Sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow jana liliendelea kuibua
mapya baada ya vigogo watatu kutoka Benki Kuu (BoT), Mamlaka ya Mapato
(TRA) na Shirika la Umeme (Tanesco) kufikishwa mahakamani wakikabiliwa
na mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa.
Kufikishwa mahakamani kwa watu hao watatu
kunafanya jumla ya watu waliopandishwa kizimbani kufikia watano baada
yaw engine wawili kutinga mahakamani mapema wiki hii.
Waliofikishwa Mahakama ya hakimu Mkazi wa Kisutu
jana ni meneja misamaha ya kodi wa TRA, Kyabukoba Leonard Mutabingwa,
mwanasheria mwandamizi wa Tanesco, Steven Roman Urassa na mkurugenzi wa
fedha wa BoT, Julius Rutta Angello, ambao wote kwa pamoja wanatuhumiwa
kuomba na kupokea jumla ya Sh1.923 bilioni zinazohusishwa na fedha
zilizokuwa Akaunti ya Tegeta Escrow.
Wote walisomewa mashtaka ya kuomba na kupokea
rushwa ya mamilioni ya fedha kutoka akaunti hiyo, kinyume na kifungu cha
15 (1)(a) cha Sheria ya Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2015.
Walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda na Devotha Kisoka
Mahakama ya Kisutu jana
Akisoma hati ya mashtaka katika kesi namba 16 ya
2015 dhidi ya Kyabukoba, mwendesha mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai
alidai mbele ya Hakimu Kaluyenda kuwa Januari 27, 2014 katika Benki ya
Mkombozi wilayani Ilala , alipokea Sh1.6 bilioni kupitia akaunti namba
00110202613801.
Swai alidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya fedha
za Akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba alipewa na James Burchard
Rugemalira, ambaye ni mshauri wa kitaalam, mkurugenzi wa kampuni ya VIP
Engineering na mkurugenzi wa zamani wa IPTL. Alisema alipewa fedha hizo
kama tuzo kwa kuiwakilisha mahakamani kampuni ya Mabibo Beer, Wines and
Spirits ambayo ni mali ya Rugemalira, kitu ambacho ni kinyume cha
sheria.
Alidai kuwa Julai 15, 2015, Kyabukoba akiwa benki
hiyo ya Mkombozi alipokea rushwa ya Sh161.7 milioni, Agosti 26,2014
alipokea tena rushwa ya Sh 161.7 milioni na Novemba 14, 2014 alijipatia
Sh161.7 milioni kupitia kwenye akaunti hiyo, ikiwa ni tuzo kwa
kuiwakilisha kampuni hiyo ya Rugemalira.
Kyabukoba alikana mashtaka hayo na upande wa
mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na akaomba
ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya
awali (PH).
Pia aliiomba mahakama kuzuia akaunti inayodaiwa kutumika kuchota
fedha hizo kwa muda hadi hapo kesi ya msingi itakapoamuliwa na kutolewa
uamuzi, ombi ambalo Hakimu Kaluyenda alikubaliana nalo.
Hakimu Kaluyenda alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na
wadhamini watatu wanaoaminika na wawili kati yao wawe watumishi kutoka
taasisi inayotambulika kisheria na mwingine awe na barua inayoaminika na
pia kila mmoja kusaini hati ya dhamana ya maneno yenye thamani ya Sh340
milioni na kwa upande wa mshtakiwa kutoa Sh1 bilioni taslimu ambayo ni
nusu ya fedha anazodaiwa kupokea kama rushwa, au hati ya mali
isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Pia alitazuiwa kutoka Dar es Salaam bila ya kuwa
na kibali cha mahakama. Mshtakiwa huyo alishindwa kukamilisha masharti
hayo na kupelekwa rumande hadi Januari 29, 2015, siku ambayo atasomewa
maelezo ya awali (PH).
Katika kesi namba 15,2015, inayomkabili Angello wa
BoT iliyokuwa mbele ya Hakimu Kisoka, ilidaiwa kuwa Februari 6, 2014
katika benki hiyo, mtuhumiwa alipokea rushwa ya Sh161.7 milioni kupitia
akaunti namba 00120102646201 ambazo aliomba na kupokea zikiwa sehemu ya
fedha za escrow.
Swai alidai kuwa fedha hizo zilikuwa tuzo kwa
kufanikisha malipo yaliyotolewa katika Akaunti ya Tegeta Escrow na fedha
hizo kulipwa PAP, jambo ambalo lilikuwa ni kinyume na mwajiri wake.
Angello alikana mashtaka na upande wa mashtaka
ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na akaomba ipangiwe
tarehe nyingine kwa ajili ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali,
lakini akaomba mahakama pia izuie akaunti yake, maombi ambayo
yalikubaliwa.
Hakimu Kisoka alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na
wadhamini wawili wanaominika, mmoja kati yao awe mtumishi wa serikali
na kila mdhamini asaini dhamana ya Sh50 milioni, ikiwa ni masharti ya
dhamana.
Pia alimtaka mshtakiwa huyo kutoa fedha taslimu Sh
80.8 milioni kiasi ambacho ni nusu ya fedha ambazo anatuhumiwa kupokea
kutoka kwa Rugemarila ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani
hiyo.
Hakimu Kisoka aliiahirisha kesi hiyo hadi Januari 27,2015 na mshtakiwa aliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Katika kesi namba 14/2015 inayomkabili Urassa wa
Tanesco, Swai alidai kuwa Februari 14,2014 mshtakiwa huyo akiwa benki
hiyo aliomba na kupokea rushwa ya Sh 161.7 milioni kutoka katika Akaunti
ya Tegeta Escrow.
Swai alidai kuwa siku hiyo, mshtakiwa huyo
alipokea kiasi hicho kupitia akaunti namba 00120102658101 na kwamba
zilikuwa sehemu ya fedha za escrow zilizotoka kwa Rugemalira, ikiwa ni
tuzo kwa kuiwakilisha Tanesco na kampuni nyingine iliyoingia nayo
mkataba mahakamani.
Kama ilivyokuwa kwa wengine, Swai alidai kuwa upelelezi umekamilika, na hivyo mshtakiwa atasomewa maelezo ya awali Februari 11
Hakimu Kaluyenda aliyeisikiliza kesi hiyo pia, alimtaka
mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na mshtakiwa
awasilishe Sh81 milioni taslimu mahakamani mahakamani hapo ama mali
isiyohamisha yenye thamani hiyo. Mshtakiwa huyo alitimiza masharti.
Kashfa hiyo ya Akaunti ya Tegeta Escrow
iliyoibuliwa na Bunge iliitikisa nchi na hadi sasa imesababisha Profesa
Anna Tibaijuka kuvuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
kutokana na kuingiziwa Sh1.6 bilioni na Rugemarila.
Pia, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
Jaji Frederick Werema alijiuzulu kwa maelezo kuwa ushauri wake kuhusu
kodi iliyotakiwa kukatwa kwenye fedha hizo, haukueleweka na badala yake
ulizua tafrani.
Pia katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi amesimamishwa kazi kwa uchunguzi.
Katika uamuzi wake, Bunge liliagiza watuhumiwa
wote wa kashfa hiyo, akiwamo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, ambaye bado ameachwa kiporo na Rais Jakaya Kikwete, na
wenyeviti wa kamati za Bunge za kisekta wawajibishwe.
Hao ni pamoja na Andrew Chenge anayeongoza Kamati ya Bunge ya Bajeti aliyedaiwa kupokea Sh1.6 bilioni kutoka akaunti hiyo.
Pia, William Ngeleja (Kamati ya Sheria na Katiba)
aliyepokea fedha, Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), ambaye pia
alikuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco.
Hali kadhalika, tayari watumishi kadhaa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamesimamishwa kutokana na kashfa hiyo
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment