Padri John Wootherspoon, raia wa Australia
ameeleza mikasa na visa mbalimbali vinavyohusiana na biashara ya dawa za
kulevya, vikiwamo vitisho na jinsi alivyozungumza na familia za
wafungwa wa Kitanzania waliokamatwa na dawa za kulevya na kufungwa Hong
Kong.
Hong Kong inatumiwa na Watanzania kama njia ya kupitisha dawa za kulevya kwenda China na nchi nyingine za mashariki ya mbali.
Wootherspoon, Padri wa Kanisa Katoliki ambaye kazi
yake ni kuwatembelea wafungwa katika magereza, kuwafariji na kueneza
neno la Mungu, amesema tangu alipofika nchini amekuwa akiwatahadharishwa
kuwa makini na watu wanaofanyabiashara ya dawa za kulevya.
“Nimeambiwa mara nyingi kuwa wanaweza kunitafuta
na kunidhuru, lakini sijaona chochote mpaka sasa na siogopi kwa kuwa
Mungu ananilinda,” alisema.
Mwandishi wa Mwananchi alikutana na Padri
Wootherspoon wakati anazitafuta familia zaidi ya 30 za Watanzania
waliofungwa Hong Kong baada ya kuwasiliana naye kwa njia ya barua pepe
tangu Novemba mwaka jana alipokuwa akipanga safari ya kuja nchini.
Padri huyo alizungumza na wanafamilia wa wafungwa
hao ambao waliandika ujumbe mfupi kwa ndugu zao kwa kuwa kila mfungwa
aliyeandika ujumbe aliweka namba ya simu ya ndugu yake.
“Niliwapa kitabu kidogo hiki kila mmoja alikitumia
kuandika ujumbe mfupi na namba ya simu, wafungwa wote hawakupata nafasi
ya kuandika kwa sababu wapo zaidi ya 130.
Padri huyo alifafanua kuwa ili kusafirisha dawa
hizo Watanzania hao humeza kete hizo na mtu mmoja anaweza kumeza hadi 90
za heroini (sawa na kilo 1.5).
Miongoni mwa wafungwa walioleta ujumbe wao ni
pamoja na msichana maarufu katika muziki wa Bongo Flevya, Binti Kiziwa
au Sandra Khan.
Sababu kubwa ya kusafirisha dawa za kulevya ambayo
wafungwa hao walimweleza Padri Wootherspoon ni umaskini na tamaa ya
fedha za haraka.
“Nilichogundua ni kuwa wengi wameshawishiwa bila
kujua madhara, walidanganywa kuwa ni rahisi zaidi kupenya katika
mipaka,” alisema.
Kadhalika alieleza kuwa wapo Watanzania wengi
China ambao ameshindwa kuonana nao kwa kuwa mtu aliyekamatwa na dawa za
kulevya nchi hiyo huhukumiwa kunyongwa.
“Niliwaruhusu kuandika barua ili wawakanye Watanzania wengine
wasibebe dawa za kulevya na hizo,” alisema huku akionyesha barua hizo.
Agawa fedha kwa familia
Baada ya kukutana na familia za wafungwa hao,
Padre Wootherspoon aligundua kuwa nyingi zinaishi katika hali ya
umaskini, jambo ambalo lilimlazimu kutoa fedha zake ili kuzisaidia.
Katika ziara hiyo, Padri huyo alitoa zaidi ya Sh6 milioni alizokuwa nazo na nyingine kutoka kwa wasamaria wanaoishi Hong Kong.
Familia zilizosaidiwa fedha nyingi zaidi ni za
watoto wa wafungwa wenye mahitaji ya ada, wazazi wanaoumwa na wake wenye
watoto wachanga.
Kwa mfano, mfungwa ambaye alikiri kuwa anaishi na
Virusi vya Ukimwi aliandika katika barua kuwa mama yake naye anaishi na
VVU wakati amemwachia mtoto mdogo.
Akutana na Nzowa
Akiwa nchini, Padri Wootherspoon alikutana na
Kamishna wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, ACP Godfrey Nzowa
na kuzungumza naye kuhusu vita ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.
Katika mazungumzo yao, Wootherspoon alimtaka Nzowa aende kuonana na wafungwa hao ili wamweleze siri nzito za biashara hiyo.
“Ni vyema ukaonane nao kwa sababu wanahitaji
faraja na watakupa mengi wanayoyajua kuhusu biashara hii. Kwa sasa
wanajutia walichokifanya, hivyo watakuwa radhi kukupa ushirikiano,”
alisema Padri Wootherspoon.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Hata hivyo, Nzowa alipinga uamuzi wa wafungwa hao kutaja majina
ya magwiji wa biashara ya dawa za kulevya katika barua na kuweka katika
tovuti kwa kuwa wanahatarisha maisha yao badala yake wangewasiliana
naye.
Padri Wootherspoon alizaliwa miaka 68 iliyopita,
baada ya kupata upadri alihamia Hong Kong ambako amefanya kazi kwa miaka
25 akiwahudumia wafungwa.
ChanzoMwananchi
ChanzoMwananchi
0 comments:
Post a Comment