwa kuwa ujenzi wa gati moja pamoja na vifaa vyote ni Dola za Marekani milioni 250 na aliporejea akaiambia kampuni ya CCCC ni kwanini inaigonga bei ya juu serikali katika ujenzi wa gati hizo.

Alisema kutokana na hali hiyo aliamua kuzipambanishwa kampuni katika ujenzi wa gati hizo na kampuni moja ilikubali kujenga kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 180.

Alisema kuwa suala la ujenzi wa gati hizo amekuwa akilieleza mara kadhaa bungeni na kwamba bado baadhi ya wabunge hawamwelewi na wapo waliomwelewa.

Dk. Mwakyembe alisema kipindi kampuni ya CCCC inaingia kwenye mkataba na serikali tayari ilikuwa imekataliwa na Benki na Dunia ambayo ilisema siyo kampuni ya kufanya nayo biashara kutokana na rushwa.

Alisema kampuni hiyo ilipokuja nchini haikuweka wazi suala hilo na hivyo kuingia mkataba na serikali wa ujenzi wa mradi gati namba 13na 14.

Kuhusu dawa za kulevya,  alisema hivi sasa viwanja vya ndege nchini siyo tena vichochoro vya kupitishia dawa hizo kama ilivyokuwa zamani, kutokana na udhibiti mkubwa.

Akizungumzia Shirika la Ndege Tanzania (ATC), alisema lilikubwa na vitendo vya ubadhilifu na kusababisha kuwapo kwa deni la Sh. bilioni 140.

Alisema hivi sasa serikali imeweka mkazo wa kuboresha miundombinu ya usafiri kwa kuviboresha viwanja vya ndege katika mikoa mbalimbali.

“Baadhi ya watu wamekuwa wakihoji kwa nini shirika la ATC halina ndege zake, lakini hawajui kwamba suala la kuwa na ndege siyo jambo kubwa la msingi hapa ni miundombuni, leo hii nikitaka ndege ni mara moja napata, lakini je, miundombinu ipo?” alihoji.

Mjadala uliibuka mwaka 2012 kuhusu ujenzi wa gati hizo hatimaye kung’olewa kwa aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu.

Kampuni hiyo  ilikuwa ikitetewa na uongozi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) uliofukuzwa kazi.

Ujenzi wa gati namba 13 na 14 ulisimama Septemba, 201.

 
SOURCE: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa