Zipo chaguzi aina mbalimbali zikiwemo za serikali za vijiji, mitaa, vitongoji, wajumbe wa viti maalumu, madiwani, wabunge na Rais.
Hapa nchini, uchaguzi mkuu hutanguliwa na uchaguzi wa serikali za mitaa na baada ya mwaka mmoja ndipo hufanyika uchaguzi mkuu wa madiwani wabunge na Rais unafuatia.
Hilo linajidhihirisha wazi hapa nchini ambapo Desemba 14, 2014 ulifanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwishoni mwa mwaka huu uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika.
Desemba 14, 2014, uchaguzi wa wenyeviti wa vijiji, vitongoji, mitaa, wajumbe wa halmashauri za vijiji na wajumbe wa kamati za mitaa na wajumbe wa viti maalumu ulifanyika.
Kwa mwaka huu, uchaguzi huo umeonekana kuwa na mvuto na hamasa kubwa kwa wananchi hususan kwa vyama vya siasa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi ), Jumanne Sagini anaelezea namna ambayo uchaguzi huo umeboreshwa tofauti na miaka ya nyuma.
Anasema miaka ya nyuma uchaguzi huo haukuwa hata na msimamizi huku akisema kuwa ulikuwa ni uchaguzi wa kienyeji.
“Huko nyuma hakukuwa hata na msimamizi,ulikuwa ni uchaguzi wa kienyeji kweli, wananchi walikuwa wanakutana wenyewe halafu wanasema fulani ndio atakuwa mwenyekiti wetu, hakuna hata kupiga kura.
“Hata hivyo, baadaye tukapiga hatua kidogo tukasema, sasa watu waandikishe wenyeviti wao kwa kura ya siri, tumetoka ngazi hiyo mwaka 2009 ‘tuka-advance’ zaidi, tukasema tuwe na karatasi nyeupe iliyogongwa muhari we halmashauri kusika ambayo anapewa mpigakura anayeorodhesha watu anaowataka wawe viongozi.
“Katika uchaguzi wa mwaka huu tukaona tuboreshe zaidi, tukaweka ‘ballot papers ‘ambazo zimetumika katika upigaji kura,” anasema Sagini
Anaongeza kuwa Watanzania kwa kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu isipokuwa kwa maeneo ya mijini ambayo anasema kulikuwa na vurugu kidogo.
Katibu mkuu huyo anafafanua uchaguzi ulifanyika vizuri na katika maeneo mengi hakukuwa na fujo ila changamoto ilitokea mijini ambako kuna baadhi ya maeneo watu walitaka waingie wote kuhesabu.
Anawataka Watanzania kujenga utamaduni wa kumpongeza anayeshinda bila kujali itikadi za vyama huku akisema kuwa katika uchaguzi wowote ni lazima kuwe washindi na watakaoshindwa.
Sagini anazitaka halmashauri nchini kutoa mafunzo kwa viongozi hao kwani wengine ni wapya katika uongozi.
Maeneo ambayo hayajafanya uchaguzi
Akitoa taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa, Kalist Luanda anasema bado kuna baadhi ya maeneo uchaguzi haujafanyika.
Anasema hiyo ni kutokana na mapingamizi ya kimahakama ambapo mahakama zilizuia mchakato wa uchaguzi kuendelea ikiwemo mikoa ya Singida na Mara.
Pia, anasema kuna baadhi ya maeneo, karatasi za orodha ya wapiga kura zilichomwa moto huku akitolea mfano wa eneo lililofanyika hivyo kuwa ni Manispaa ya Sumbawanga.
“Kuna maeneo ambayo wagombea wake walifariki siku ile ya uchaguzi na taratibu zinasema inapotokea hivyo, chama husika kinapaswa kupeleka mgombea mwingine.
“Kwa hiyo uteuzi unaanza hadi jina like lipite kwenye Chama, liteuliwe kisha mgombea afanyiwe kampeni ndipo uchaguzi ufanyike,” anasema Luanda
Hata hivyo, anasema maeneo ambayo bado hayajapandwa uchaguzi ni machache kiasi ambacho hayawezi kubadilisha asilimia ya chama chochote katika matokeo.
Matokeo ya jumla
Luanda anasema vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo ni 15 ambavyo ni CCM, Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi, TLP, NLD, ACT, UDP, APPT-Maendeleo, Chauma, NRA, DP, Tadea, UMD na ADC.
Anasema Tanzania Bara kwa sasa ina vijiji 12,443, Mitaa 3,875 na vitongoji 64,616 huku akisema kuwa matokeo yaliyopatikana ni asilimia 99 ya matokeo yote yaliyotakiwa kupatikana.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kati ya vijiji 12,443, vijiji vilivyotoa matokeo ni 11,750 huku akisema vijiji takribani 700 havijapeleka matokeo (uchaguzi bado).
Akitoa matokeo ya wenyeviti wa vijiji, Luanda anasema kati ya vijiji hivyo 11,750 , CCM kimepata vijiji 9,378 sawa na asilimia 79.81, Chadema vijiji 1,754 sawa na asilimia 14.93,CUF vijiji 516 sawa na asilimia 4.39.
NCCR-Mageuzi vijiji 67 sawa na asilimia 0.57, TLP vijiji 10 sawa na asilimia 0.09 NLD vijiji 2 sawa na asilimia 0.02, ACT vijiji 8 sawa na asilimia 0.07, UDP 14 sawa na asilimia 0.12, NRA kijiji 1 sawa na asilimia 0.001 na vyma vingine havijapa kura.
Vitongoji
Kwa upande wa wenyeviti wa vitongoji Luanda anasema kati ya vitongoji 64,616 matokeo yaliyopatikana ni ya vitongoji 60,688 ambapo Kati ya vitongoji hivyo CCM imepata vitongoji 48,447 sawa na asilimia 79.83.
Chadema vitongoji 9,145 sawa na asilimia ,CUF vitongoji 2,561 sawa na asilimia 4.22 ,NCCR Mageuzi vitongoji 339 sawa na asilimia 0.56.
TLP vitongoji 55 sawa na asilimia 0.09, NLD vitongoji 2 sawa na asilimia 0.02, ACT vitongoji 72 sawa na asilimia 0.12, UDP vitongoji 54 sawa na asilimia 0.09 na vyama vingine haikupata kura.
Mitaa
Luanda anasema hivi sasa kuna mitaa 3,875 huku akisema kuwa, mitaa yote imetoa matokeo yao na kwamba kati ya mitaa hiyo, CCM imepata mitaa 2,583 sawa na asilimia 66.66, Chadema mitaa 980 sawa na asilimia 25.29, CUF mitaa 266 sawa na asilimia 6.86, NCCR-Mageuzi mitaa 28 sawa na asilimia 0.72 .
Aidha, anasema TLP imepata mtaa mmoja sawa na asilimia 0.03, ACT mitaa 12 sawa na asilimia 0.31, UDP Mitaa 3 sawa na asilimia 0.08, NRA mtaa mmoja sawa na asilimia 0.03 na vyama vingine haijapata kura.
Kwa upande wa wajumbe wa serikali za vijiji na mitaa anasema kulikuwa na nafasi 125,169 ambapo CCM imepata wajumbe 100,436 sawa na asilimia 80.24, Chadema wajumbe 28,527 sawa na asilimia 14.8, CUF 5,395 sawa na asilimia 4.31 NCCR Mageuzi wajumbe 598 sawa na asilimia 0.48 .
Anasema TLP imepata wajumbe 62 sawa na asilimia 0.05 ,ACT wajumbe 106 sawa na asilimia 0.08 ,APPT Maendeleo mjumbe 1 sawa na asilimia 0.00,Chauma mjumbe 1 ,NRA wajumbe 4 na vyma vingine haikupata kura.
Kuhusu wajumbe wa Viti maalum Luanda anasema Kati ya wajumbe 80,537 CCM imepata wajumbe 66,147 sawa na asilimia 82.13,Chadema wajumbe 10,471 sawa na asilimia 13,CUF wajumbe 2,676 sawa na asilimia 3.32, NCCR Mageuzi wajumbe 455 sawa na asilimia 0.56.
TLP imepata wajumbe 63 sawa na asilimia 0.08,NLD mjumbe 1 sawa na asilimia 0.00001 ,ACT wajumbe 57 sawa na asilimia 0.057,UDP wajumbe 43 sawa na asilimia 0.05 ,APPT Maendeleo mjumbe 1 ,Chauma mjumbe 1 na vyama vingine havikupata kura.
Viongozi wote walichaguliwa katika uchaguzi huo ndio wasimamizi wa shughuli mbalimbali za maeneo husika ikiwemo shughuli za maendeleo na usimamizi wa miradi na kuhakikisha fedha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Halmashauri zinapaswa kutoa mafunzo kwa viongozi hao ili waweze kutimiza majukumu Yao kwa ufanisi zaidi.
0767-922165
Chanzo:Jambo Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment