MAKAMU wa Rais Dkt.
Mohamed Gharib Bilal, amewataka Watanzania wasikubali kuchagua viongozi
wanaotoa rushwa ili kutaka uongozi katika Uchaguzi Mkuu badala yake
wachague viongozi wenye maadili na hofu ya Mungu.
Dkt. Bilal aliyasema
hayo juzi kwenye mkesha maalumu wa kuliombea Taifa amani na kukaribisha
mwaka mpya wa 2015 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Alisema mwaka 2015
Taifa litafanya Uchaguzi Mkuu hivyo ni vyema Watanzania wakatumia fursa
hiyo kuchagua viongozi ambao wataendeleza amani na utulivu wa nchi.
“Ndugu zangu
Watanzania, taifa letu limekuwa na amani, utulivu kwa kipindi kirefu
tangu uhuru hivyo tusikubali kikundi cha watu wenye uchu wa madaraka
waivuruge amani yetu.
“Serikali itaendelea
kuilinda amani tuliyonayo kwa gharama yoyote ili Watanzania waendelee
kuishi kwa amani katika nchi yao... nawaomba mshiriki kikamilifu katika
mchakato wa kupata Katiba mpya Aprili 30, mwaka huu kwa kuipigia kura ya
ndiyo Katiba Inayopendekezwa,” alisema.
Baadhi ya viongozi
walioshiriki katika tamasha hilo ni pamoja na Waziri wa Uchukuzi, Dkt.
Harrison Mwakyembe, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Mecky
Sadiki, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Bi. Sophia Mjema na wengine.
Wakati huo huo, Askofu
wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, mkoani Kagera, Mhashamu Deusderius
Rwoma, ameitaka Serikali isambaze Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa kwa
wananchi ili waisome na kuielewa kabla ya kuipigia kura.
Alisema katiba hiyo
ikisambazwa, wananchi wanapaswa kuisoma na kuielewa pamoja na kuwataka
waumini wa kanisa hilo, kuliombea Taifa ili mchakato huo uweze
kukamilika salama kwa amani na utulivu.
Askofu Rwoma alisema hayo juzi kwenye misa ya mkesha wa mwaka mpya iliyofanyika Kanisa Kuu, Jimbo la Bukoba.
“Waumini mnapaswa
kumshukuru Mungu kwa mazuri yote aliyowafanyia mwaka 2014... kuna watu
ambao walitamani kuuona mwaka 2015 lakini hawakuweza,” alisema.
Aliwaomba waumini
kuyaombea makundi maalumu ya watu wenye shida na kuwatembelea wakiwemo
yatima, wagonjwa na wafungwa ili kuwafariji.
Wakati huo huo, Watanzania wote wameshauriwa kufanyakazi kwa bidii mwaka 2015, kuungama na kumrudia Mungu.
Msaidizi wa Askofu wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini
Magharibi, Mchungaji Remy Rwankomezi, aliyasema hayo juzi katika ibada
ya mkesha wa mwaka mpya katika Kanisa la Kengele Tatu, Bukoba.
Chanzo:Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment